KAMPENI za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu zinaendelea tena kwa vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi huo.
Hata Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo Luhaga Mpina naye amechukua fomu,zile changamoto zake za mambo ya kisheria yaliyokuwa mahakamani yamekwisha na Septemba 13 amerudisha fomu kugombea urais.
Hata hivyo taarifa ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC)nasikia imemuondoa tena Mpina katika orodha ya wagombea urais katika uchaguzi.Ngoja tuone labda atarejeshwa tena.Masuala ya kisheria tunawaachia Wanasheria.
Wagombea wa urais wao wanaendelea na kampeni zao za kuomba ridhaa katika uchaguzi Mkuu mwaka huu hata mgombea urais kupitia CHAUMA Salum Mwalimu naye anaendelea kuomba kura.
Unauliza CHAUMMA ndio chama gani? Ni kile ambacho Mgombea wake katika uchaguzi mkuu mwaka 2015 na uchaguzi mkuu 2020 alikuwa Hashim Rungwe aliyekuwa akitamba na sera ya Ubwabwa.
Yaani yeye alikuwa anaeleza waziwazi kabisa akipata ridhaa ya kushika dola na kuwa Rais basi wananchi tutakuwa tunakula ubwabwa kwa raha zetu. Ila ndio hivyo tena mzee Rungwe safari hii kamuachia Salumu Mwalimu kugombea nafasi hiyo.
Ni yule Salumu Mwalimu aliyekuwa CHADEMA lakini alishaachana na CHADEMA ,yupo zake CHAUMA.Kwani shida iko wapi?
Ndio hivyo kampeni zinaendelea na kama nilivyosema wagombea urais wanaendelea kuchanja mbuga wakiomba kura hata rafiki na ndugu yangu Hassan Doyo wa ADC na sera yake kubwa ndugu ni ya kubana matumizi ya Serikali.
Doyo kama unakumbuka alikuja na sera yake kwamba akiwa Rais atauza yale magari mazuri mazuri tunayaitaga kwa jina la mashangingi .Ni yale magari ya kifahari atayauza yote.Kisa yanatumia mafuta mengi hivyo kumaliza hela.
Ila bwana malipo ni hapa hapa ujue Doyo baada ya kuchukua fomu ya kugombea urais unajua nini kilifuata ?Kapewa shangingi jipya zero kilometa.
Yaani gari mpya kabisa ,ndio anayozunguka nayo akiomba kura hata ile kauli yake ya kwamba atauza mashangingi haisikiki tena.Nadhani atakuwa ameanza kunogewa.
Acha tusubiri wapiga kura wataamua.Kila la heri ndugu yangu Hassan Doyo.Gari hiyo imetolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi(INEC).Doyo mwenyewe anainjoi tu kwenye shangingi jipya.
Halafu unajua baada ya kupewa lile Shangingi hakutaka kulipanda mbele ya waandishi wa habari akaenda kupandia nje eti tusimuone.Doyo bwana ana akili kama Sungura na ile hadithi ya sizitaki mbichi hizi.
Ni kama nilivyoeleza pale juu kabisa kampeni zinaendelea halafu ni kwambie tu mtanzania mwenzangu uwe makini katika kusikiliza sera za wagombea kisha ufanye uamuzi sahihi.
Wakati naandika kuhusu wagombea kichwani amenijia mgombea urais kule Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wakulima (AAFP)Said Soud Said yeye amekuja na sera yake ya kwamba atapiga marufuku mafundi kutengeneza kitanda cha futi sita kwa sita.
Yeye anasema akiwa Rais basi vitanda anataka viwe ni futi nne kwa nne eti wanandoa wanapolala wawe karibu.Unajua kwanini?Ni kwamba anataka kuona watu wanaongezeka kwa kuzaliana kwa wingi.
Usicheke ndio sera ya mgombea urais hiyo.Ninaposema uwe makini kusikiliza sera za wagombea urais na mipango yao uwe makini.Uwe unawaelewa. Ukizubaa umeuziwa mbuzi kwenye gunia.
