Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Manyara imebatilisha uamuzi uliowaachia huru Meja Gidarge na Hussein Ally waliokuwa wameshtakiwa kwa kosa la kumiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria na kuwatia hatiani kwa kosa hilo.
Juni 10, 2024 katika eneo la Kambini Kijiji cha Gijedaboung, Wilaya ya Babati mkoani Manyara, watu hao walidaiwa kukutwa na meno ya tembo matano na vipande vitatu ambayo yalikuwa sawa na tembo wanne waliouawa bila kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori na watuhumiwa walishitakiwa Mahakama ya Wilaya ya Babati.
Hukumu hiyo iliyobatilisha uamuzi huo wa mahakama ya chini, imetolewa Septemba 12, 2025 na Jaji Devotha Kamuzora, aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo.
Jaji Kamuzora amesema baada ya kupitia mwenendo, sababu za rufaa amejiridhisha kuwa mahakama ya chini ilikosea kuwaachia huru wajibu rufaa hao na kuwa kesi dhidi yao ilithibitishwa hivyo mahakama hiyo inawatia hatiani.
Rufaa hiyo ilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji, Jamhuri iliwakilishwa na Wakili Leonce Bizimana, ambaye aliieleza mahakama kuwa hawakuweza kuwapata wajibu rufaa kupitia anwani zao.
Aliieleza mahakama kuwa notisi ya wito mahakamani ilichapishwa mara tatu katika gazeti la Mwananchi lakini hawakutokea, hivyo usikilizwaji wa rufaa hiyo uliendelea bila ya wajibu rufaa kuwepo, chini ya kifungu cha 403 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Katika rufaa hiyo Jamhuri iliyopinga hukumu iliyowaachia huru watu hao wawili, ambapo aliwasilisha sababu sita ikiwemo Hakimu alikosea kwa kushikilia kuwa shtaka hilo halikuthibitishwa na upande wa mashtaka pasipo kuacha shaka.
Nyingine ni hakimu alishindwa kutathmini ipasavyo na kuchambua ushahidi uliotolewa, h alikosea kushikilia kuwa kulikuwa na mkanganyiko kwenye ushahidi wa mashtaka, alikosea kushikilia kuwa shahidi wa saba alikuwa wa ajabu.
Sababu nyingine ni hakimu alikataa kimakosa kupokelewa kama kielelezo, amri ya upekuzi na cheti cha ukamataji hivyo alikosea kisheria kusema kuwa kesi dhidi ya wajibu rufaa ni ya uzushi.
Wakili alieleza kuwa katika kesi hiyo amri ya upekuzi ilitolewa chini ya kifungu cha 38 cha CPA kinachotoa mamlaka hayo kwa Ofisa wa kituo cha Polisi (OCS), na kuwa mahakama ya chini ilijielekeza vibaya kwa kushindwa kupokea amri ya upekuzi na cheti cha ukamataji.
Aliieleza mahakama kuwa ni kanuni kwamba kutotumwa kwa amri ya upekuzi kwa hakimu kunaweza kutibika chini ya kifungu cha 388 cha CPA, ikiwa hakuna ushahidi wa ukiukwaji wa haki.
Kuhusu uchambuzi wa ushahidi, wakili huyo alieleza kuwa maelezo ya wajibu rufaa yalikubaliwa mahakamani yakionyesha kuwa walikiri kosa, lakini ushahidi huo haukuzingatiwa na mahakama ya chini katika uamuzi wake.
Wakili huyo alieleza ushahidi bora katika kesi ya jinai ni kukiri kosa lililotolewa kwa hiari na mshtakiwa, na kuwa maelezo ya onyo ya wajibu rufaa yalikuwa ushahidi muhimu ambao ungeweza kuwatia hatiani, hivyo kushindwa kuzingatia ilikuwa ni tathmini isiyofaa ya ushahidi.
Wakili huyo alieleza kuwa kosa la kumiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria lilithibitishwa bila shaka.
Jaji Kamuzora amesema kabla hajaenda kwenye uhalali wa kukata rufaa anaanza kutaja utofauti uliopatikana katika uamuzi wa mahakama iliyosikiliza kesi hiyo ambapo amenukuu sehemu ya uamuzi huo kama ifuatavyo;
“Ni kwa sababu hizo naona washtakiwa wote ambao ni Meja Gidarge Washing na Hussein Ally walioshitakiwa kwa pamoja katika kesi hii hawakupatikana na hatia ya kumiliki nyara za Serikali kinyume na kifungu cha 86 (1) na (2) (b) cha Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori,”
“Na aya ya 14 ya jedwali la kwanza na vifungu vya 57(1) na 60 (2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupanga (EOCCA). Ninaendelea kuwatia hatiani ipasavyo Kifungu cha 235 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai,” amenukuu Jaji Kamuzora sehemu ya uamuzi huo.
Jaji Kamuzora amesema hakimu katika hitimisho lake kueleza kuwa hajawatia hatiani, huo ni ukiukwaji unaoathiri uamuzi wa mahakama.
Akirejea sababu za rufaa Jaji huyo amesema wakili wa Jamhuri aliomba mahakama hiyo ifanye tathmini upya ya ushahidi, kufuta hukumu iliyowaachia huru wajibu rufaa hao kisha iwatie hatiani na kuwahukumu.
Jaji Kamuzora baada ya kuchunguza kwa kina mwenendo na hukumu ya mahakama hiyo, alieleza kukubaliana na wakili wa mrufani kuwa licha ya kuchambua ushahidi huo, mahakama hiyo haikutathmini ipasavyo na kutoa uzito kwa kila ushahidi kabla ya kufikia tamati.
Jaji amesema kwa sababu kuhusu hoja ya mkanganyiko wa ushahidi wa upande wa mashtaka, amepitia upya ushahidi kwenye kumbukumbu ili kutathmini kama kulikuwa na mikanganyiko hiyo.
Kuhusu ushahidi wa maelezo ya onyo ya wajibu rufaa, Jaji Kamuzora amesema hakimu alishindwa kuzingatia ushahidi huo bila kutaja sababu na kuwa rekodi inaonyesha maelezo hayo ya onyo yalikubaliwa, ila hakuna mahali popote katika hukumu hakimu aliporejelea ushahidi huo kwa kuupa uzito au kuudharau.
Baada ya kuchambua sababu zote Jaji Kamuzora alihitimisha kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha pasipo shaka kuwa wajibu rufaa walikutwa na nyara hizo za Serikali kinyume cha sheria, hivyo hakimu angezingatia na kuupa uzito ushahidi kwa ujumla wake angefikia hitimisho tofauti.
“Kwa hivyo ninapata uhalali katika sababu zote za kukata rufaa. Ushahidi wa upande wa mashtaka ulithibitisha kosa dhidi ya wajibu rufaa pasipo shaka, kwa hiyo uamuzi wa mahakama ya chini unatenguliwa na kuwekwa kando. Mahakama hii inawatia hatiani Meja Gidarge na Hussein Ally, kwa kumiliki nyara ya Serikali kinyume cha sheria.”
Jaji Kamuzora aliwatia hatiani chini ya kifungu cha 86 (1) na (2) (b) cha Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori na aya ya 14 ya jedwali la kwanza na vifungu vya 57(1) na 60 (2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupanga (EOCCA).