MUDA mchache kabla ya mchezo wa Ngao ya Jamii unaozikutanisha Yanga dhidi ya Simba, kuna presha iliibuka kwa mashabiki wa pande zote.
Tukianza na Yanga, mashabiki wengi walianza kutishwa na taarifa kwamba kiungo wao fundi, Pacome Zouzoua hatakuwa sehemu ya mchezo huo.
Hiyo ilitokana na Pacome kutoonekana kucheza mechi ya kilele cha Wiki wa Mwananchi dhidi ya Bandari, zaidi ya kupita mbele ya mashabiki wa timu hiyo kwenye utambulisho.
Kiungo huyo aliibuka wasiwasi zaidi kwani hakuonekana hata kupasha misuli wakati Yanga inaipiga Bandari ya Kenya bao 1-0, kama ilivyokuwa kwa mshambuliaji Clement Mzize.
Mashabiki wa Yanga walianza kutishwa wakiona kama timu yao itayumba wakimkosa raia huyo wa Ivory Coast.
Presha ya kumkosa Pacome ilichagizwa zaidi na kauli ya kocha wa Yanga, Romain Folz ambapo akizungumza mapema jana mbele ya waandishi wa habari, alisema: “Tuna majeruhi ndio, lakini hapa sio sehemu salama kusema nani tunaweza kumkosa.”
Kauli hiyo ya Folz ndio iliwajaza presha mashabiki wa timu hiyo, wakiona Pacome na Mzize wanaweza kukosekana kutokana na kuwa majeruhi.
Wakati hali ikiwa hivyo Yanga, kule Simba nako kuna presha kama hiyo ilitokana na taarifa kwamba kiungo wao mpya mwingine Allasane Kante ataukosa mchezo huo.
Itakumbukwa mapema mashabiki wa Simba, walishahakikishiwa kwamba, kiungo Mkenya Mohammed Bajaber, ataukosa mchezo huo kutokana na jeraha la nyama za paja.
Mashabiki wa Simba hapa uwanjani kabla ya kikosi hakijatangazwa, walishaanza kupata presha wakisikia uvumi kwamba, Kante naye ataukosa mchezo huo kutokana na shida kama hiyo.
Mapema tu Simba ilithibitisha juu ya kukosekana kwa Bajaber pekee lakini Kante ambaye alicheza dakika za mwisho kwenye mechi dhidi ya Gor Mahia katika Tamasha la Simba Day, ikiwa bado haijathibitishwa.
Mbali na wawili hao, Simba pia itamkosa mshambuliaji mpya Jonathan Sowah ambaye anatumikia adhabu ya kusimamishwa kikanuni, baada ya raia huyo wa Ghana, kupata kadi nyekundu kwenye Fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) msimu uliopita alipokuwa Singida Black Stars.
Presha hiyo ilikuja kuzimwa baada ya vikosi vya timu zote kutangazwa ikiwa ni takribani saa 1 kabla ya mchezo kuanza.
Katika vikosi vilivyotajwa, Pacome ameanza ndani ya Yanga na Mzize akiwa benchi, huku Kante naye akianza kule Simba.
Kikosi cha Yanga: Djigui Diarra, Israel Mwenda, Chadrack Boka, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Aziz Andabwile, Prince Dube, Mudathir Yahya na Pacome Zouzoua.
Benchi kuna Aboutwalib Mshery, Bakari Mwamnyeto, Abubakar Nizar ‘Ninju’ Mohamed Hussein, Abulnassir Mohammed ‘Casemiro’, Moussa Balla Conte, Lasine Kouma, Mohamed Doumbia, Celestine Ecua na Clement Mzize.
Kikosi cha Simba: Moussa Camara, Shomari Kapombe, Naby Camara, Abdulrazack Hamza, Rushine De Reuck, Yusuf Kagoma, Kibu Denis, Alassane Kante, Steven Mukwala, Jean Charles Ahoua na Elie Mpanzu.
Benchi kuna Yakoub Suleiman, Ladack Chasambi, Anthony Mligo, Chamou Karaboue, Wilson Nangu, Mzamiru Yassin, Neo Maema, Seleman Mwalimu, Morice Abraham na Joshua Mutale.