Hata Chama cha Wananchi (CUF) nacho hakiko nyuma wamemsimamisha Samandito Gombo kuwania urais na kwa upande wa Zanzibar ni Hamad Masoud Hamad .Mzee wangu na rafiki yangu sana Profesa Ibrahim Lipumba ameamua kupumzika.
Hakugombea ameacha na wengine .CUF sera yao kuu ni Haki Sawa kwa Wote,Ila CUF yenyewe nayo ni kama ipo haipo.Wakati ule wa Ngangari ilikuwa ngangari kweli kweli.Ila siku hizi CUF ndembendembe.Ila wamo na huwezi jua acha tuendelee kusikiliza sera zao.
Baada ya maelezo hayo kuhusu uchaguzi mkuu na kampeni zinazoendelea kwa wagombea urais sasa naomba rudisha akili yako kichwa,weka medula oblangata yako vizuri ili unielewe vizuri kipindi hiki cha kuelekea Oktoba 29,2025.
Oktoba ndiyo siku ambayo Watanzania tutajipanga katika mistari mireeeeeeefu kwa ajili ya kupiga kura kuchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Wabunge na madiwani.
Katika uchaguzi huo, Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alizindua kampeni zake katika viwanja vya Tanganyika Packers pale Kawe Dar es Salaam.
Ni pale Kawe ambako kwa sisi wengine kwetu ni eneo muhimu na maalum ambako Mtume na Nabii Boniface Mwamposa huwa anatutamka na kutuombea baraka.
Ni eneo ambalo tumekuwa tukipata baraka zenye upako ambao hakika wenye magonjwa tunapona, wenye shida nazo zinapata ufumbuzi.
Hapo ndio CCM ilikutanisha maelfu ya Watanzania kuanza safari za kampeni za kusaka dola.Ilitumia jukwaa hilo kushusha upako na utakaso wa sera na ahadi kemkemu kwa wananchi.
CCM bwana wanajua kujipanga katika mambo. Ukisikiliza mipango na mikakati ya Serikali katika miaka mitano ijayo iwapo unabaini Chama sahihi ndio hicho.Nikwambie ukweli CCM ndio chama kiongozi,chama chenye dhamira ya kweli,chama kilichobeba matarajio ya watu wake.
Katika uzinduzi ule wa kampeni za mgombea urais ,Dk.Samia Suluhu Hassan aliweka wanini ambacho Serikali itakwenda kufanya katika kipindi cha miaka mitano. Ukifuatilia hotuba yake ya ufunguzi wa kampeni zake unaiona kabisa dhamira yake njema kwa Taifa hili la Tanzania.
Ukimsikiliza Dk.Samia Suluhu Hassan na sera zake sambamba na Ilani ya Uchaguzi Mkuu 2025-2030 kuna tofauti kubwa kati yake na wale wagombea wengine nilioanza kuwaeleza.
Kuna tofauti ya mbingu na ardhi kati ya mgombea urais kwa tiketi ya CCM na wale wagombea wengine wa upinzani.Niamini mimi lakini kama hunielewi ninachokwambia sasa basi jipe muda ufuatilie ninachokwambia.
Bila kupepesa macho katika uchaguzi mkuu 2025 kura yangu ni kwa Dk.Samia ,kura za Watanzania ni kwa Dk.Samia ,huo ndio ukweli na wala hakuna sabababu ya kukuficha.
Nimefanya utafiti wangu wa kawaida kwa wagombea urais .Ni utafiti ambao sio rasmi kama ule unaofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam au REDET
Nimejiridhisha Dk.Samia ndio mgombea urais sahihi kwa sasa.Namuona kabisa Dk.Samia anavyokwenda kushinda kwa kura nyingi.Namuona akienda kushinda kwa zaidi ya asilimia 90 .
Anakwenda kuandika historia ya kuwa mgombea urais aliyeshinda kwa kura nyingi.Ndio nakwambia hivyo hata ukikunja sura haitakusaidia.
Ngoja nitoe sababu za kwanini katika uchaguzi mwaka huu atashinda kuwa nyingi? Kunywa maji kwanza au meza fundo la mate halafu endelea kusoma.Ni kama dakika tano hivi utakuwa umemaliza kunisoma.Endelea sasa.
Sababu namba moja ambayo inambeba Dk.Samia Katika uchaguzi mkuu 2025 ni ubora wa Ilani ya CCM yenye kurasa 60 lakini ni kurasa zilizobeba maisha ya Watanzania.Ilani inayotoa muelekeo kwa miaka mitano ijayo.
Ilani ya Uchaguzi Mkuu 2025 ya CCM lengo kuu lake ni kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa wananchi.Ngoja nikwambie unapoangalia lengo kuu la Ilani hiyo unaona jinsi Chama na mgombea wake wa urais wako SIRIAZI.
Ukiondoa lengo hilo, Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ina ahadi na maelekezo ya Chama hicho 2025-2030 sambamba na vipaumbele vya Ilani ambavyo vimetajwa kwa ufasaha katika ukurasa wa 28 wa Ilani hiyo.
Vipaumbele hivyo ni kuchochea mapinduzi ya uchumi wa kisasa, fungamanishi ,jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa kuongeza thamani rasilimali zinazozalishwa.
Pia kuongeza fursa za ajira kwa vijana,kuongeza kipato kwa wananchi na kupunguza umasikini.Kipaumbele kingine ni kuboresha maisha ya watu na ustawi wa jamii.
Vipaumbele vingine ni kuendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, kukuza na kuimarisha matumizi ya sayansi na teknolojia katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
Pia kudumisha demokrasia na Utawala bora, kuendelea kudumisha amani, utulivu na usalama , kududumisha utamaduni wa taifa, na kukuza sanaa na michezo wakati kipaumbele namba tisa ni kuendeleza kasi ya maaendeleo vijijini.
Hivyo unapoangalia Ilani hiyo, lengo na vipaumbele vyake unaona kabisa katika miaka mitano ijayo inakwenda kuifanya Tanzania kuwa bora zaidi.
Yaani kwa kifupi Dk.Samia anakwenda kubadilisha maisha ya Watanzania kuwa yenye ustawi wa maendeleo. Ushindi wa Dk.Samia unaanza kuona kuanzia kwenye Ilani ya Uchaguzi.
Kauli ya Kazi na Utu Tunasonga mbele nayo imekuwa sababu ya msingi ambayo imewafanya Watanzania katika mikoa ambayo tayari amepita kuilewa kauli mbiu hiyo ambayo CCM imekuja nayo katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
Mgombea Dk.Samia Suluhu Hassan amekuwa akielezea Kazi na Utu Tunasonga Mbele na moja ya ufafanuzi wake kuhusu kauli mbiu hiyo ni jinsi ambavyo CCM inaamini katika utu wa mtu,inaamini katika kutekekeleza majukumu yake ya kuwahudumia watanzania kwa kuangalia utu zaidi.
Dk.Samia hataki kabisa kuwa na Serikali ambayo ufanyaji kazi wa watumishi wake wawe watumwa,wawe wenye hofu,wawe wenye kuhangaika na maslahi yao.
Anataka kuwa na Serikali ambayo inaamini katika kazi lakini inaamini katika utu.Yale mambo ya utumishi kuiona kazi anayoifanya kama yuko jela kwa Dk.Samia hapana.
Lakini kwa Dk.Samia hii kauli mbiu ya Kazi na Utu Tunasonga Mbele unapoitazama kifalsa na kiitikadi kwa sera za CCM ni suala la usawa wa kibinadamu na usawa wa binadamu haimaanishi binadamu wote tutengeneze usawa tuwe na kimo kimoja hapana, haimaanishi kuwa na rangi moja ,jinsia moja hapana.
Haimaanishi mapato yanayofanana hapana usawa wa kibinadamu kwa mujibu wa itikadi na falsafa ya CCM ni kuheshimu utu wa kila binadamu awe mrefu au mfupi kama mbilikimo.Katika suala la heshima ya utu wake yeye ni sawa.
Hivyo unapomsikiliza Dk.Samia anapozungumzia Kazi na Utu unaona anazungumza kuhusu ujenzi wa miradi ya maendeleo kama shule,maji ,afya.
