ZIMEPITA siku 83 tangu kumalizika kwa msimu uliopita wa Ligi Kuu na leo mzigo umerudi upya ikiwa ni saa 24 baada ya kupigwa kwa mechi ya Ngao ya Jamii iliyozikutanisha Simba na Yanga.
Msimu uliopita ligi ilifungwa na pambano la Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Juni 25 na leo inaanza kwa mechi mbili zitakazopigwa jijini Dar es Salaam na Tanga.
Ufunguzi utaanza na na mechi kati ya KMC na Dodoma Jiji itakayopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex kuanzia saa 10:00 jioni, kisha saa 1:00 usiku Coastal Union itaikaribisha Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Mechi hizi mbili zina historia yake kutokana na timu hizo, lakini mbali na hilo kuanza kwa ligi hiyo kuna mambo mengi yanakwenda kushindaniwa mbali na ubingwa unaoshikiliwa na Yanga.
Tumeshuhudia msimu uliopita kinara wa mabao alikuwa Jean Charles Ahoua wa Simba aliyefunga 16, huku Feisal Salum kutoka Azam akiwa kinara wa asisti akimiliki 13. Kipa mwenye clean sheet nyingi alikuwa Moussa Camara wa Simba aliyemaliza na 19. Safari hii itakuaje?
Ukiangalia timu zote 16 zinazoshiriki ligi hiyo zimefanya maboresho makubwa katika maeneo yote ndani ya vikosi vyao, pia zipo zilizoboresha hadi mabenchi ya ufundi.
Ni mechi inayoturudisha Aprili 18, 2025 timu hizo zilikutana kwa mara ya mwisho kwenye uwanja huo wa KMC, huku wenyeji wakishinda kwa mabao 2-1.
Katika mechi tano za mwisho timu hizo kukutana, kila moja imetamba nyumbani, hii inatoa taswira kwamba KMC ina nafasi kubwa ya kushinda leo, lakini Dodoma Jiji ina uwezo wa kupindua meza na kuweka utawala mpya.
Dodoma Jiji, iliyoshiriki Ligi kwa msimu wa sita, kucheza ugenini mechi ya kwanza itakuwa ni mara ya pili baada ya msimu uliopita ilipokutana na kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mashujaa. Timu hiyo katika misimu mitatu ya kwanza, ilianza ligi kwa kucheza nyumbani. Rekodi za mechi ya kwanza zinaonyesha Dodoma Jiji imeshinda tatu na kupoteza mbili, haina sare.
KMC yenyewe huu ni msimu wa nane inashiriki Ligi Kuu Bara, inaanzia nyumbani kwa mara ya nne, huku msimu uliopita ikianza na sare ya 1-1 dhidi ya Coastal Union. Katika misimu saba iliyopita, KMC mechi za kwanza imeshinda moja pekee msimu wa 2020-2021 ilipoichapa Mbeya City mabao 4-0. Mbali na hapo, imepoteza tatu na sare tatu.
Vikosi vyote vimefanyiwa maboresho kuanzia wachezaji hadi benchi la ufundi ambapo KMC inanolewa na Mbrazili, Marcio Maximo, wakati Dodoma Jiji ipo chini ya Kocha Vincent Mashami raia wa Rwanda.
Akizungumzia mechi dhidi ya Dodoma Jiji, Maximo alisema anakiheshimu kikosi hicho lakini anaamini timu yake ipo kwenye kiwango cha ushindani na morali iko juu.
“Dodoma Jiji ni timu nzuri, yenye wachezaji wazuri na uzoefu wa ligi hii. Lakini maandalizi yetu yametupa imani kwamba tunaweza kuanza kwa nguvu na kupata matokeo mazuri,” alisema Maximo.
Kwa upande wa Mashami, alisema: “Tumejiandaa kuanza vizuri, tunafahamu kucheza ugenini ni changamoto na rekodi zinaonyesha huwa hatuna matokeo mazuri, lakini safari hii tumejipanga kubadilisha hilo.
“Malengo ni kuona tunakusanya pointi nyingi mapema kwani ukianza vizuri inakufanya kuwa na matumaini ya kufikia malengo yako.”
KMC 2-1 Dodoma
KMC 1-2 Dodoma Dodoma 1-0 KMC
Mei 12, 2025, timu hizi zilikutana mara ya mwisho katika Ligi Kuu Bara ambapo Tanzania Prisons iliibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Coastal Union, mechi ikipigwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya. Safari hii, ngoma inapigwa Mkwakwani, Tanga nyumbani kwa Wagosi ambapo mara ya mwisho hapo timu hizo zilitoka 0-0 ikiwa ni msimu wa 2023-2024 mechi ikichezwa Mei 6, 2024. Kumbuka msimu uliopita 2024-2025, Coastal mechi za mwanzoni za nyumbani ilikuwa ikiutumia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo Arusha huku ikiichapa Tanzania Prisons 2-1, baadaye ikarejea Mkwakwani kufuatia uwanja huo kufanyiwa marekebisho.
Katika mechi tano za mwisho, Coastal Union ni mbabe wa Tanzania Prisons kwani imeshinda tatu na kupoteza moja sawa na sare. Hata hivyo, timu hizo zimekutana kipindi cha maandalizi ya msimu na kucheza mechi ambayo haikuwa na mbabe.
Utamu wa mechi hii unatokana na timu hizo kushiriki Ligi Kuu Bara kwa misimu mingi ambayo ni zaidi ya kumi, hivyo kila mmoja atataka kuonyesha ukongwe wake.
Ukiweka kando ukongwe wao, misimu mitano iliyopita, rekodi zinaonyesha Coastal Union katika mechi za kwanza za msimu, imeshinda moja pekee, huku ikipoteza mbili na sare mbili. Licha ya hivyo, lakini haijapoteza nyumbani zaidi ya kupata sare moja na kushinda moja ndani ya kipindi hicho.
Tanzania Prisons rekodi zake za kushangaza kidogo kwani tangu msimu wa 2013-2014 hadi sasa imekuwa ikianzia ugenini mechi ya kwanza ya ligi. Mara ya mwisho kuanzia nyumbani ilikuwa 2012-2012 ilipot0ka 0-0 dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Misimu mitano ya karibuni, Tanzania Prisons haijashinda mechi yoyote ya kwanza kwenye ligi, imetoka sare tatu na kupoteza mbili.