Dar es Salaam. Utekelezaji wa matumizi ya mfumo wa malipo ya papo kwa papo (TIPS) na matumizi ya msimbo namba (QR code) unaofahamika kama TANQR, umetajwa kuwa sababu ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutunukiwa tuzo kuu ya ubunifu katika huduma jumuishi za fedha.
Tuzo hiyo ijulikanayo kama Nestor Espenilla Jr. Financial Inclusion Innovation Award, imetolewa na Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha (AFI), yenye nchi wanachama 84, ikilenga kutambua nchi wanachama wa AFI ambao wameonyesha juhudi kubwa katika ubunifu na matumizi ya teknolojia.
Ripoti ya takwimu za utafiti wa huduma za fedha (Finscope) za mwaka 2023 zinaonyesha kuwa ujumuishi wa kifedha nchini umefikia asilimia 76, na katika kiwango hicho benki zikichangia asilimia 22 pekee.
Akizungumza na wanahabari, leo Septemba 16, 2025, Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa wa BoT, Lucy Shaidi amesema tuzo hiyo pia inatambua uongozi imara katika kuchochea kasi ya upatikanaji na matumizi ya huduma jumuishi za fedha.
“Utekelezaji madhubuti wa mfumo wa malipo ya papo kwa papo yaani TIPS na namna ambavyo umesaidia kupunguza gharama kwa wananchi kufanya miamala kwa njia ya kidigitali, ni moja ya mambo ambayo yamechangia sisi kushinda tuzo hii,” amesema.
Pia mafanikio katika matumizi ya msimbo milia wa malipo, TANQR, unaowezesha wafanyabiashara nchini kupokea malipo ya bidhaa na huduma kwa njia rahisi kutoka kwa benki na kampuni za simu, ni sababu nyingine.
“Mchango wa Benki Kuu kwenye ubunifu huu umeonekana katika machapisho mbalimbali duniani ambayo Benki Kuu iliyafanya juu ya mfumo wa TIPS na TANQR.
Pia Benki Kuu imekuwa mstari wa mbele katika kugawa ujuzi kwa nchi nyingine kwenye ubunifu huu ikiwemo nchi za Kenya, Lesotho, Rwanda na Uganda,” amesema.
Mafanikio hayo ya ubunifu yamewezesha kuwapo kwa ongezeko la miamala kwa mwaka wa fedha 2024/25 hadi kufikia milioni 560, yenye thamani ya Sh41 trilioni huku miamala inayotumia msimbomilia na LipaNamba ilifikia milioni 60 ikiwa na thamani ya Sh4 trilioni.
Meneja Msaidizi, Kurugenzi Mifumo ya Malipo ya Taifa, Mutashobya Mushumbusi amesema katika hatua nyingine za kuchangia matumizi ya huduma jumuishi za fedha, BoT imeanzisha mazingira ya majaribio ya ubunifu ili kuchochea wabunifu kuweza kujaribu bunifu zao.
Pia Benki Kuu kwa kutambua umuhimu wa huduma bora, imeanzisha mfumo maalumu wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi (Sema na BoT) ili kuhakikisha kero za wananchi juu ya huduma za fedha zinashughulikiwa kwa wakati.
“Mafanikio haya ni kielelezo cha uongozi thabiti katika kusimamia juhudi za kuongeza na kuchochea matumizi ya huduma za fedha kwa kutumia teknolojia. Hatua hizi zinalenga kuongeza ufanisi, kupunguza gharama, na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa na kuboresha maisha yao,” amesema.