Na Dk.Samia haiwezi kufanya tofauti na hata unapoangalia Chama Cha Mapinduzi kinajenga shule, zahanati, vituo vya afya ,maji, mawasiliano na maeneo mengine hiyo yote ni kulinda heshima ya utu wa watu wote.
Sababu nyingine ya Dk.Samia kushinda kwa asilimia kubwa katika uchaguzi mkuu mwaka huu ni kwamba nimefuatilia mapokezi ya wananchi katika mikutano yake ya kampeni ya kuomba ridhaa.
Maelfu ya wananchi wamekuwa wakijitokeza kumsikiliza na wengi baada ya kueleza mipango yake wanamuelewa na kwa sehemu kubwa wako tayari KUTIKI Oktoba 29 .
Binafsi nimebahatika kuwepo katika mikutano ya kampeni ya Dk.Samia nilikuwepo pale Kawe jijini Dar es Salaam na kisha katika mikutano ya Mkoa wa Morogoro,Dodoma, Songwe,Mbeya, Njombe,Iringa, Singida,Tabora na Kigoma .Amepita mikoa 10 mpaka sasa.
Kote huko maelfu ya wananchi wamejitokeza kumsikiliza Dk.Samia,kumuona na kubwa zaidi wengi wanafurahia yaliyomo katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu .
Lakini pia wanafurahishwa na mipango ya Dk.Samia hasa yale ambayo amepanga kuyatekeleza ndani ya siku 100 za kwanza baada ya kupata ridhaaa kuongoza nchi.
Sababu nyingine ni kwa yale ambayo Dk.Samia Suluhu Hassan ameyafanya katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wake.Yanatosha kabisa kuwafanya Watanzania kumpigia kura na kumchagua.
Dk.Samia amegusa maeneo yote katika nchi hii,amegusa katika elimu,maji,kilimo,ufugaji,uvuvi, umeme,barabara, ujenzi vituo vya vituo vya afya,zahanati ,hospitali za wilaya na mkoa.Sitaki kwenda ndani zaidi maana sote ni mashahidi ukitaka kuamini waulize wakulima ambao wamepatiwa mbolea na pembejeo ya ruzuku.
Waulize akina mama ambao Dk.Samia amewatua ndoo kichwani.Waulize wafugaji jinsi ambavyo wamepunguziwa changamoto nyingi ikiwemo ya maeneo ya malisho lakini kupatiwa chanjo ya ruzuku kwa ajili ya mifugo.
Ukitaka kujua Dk.Samia amewagusa kwa kiwango gani Watanzania waulize wazazi na walezi wanaosomesha watoto.Kuanzia elimu ya awali,msingi,sekondari ni bure.
Kule kwa wanafunzi wa vyuo vikuu wanafurahia mikopo ya elimu ya juu.Ujenzi wa vyuo vya ufundi (VETA) hapo naweka kiporo. Hivyo ukisia wanasema Mitano tena kwa Dk.Samia basi wanasababu inayowafanya Oktoba 29 waseme TUNATIKI .Hata mimi nitatiki kwa Samia,kubwa tuombe uzima na uhai.
Pamoja na yote hayo lazima ukubaliane nami Dk.Samia anatoka katika Chama ambacho kimezungukwa na wazee wenye kujua historia ya nchi ya Tanzania, wazee wenye hekima,busara na maarifa.Wapo wazee ambao wamehudumu katika nafasi za juu za uongozi katika Taifa hili la Tanzania .Kwa kifupi Dk.Samia anao wazee wa kumshauri .Inatosha kwa leo.
Maisha ndio hayahaya tu.Halafu nikwambie kitu mtu wangu hapa juzi kati nimemsikia mgombea urais kupitia AAFP Kinje Ngombale Mwiru akisema akipata nafasi ya kushika dola na kuwa Rais eti atahakikishia Pikipiki a.k.a bodaboda zote nchini hazitapata pancha.Sijui anatuonaje waendesha bodaboda.
Ndio hivyo huyo naye anataka kuwa Rais na yuko kwenye kampeni. Tuache utani na Urais, sio kila mtu anaweza akawa.USISAHAU OKTOBA 29 mwaka huu TUNATIKI KWA SAMIA.
Mawasiliano yangu yaleyale tu