Yanga sasa wababe wa Kariakoo Dabi

Yanga imeendeleza ubabe kwa Simba baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa fainali ya Ngao ya Jamii uliochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Shujaa wa Yanga katika mchezo huo alikuwa ni Pacome Zouzoua aliyefumania nyavu katika dakika ya 54 ya mchezo.

Ushindi huo umekuwa ni wa sita mfululizo kwa Yanga katika mechi ilizocheza dhidi ya Simba.

Katika kipindi cha kwanza, timu hizo zilicheza kwa kupishana na zilishambuliana mara kwa mara jambo ambalo lilifanya kila moja ipate nafasi kadhaa ambazo kama ingezitumia vizuri ingeweza kupata bao au mabao.

Mfano wa nafasi nzuri ambayo Yanga ilipata katika kipindi hicho cha kwanza ni ile ya Dube ambaye alipigiwa krosi nzuri na Aziz Andabwile lakini mshambuliaji huyo aliunganisha mpira huo kwa bega na kumrahisishia kazi kipa Mousa Camara kuuokoa.

Simba walipata nafasi mbili nzuri ambazo kama wachezaji wake wangekuwa na utulivu zingeweza kuwa na faida kwao.

Dakika ya 25, Simba walipata pigo baada ya beki wake Abdulrazack Hamza kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Chamoue Karaboue.

Ya kwanza ilikuwa dakika ya 27 ya Kibu Denis na nyingine ya 40 ya Shomari Kapombe ambao wakiwa wanatazama na kipa Djigui Diarra walipiga mashuti ambayo kipa huyo aliokoa na kuliweka salama lango la Yanga.

Kosakosa hizo ziliendelea hadi pale Refa Ahmed Arajiga alipopuliza filimbi ya kuhitimisha kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kufanya mabadiliko ya kumtoa Mudathir Yahya na kumuingiza Mamadou Doumbia.

Yanga iliongeza kasi ya mchezo baada ya mabadiliko hayo na dakika tisa tu baada ya kipindi cha pili kuanza, Pacome Zouzoa aliifungia bao la kuongoza akimalizia pasi ya Maxi Nzengeli.

Baada ya bao hilo, Simba ilibadilika na kulishambulia mara kwa mara lango la wapinzani wao lakini safu ya ulinzi ya Yanga ilikuwa makini kuokoa hatari hizo.

Yanga katika kipindi hicho cha pili ilifanya mabadiliko mengine ya kuwatoa Chadrack Boka, Prince Dube, Duke Abuya na Maxi Nzengeli na kuwaingiza Balla Conte, Celestine Ecua, Clement Mzize na Mohamed Hussein.

Simba pia iliwatoa Elie Mpanzu, Steven Mukwala na Allasane Kante ambao nafasi zao zilichukuliwa na Neo Maema, Seleman Mwalimu na Anthony Mligo.

Yanga ilianza na kikosi kilichoundwa na Djigui Diarra, Israel Mwenda, Chadrack Boka, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Aziz Andabwile, Maxi Nzengeli, Duke Abuya, Prince Dube, Mudathir Yahya na Pacome Zouzoua.

Kikosi cha kwanza cha Simba kiliundwa na Mousa Camara, Shomari Kapombe, Naby Camara, Rushine De Reuck, Abdulrazack Hamza, Allasane Kante, Kibu Denis, Yusuph Kagoma, Steven Mukwala, Jean Ahoua na Ellie Mpanzu.