Mkutano wa Doha utawezesha kuizima Israel?

Doha. Linaweza kuwa swali la kizushi. Je, mkutano wa dharura uliokutananisha mataifa ya Kiarabu na Kiislamu Doha nchini Qatar unaweza kudhoofisha ubabe wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Ni mkutano uliokuwa chini ya uenyekiti wa Amiri wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani baada ya Israel kuishambulia Doha wiki moja iliyopita na kusababisha vifo vya watu sita na majeruhi kadhaa.

Mashambulizi ya Israel yalilenga viongozi wa Hamas wanaolezwa kuishi nchini Qatar. Si mara ya kwanza kwa Israel kuzishambulia nchi ambazo wanahisi kuna viongozi wa Hamas, nchi ambazo zimewahi kushambuliwa ni Iraq, Lebabon.

Hata hivyo, shambulio la Israel dhidi ya Qatar limeshangaza kwa sababu nchi hiyo inalindwa na majeshi ya Marekani kwa mkataba maalumu.

Lakini, pia Qatar imebeba jukumu la kuwa mpatanishi wa kumaliza vita vya Gaza na migogoro mingine ikiwamo mgogoro wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa marais Paul Kagame (Rwanda) na Felix Tshisekedi (DRC).

Siku za karibuni, Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani, alikutana binafsi na mjumbe mkuu wa mazungumzo wa Hamas, Khalil Al-Hayya, kwa lengo la kusukuma mbele mpango mpya wa kusitisha mapigano unaoongozwa na Marekani pamoja na makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka.

Majibu ya Hamas yalitarajiwa katika mkutano wa kufuatilia uliokuwa ufanyike siku moja baadaye, lakini saa chache kabla ya mkutano huo, ndege za kivita za Israel zilishambulia jengo la makazi mjini Doha, na kuua wanachama watano wa Hamas pamoja na ofisa mmoja wa usalama wa Qatar.

Shambulio hilo ndio sababu ya kutishwa mkutano wa dharura wa juzi Jumanne kwa zaidi ya 50 zikiwamo za Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (League of Arab States), inayojumisha nchi takriban 22 na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) inayojumuisha nchi 57 zilikutana Doha nchini Qatar.

Chini ya uenyekiti wa Amiri wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, pamoja na kulaani shambulio hilo, viongozi hao walitoa maazimio kadhaa ikiwamo kufanya juhudi za kidiplomasia, kisiasa, na kisheria kuhakikisha Israel inatii wajibu wake, kama nchi inayotawala, kwa wajibu wake wa kuzingatia hatua za hiari zilizotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki tarehe 26 Januari 2024 katika kesi inayohusu Matumizi ya Mkataba wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari (Genocide) katika Ukanda wa Gaza.

Pia, wametaka utekelezaji wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la “Tamko la New York” kuhusu utekelezaji wa suluhisho la nchi mbili na kuanzishwa kwa nchi huru ya Palestina.

Tamko hilo ni nia ya wazi ya jumuiya ya kimataifa inayounga mkono haki halali za watu wa Palestina, ikiwa ni pamoja na haki yao ya kuanzisha taifa lao huru.

Kwenye mkutano huo, Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani, ameitaka jumuiya ya kimataifa ikatae visingizio vya Israel vya kudai mashambulizi yake yamelenga kujilinda na ilitie hatiani taifa hilo.

“Wakati umefika kwa jumuiya ya kimataifa kuacha kutumia viwango viwili vya haki na kuiadhibu Israel kwa uhalifu wote ilioufanya,” alisema Waziri Mkuu Al Thani.

Licha ya shambulio hilo, Qatar inajivunia sifa ya kimataifa na rekodi ya mafanikio kama mpatanishi asiyeegemea upande wowote, anayeaminika na mwenye kuwajibika, ambaye hualikwa kusaidia pande husika kufikia makubaliano.

Kuitishwa kwa mkutano huo wa dharura ni ishara Qatar inayo onyesha dhamira ya kikatiba ya muda mrefu ya kutatua migogoro ya kimataifa kwa njia ya amani, kama ilivyo ndani ya katiba yake.

Ibara ya 7 ya Katiba ya Qatar inaeleza kuwa upatanishi ni kipaumbele katika sera yake ya mambo ya nje: “kulingana na kanuni ya kuhimiza utatuzi wa amani wa migogoro ya kimataifa.”

Lengo la upatanishi wa Qatar ni kukuza na kufanikisha usimamizi wa migogoro, na kutatua migogoro na mizozo kwa njia ya amani.

Upatanishi wa Qatar hufanyika kati ya mataifa, pamoja na kati ya taifa na wahusika mbalimbali wasio wa kiserikali.

Mwaka 2023, Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar ilianzisha nyadhifa mpya za mawaziri, na kutoa uzito wa kidiplomasia zaidi kwa masuala ya upatanishi, sambamba na kuimarisha timu ya Wajumbe Maalumu na Maofisa wengine wa ngazi za juu wanaohusika na upatanishi.

Qatar imefanya kazi kuimarisha ushirikiano wake na nchi muhimu katika nyanja ya upatanishi na utatuzi wa mizozo kwa kusaini makubaliano ya maelewano na Sweden, Norway na Finland. Aidha, Qatar ina mahusiano mengine ya pande mbili ya kiserikali yanayolenga kubadilishana maarifa na kushirikiana zaidi katika masuala ya upatanishi na utatuzi wa mizozo.

Licha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kutoa hati ya kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, bado ameendelea kuwa mwiba na mashambulizi dhidi ya mataifa mengine.

Novemba 21, 2024, kufuatia uchunguzi kuhusu uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, ICC ilitoa hati za kukamatwa kwa maofisa wawili waandamizi wa Israel: Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel, na Yoav Gallant, Waziri wa zamani wa Ulinzi wa Israel.

Wawili hao wanatuhumiwa kuwa na uwajibikaji kwa uhalifu wa kivita wa kutumia njaa kama mbinu ya vita, pamoja na uhalifu dhidi ya ubinadamu unaojumuisha mauaji, mateso ya kikundi, na matendo mengine ya kinyama wakati wa vita vya Gaza.

Hati hiyo ya kukamatwa dhidi ya Netanyahu ndiyo ya kwanza kutolewa dhidi ya kiongozi wa nchi ya kidemokrasia inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi kwa tuhuma za uhalifu wa kivita.

Nchi zote 125 wanachama wa ICC, zikiwamo Ufaransa na Uingereza, zinawajibika kisheria kumkamata Netanyahu na Gallant endapo wataingia katika maeneo yao ya mamlaka.

Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao