JKT Queens yanyakua ubingwa CECAFA

HATIMAYE JKT Queens imetawazwa kuwa bingwa wa michuano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) Wanawake baada ya kuitandika Rayon Sports ya Rwanda bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa leo Septemba 16, 2025 kwenye Uwanja wa Moi Kasarani jijini Nairobi nchini Kenya.

Bao la Winifrida Gerald dakika ya tano akifunga kwa kichwa baada ya kumalizia pasi ndefu iliyopigwa na kiungo Janeth Pangamwene, lilidumu dakika zote 90 likiipa timu hiyo ubingwa wa pili kwenye mashindano hayo.

Mara ya kwanza JKT Queens kunyakua ubingwa huo ilikuwa mwaka 2023 ikiichapa CBE ya Ethiopia kwa mikwaju ya penalti 5-4 kufuatia mchezo kumalizika bila timu hizo kufungana. Mashindano hayo yalifanyika jijini Kampala nchini Uganda.

Kwa ubingwa huo, unaifanya JKT Queens kuwa timu pekee kutoka Ukanda wa CECAFA kuwakilisha kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Wanawake itakayofanyika Oktoba 2025 nchini Algeria.

Wanajeshi hao wa kike walicheza kwa kiwango kikubwa wakiiheshimu Rayon Sports ambayo ilikuwa mara ya kwanza kucheza fainali hiyo tangu mashindano hayo yaanzishwe mwaka 2021.

Licha ya JKT Queens kucheza kwa uzoefu, lakini timu hiyo ilionekana kuwa na upungufu kwenye eneo la kiungo, mipira mingi haikufika kwa washambuliaji Stumai Abdallah na Jamila Rajabu.

Hata pasi zilizopigwa na kiungo Elizabeth Chenge na Christer Bahera, hazikufika kwa usahihi zikionekana kuishia kwa viungo wa Rayon Sports ambao walikata mawasiliano baina ya viungo wa JKT Queens na washambuliaji.

Wakati mashindano hayo yanafikia tamati, mshambuliaji wa JKT Queens, Jamila Rajabu ameibuka mfungaji bora baada ya kuweka kambani mabao matano kwenye mechi nne. 

Alianza kwa kufunga hat-trick dhidi ya JKU, kisha akafunga bao moja dhidi ya Yei Joints ya Sudan kwenye hatua ya makundi ambayo timu hiyo ilimaliza kinara Kundi C na pointi sita. Kisha bao la tano alifunga kwenye nusu fainali dhidi ya Kenya Police.