Lissu aibua jipya kuhusu mashahidi wa Jamhuri

Dar es Salaam.  Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameibua hoja mpya dhidi ya mashahidi wa Jamhuri wanaotarajiwa kutoa ushahidi katika kesi ya uhaini inayomkabili, akidai kuwa ni hawastahili kisheria kufika mahakamani kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo.

Lissu ameibua madai hayo leo Jumanne, Septemba 16, 2025, katika mwendelezo wa usikilizwaji wa pingamizi lake kuhusiana na uhalali wa kesi hiyo.

Hii ni sababu ya mpya aliyoiongeza leo katika sababu za awali za pingamizi lake hilo na kufanya kuwa na sababu tatu za kupinga kesi hiyo.

Katika hoja zake Lissu amesema kuwa mashahidi hao wa Jamhuri walioorodheshwa hawastahili kisheria kutoa ushahidi wao katika kesi hiyo, kwa kuwa maelezo ya ushahidi wao yaliyowasilishwa mahakamani ni batili kutokana na kuandaliwa kinyume cha sheria.

Akihitimisha hoja zake za kupinga kesi hiyo ameieleza Mahakama kuwa ameonewa kwa kuwa hana hatia na hajamkosea mtu yeyote bali ameshtakiwa na kukaa mahabusu muda wote mpaka sasa kwa kosa lisilokuwepo.

Hivyo ameisihi Mahakama kukomesha huo anaodai ni uonevu dhidi yake, kwa kutenda haki.

Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:-

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”

Kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali Septemba 8, 2025, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na jopo la Majaji watatu, Dunstan Ndunguru (kiongozi wa jopo) James Karayemaha na Ferdnand Kiwonde.

Hata hivyo Lissu aliibua pingamizi akiiomba mahakama hiyo isiisikilize kesi hiyo bali iifute akitoa sababu mbili, Mosi ubatili wa hati ya mashtaka na mamlaka ya mahakama.

Mahakama ilielekeza kusikiliza kwanza sababu ya  ambayo mahakama hiyo jana Jumatatu, Septemba 15, 2025 ilitoa uamuzi ambapo iliitupilia mbali sababu ya Mahakama kutokuwa na mamlaka ya kuisikiliza.

Baada ya uamuzi ndipo Lissu akaanza hoja ya ubatili wa hati ya mashtaka ambayo ameendelea nayo leo huku akiibua sababu hiyo mpya ya tatu ya pingamizi kuwa maelezo ya mashahidi hao yaliyosomwa katika Mahakama ya Ukabidhi (committal court), Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu ni batili.

Kuhusu hoja hiyo amedai kuwa maelezo ya mashahidi 10 ambao ni maofisa wa Polisi yana kasoro za kisheria kwa  kuwa wameandika maelezo yao wao wenyewe na wamejionya wenyewe na wamejithibitisha wenyewe, wakati utaratibu unataka waende kuthibitishwa mbele ya ofisa mwingine wa Polisi.

Lissu amedai Mahakama Kuu ilitoa amri ya kulinda mashahidi ambao sio maofisa wa Polisi kwa kuficha anuani zao, makazi yao, ndugu zao na ajira zao, lakini katika maelezo ya mashahidi niliyopewa, amri hiyo ya kuwaficha mashahidi haikutekelezwa kwani kuna baadhi mashahidi wamewekwa hadi namba za simu.

Lissu amefafanua kuwa mashahidi hao wameonekana kufichwa majina yao tu, lakini anuani za makazi, ndugu zao, ajira zao taasisi wanazotoka hazijafichwa na hivyo inaweza kupelekea kutambuliwa.

“Hivyo nina maelezo ya mashahidi ambao yamekiuka sheria na amri ya Mahakama Kuu, iliyotolewa katika kulinda mashahidi” amedai.

Amedai kuwa kifungu 195(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), kinasema maelezo hayo yanayopaswa kufutiliwa mbali kwa kuwa yana kasoro zisizoweza kurekebishika.

“Nawaomba majaji mfute uonevu huu vyovyote itakayokuwa kwa haya niliyosema naombeni mfute uonevu huu, mimi ni mtu ambaye sina hatia, sijakosea mtu yoyote, leo ni siku ya 162 nipo rumande,”amedai Lissu.

Amehitimisha kwa kusema kwa majumuisho ya hoja zake zote kuwa ameionesha Mahakama hati ya mashtaka ina kasoro za kisheria zisizorekebishika, kwa kutoonesha kosa si tu la uhaini bali hata la jinai ya aina yoyote.