Mariam Ibrahim Aungana na Wanawake wa Pwani Kufagia Uwanja wa Uzinduzi wa Kampeni Bagamoyo

 

 

Mgombea Ubunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani, Mariam Ibrahim, leo Septemba 16 ameungana na Umoja wa Wanawake wa Mkoa wa Pwani kufagia viwanja vya Shule ya Msingi Majengo vilivyopo Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani.

Hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi ya mkutano mkubwa wa uzinduzi wa kampeni za Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bagamoyo, Subira Khamis Mgalu, unaotarajiwa kufanyika kesho katika viwanja hivyo.

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, Mariam alisisitiza mshikamano wa wanawake katika kuunga mkono harakati za maendeleo na kuhamasisha wananchi wa Bagamoyo kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye uzinduzi huo wa kampeni.
“Wanawake ni nguzo kubwa ya maendeleo. Leo tumeonesha mshikamano wetu kwa vitendo kwa kuandaa uwanja huu, na kesho tunaungana Mh.Subira Mgalu kwenye safari ya kuendeleza maendeleo ya Bagamoyo,” alisema Mariam.

Aidha, baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo walionesha furaha na kuahidi kujitokeza kesho kwa wingi.

“Tumehamasika sana kuona viongozi wetu wakishiriki kwa vitendo. Hii inatupa moyo wa kushiriki na kuunga mkono kampeni zinazokuja,” alisema Mwanaid Juma, mkazi wa Bagamoyo.

Wanawake waliohudhuria pia walisisitiza kuwa mshiriki na umoja ni nguvu ya pamoja katika kuleta ushindi na maendeleo ya jimbo hilo.