Mgombea ubunge aahidi kuondoa tatizo la maji Uyui

Tabora. Zikiwa zimepita siku chache tangu mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, kunadi sera za chama hicho mkoani Tabora, Wilaya ya Uyui nayo imezindua rasmi kampeni zake za uchaguzi.

Katika uzinduzi huo, mgombea wa ubunge wa Jimbo la Uyui kupitia CCM, Shaffin Sumar ameahidi kutekeleza ilani ya chama iwapo atapewa ridhaa ya kuongoza.

Ametaja vipaumbele vyake kuwa ni kuboresha miundombinu ya barabara, huduma za maji safi na salama, afya pamoja na elimu katika jimbo hilo.

Sumar amesema hayo leo Septemba 16,2025 wakati akinadi sera za chama chake katika uzinduzi wa kampeni kwa jimbo la Uyui uliofanyika katika kata ya Mabama wilayani Uyui mkoani Tabora.

“Mkinichagua nitahakikisha natekeleza ahadi zetu ndani ya jimbo hili najua bado maeneo mengine maji bado lakini barabara zetu sio nzuri kwa baadhi ya maeneo, kama alivyotuahidi mwenyekiti wetu wa chama Taifa, Samia Suluhu Hassan kwamba akishinda nafasi ya uraisi barabara zitaboreshwa na mengine yote yatakaa sawa,” amesema.

Wananchi wa jimbo la Uyui mkoani Tabora wakisikiliza sera za mgombea ubunge kupitia chama cha mapinduzi kwenye jimbo hilo Shaffin Sumar.Picha na Hawa Kimwaga

“Sisi Chama cha Mapinduzi tuna ushirikiano mkubwa kuhakikisha yale tunayoahidi kwa wananchi yanatekelezeka kwa vitendo na nadhani mnaona maendeleo yaliyopo kupitia ilani ya 2020-2025 CCM ilivyozingatia, hivyo hata sasa maendeleo makubwa yanakuja katika jimbo la Uyui,” ameongeza Sumar.

Kwa upande wake Katibu msaidizi wa CCM Mkoa wa Tabora, Abdallah Kazwika amewaambia wananchi wasikubali kurubuniwa kwa vitu vidogo iliĀ  kuvuruga uchaguzi, kwani kufanya hivyo ni kujinyima haki ya msingi ya kupata kiongozi bora wa kuwaletea maendeleo.

Kwa upande wake mgombea wa ubunge jimbo la Tabora Mjini, Hawa Mwaifunga amesema endapo atachaguliwa atahakikisha huduma za afya Tabora zinaboreshwa kwani ni miongoni mwa mahitaji muhimu ya wananchi.

“Ndugu zangu wana Tabora mtaji wa kwanza wa maendeleo ni afya, hivyo cha kwanza nitahakikisha afya inakua bora ili kuleta maendeleo yetu wana Tabora,” amesema.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Mkoa wa Tabora, Mwanne Nchemba, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni hizo, amesema kuwa CCM kimejikita katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na kitaendelea kusimamia maendeleo ya kweli kwa Watanzania wote.

“Twende pamoja tushirikiane, tulete maendeleo wananchi nyie mnataka maendeleo na sio maneno na kejeli zisizo na tija kwao,” amesema.