Muheza. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema dhamira ya chama hicho katika miaka mitano ijayo ni kuibadilisha Wilaya ya Muheza, Mkoa wa Tanga iwe ya kisasa na kichocheo cha uchumi wa wananchi.
Dk Nchimbi amesema hayo leo Jumanne, Septemba 16, 2025 katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu, uliofanyika Uwanja wa Jitegemee, Muheza Mjini.
Amemwombea kura mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani.
Katika mkutano wa leo, mgombea ubunge wa Muheza, Khamis Mwijuma, maarufu Mwana FA ameeleza mafanikio, changamoto za miaka mitano iliyopita huku Dk Nchimbi akibainisha nini wanatarajia kukifanya wakishinda uchaguzi mkuu wa Jumatano Oktoba 29, 2025.

Dk Nchimbi amesema CCM haijabadili utamaduni wake wa kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi na ndiyo maana imepanga kufanya maendeleo makubwa katika miaka mitano ijayo endapo wataibuka na ushindi kwenye uchaguzi mkuu.
Amesema wanadhamiria kufanya upanuzi mkubwa wa Hospitali ya Wilaya ya Muheza, kuongeza vituo vya afya vitatu, kujenga zahanati 10 pamoja na kuongeza madaktari na wauguzi.
“Shule mpya 10 za msingi na sekondari tano tutajenga. Madarasa ya shule za msingi 215 na sekondari 115 yatajengwa. Lakini pia, maabara mpya 20 zitajengwa,” amesema Dk Nchimbi.
Aidha amesema, miradi mipya 12 ya maji vikihusisha visima virefu vitaanzishwa ili kufanya upatikanaji wa maji kufikia asilimia 90.

Kuhusu ubora wa barabara, Dk Nchimbi amesema kiwango cha lami za mjini kitaongezeka na za changarawe. Tutaboresha chanzo na tiba ya mifugo ili kuwawezesha wafugaji kufurahia ufugaji wao.
Awali, Dk Nchimbi amempa nafasi, mgombea ubunge wa Muheza, Khamis Mwijuma, kuzungumza ambapo amesema kata 13 hazikuwa na shule za sekondari lakini mpaka sasa zimesalia tatu tu.
Mwana FA ambaye pia ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema shule 15 za sekondari zinatarajiwa kujengwa miaka mitano ijayo.

“Hatukuwahi kuwa na Hospitali ya Wilaya ya Muheza, lakini Rais Samia akiwa makamu wa Rais alianzisha mchakato na huduma kwa sasa zinatolewa na amekwishaleta Sh3.3 bilioni za kuboresha ikiwamo vifaatiba na watumishi,” amesema.
Mwana FA amesema, katika kipindi cha miaka minne na nusu ya utawala
wa Rais Samia, Wilaya ya Muheza ikiwa na miaka 47, ilikuwa na kituo kimoja cha afya lakini sasa kuna vituo vinne: “Yaani miaka minne na nusu tu, vituo vitatu vimejengwa.”
Amebainisha changamoto ni soko la mazao kama pilipili, mdalasini na machungwa ambayo yamekuwa yakiharibika kabla hayajafika sokoni.
“Lengo tuwe na soko la kimataifa la machungwa na viungo ili kuwanufaisha wakulima wetu,” amesema Mwana FA.
Kwa upande wake, Katibu wa Oganaizesheni wa CCM, Issa Ussi Gavu amesema, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Samia amefanya mengi ikiwemo kwenye sekta ya elimu kwa kuongeza shule, madarasa na nidhamu.
“Rais Samia amejiandaa mtoto wa Kitanzania anapozaliwa, asikose sababu ya kusoma, kuanzia shule ya msingi hadi vyuo vikuu, elimu ndiyo msingi wa yote,” amesema Gavu.
Naye Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Wilaya ya Songea Mjini, Mkoa wa Ruvuma, Hamis Ally amesema wanawakumbusha wananchi kujua huu ni mwaka wa uchaguzi na kwa kazi kubwa iliyofanyika sekta mbalimbali, tumwongezee mitano mengine.
Ally amesema vifo vya mama na watoto vimepungua zaidi kwa sababu ya uwekezaji mkubwa wa vifaatiba hali inayosaidia kujua maendeleo ya mjamzito kuanzia anapokuwa na mimba ya miezi miwili.
“Sasa mama mjamzito anaweza kujua mtoto amekaaje, yupo nje ya mfuko au la, kukiwa na changamoto yoyote unaelezwa. Haya ni mafanikio makubwa ya Serikali ya Rais Samia,” amesema Ally.
Amesema mikopo kwa wanafunzi vyuo vikuu inaongezeka na inatoka kwa wakati: “Haya ni machache kati ya mengi, Oktoba 29 tujitokeze kwa wingi kuichagua CCM ili iendelee kutuongoza kwani miaka mitano wameonesha wanaweza.”