Salum Mwalimu atoa ahadi kwa wachimbaji akiomba kura

Katoro. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ameahidi mageuzi makubwa katika sekta ya madini kwa kuwalinda wachimbaji wadogo, hasa vijana, dhidi ya kile alichokiita ni unyanyasaji wa kuondolewa katika maeneo yenye rasilimali kama atachaguliwa.

Amesema wimbi la unyanyasaji kwa wachimbaji hao limezidi, wanafukuzwa kwa nguvu na kunyimwa haki baada ya wawekezaji wakubwa au watu wenye ushawishi mkubwa kuvutiwa na maeneo hayo.

Hivyo, amesema Chaumma kikipewa ridhaa ya kuongoza dola Oktoba 29 mwaka huu, ataenda kukomesha hali hiyo.

Akizungumza leo Jumanne Semptemba 16, 2025 kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika, Katoro mkoani Geita, Mwalimu amesema wachimbaji wadogo wanapitia wakati mgumu hasa wakigundua madini, wanafukuzwa na maeneo hayo kukabidhiwa kwa wawekezaji wenye mitaji mikubwa.

“Utawahamisha vijana wa Kitanzania hadi lini, wakati Mungu aliwapa dhahabu hizo ili ziwaondoe kutoka kwenye umaskini? Maeneo madogo madogo kama Nyarugusu na Nyatwiga yatalindwa. Hawataondolewa; vijana watapewa fursa ya kunufaika na rasilimali hizo Serikali ya Chaumma itasimamia.” amesema Mwalimu.

Ameahidi sera rafiki kwa wachimbaji wadogo, ikiwamo ya kurasimisha maeneo yao ya kazi ili waweze kupata dhamana ya mikopo kutoka taasisi za kifedha, jambo ambalo litawawezesha kukuza mitaji yao na kujiendeleza kiuchumi.

“Haiwezekani mtu mdogo akigundua madini leo, kesho anaondolewa eti mwekezaji anakuja na mtaji mkubwa. Serikali ya Chaumma haitakubali mtego huo. Rasilimali zikitambuliwa, mwananchi kwanza ushukuru Mungu. Mwekezaji aje, lakini tuketi mezani, tugawane hisa,” amesema Mwalimu.

Kwa mujibu wa maelezo ya Mwalimu, amesema chini ya serikali ya Chaumma, wenye ardhi na vijana watahusishwa moja kwa moja katika umiliki wa miradi ya madini, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi na kupunguza tatizo la ajira.

 “Serikali ya Chaumma itawezesha wenye ardhi kuwa sehemu ya umiliki, ili kutajirisha vijana, kuwainua kiuchumi, kuwawezesha kuwekeza, na kuunda ajira nyingi” ameongeza.

Katika kuonyesha msisitizo kwa vijana, Mwalimu amesema ajira kwa vijana haitakiwi kuwa ya dhiki wala fedheha:

“Maono ya Chaumma ni ajira zenye heshima. Kuendesha baiskeli si ajira ya kuaminika kwa vijana wa leo. Leo hii kati ya vijana 10, ni wangapi wana ajira rasmi?” amehoji

Hata hivyo, hotuba ya Mwalimu Katoro imepokelewa kwa shangwe, huku vijana na wachimbaji wakionesha matumaini makubwa kwa sera mpya alizoziahidi kama atachaguliwa kuwa Rais

Kuhusu kulinda wachimbaji wadogo, Joseph Mwisa ameunga mkono sera hiyo akisema ni muhimu kuweka utaratibu wa kuwalinda wachimbaji wadogo, hasa vijana, ili wawekezaji wanapopewa maeneo, pia pawe na mpango wa kuwaendeleza vijana waliopo badala ya kuwaondoa kabisa.

“Hatuwezi kuendeleza uwekezaji kwa kuumiza kundi muhimu kama vijana. Serikali inapaswa kuhakikisha kunakuwa na mpango wa pamoja wa kunufaisha pande zote,” amesema Mwisa.