NYOTA wapya wa Simba, Neo Maema na Naby Camara wameeleza vile walivyo na shauku ya kucheza Ligi Kuu Bara mara ya kwanza huku wakiwa na malengo ya kuisaidia timu hiyo kurejesha heshima.
Kwa misimu minne mfululizo, Simba imekuwa ikishuhudia Yanga ikitwaa ubingwa wa ligi jambo ambalo wadai linawapa hamasa kupigania kurejesha makali ya Msimbazi.
Maema, kiungo mshambuliaji kutoka Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, alisema amejiunga na Simba akiwa na kiu ya mafanikio mapya na anaamini ligi ya Tanzania itampa changamoto na nafasi ya kuonyesha thamani yake.
“Nimekuja hapa kwa sababu najua Simba ni klabu kubwa, yenye historia na yenye mashabiki wanaopenda kuona timu inashinda. Nataka kuchangia katika mafanikio yao na naamini huu ni mwanzo wa safari nzuri kwangu,” alisema Maema.
Kwa upande wake, nyota wa Guinea, Naby Camara aliyejiunga akitokea AS Kaloum Star, alisema: “Kucheza Simba ni heshima kubwa. Najua matarajio ni makubwa sana, lakini nimejiandaa kupigana kwa ajili ya timu hii. Mashabiki wategemee kujitoa kwangu uwanjani na kupambana hadi dakika ya mwisho.”
Camara mwenye uwezo wa kucheza kama beki wa kati, pembeni au kiungo, ameanza kuingia kwenye mioyo ya mashabiki wa Simba kutokana na kiwango alichoonyesha kwenye tamasha la Simba Day dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.
Nyota huyo alianza kucheza kama kiungo na baadae akatumika beki ya kushoto baada ya kocha Fadlu Davids kuamua kumpumzisha, Anthony Mligo, licha ya mabadiliko hayo alionekana kufanya vizuri.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids anategemea nyota hao wapya kuongeza kitu tofauti ndani ya kikosi, Maema akiwa suluhisho la ubunifu katikati ya dimba na Camara akiongeza wigo kutumika katika nafasi tofauti.
Simba ilifanya usajili wa kimkakati kuelekea msimu huu ikilenga kurejesha makali kwenye Ligi Kuu Bara na kuendelea katika michuano ya kimataifa. Ikumbukwe msimu uliopita timu hiyo ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Maema alisema mafanikio hayaji kwa maneno bali kwa kazi na mshikamano wa wachezaji. “Tunapaswa kushirikiana kama familia moja. Ndio njia pekee ya kupata matokeo. Na mimi niko tayari kwa changamoto hii,” alisema Maema, huku Camara akiongeza:
“Hakuna kitu kizuri kama kuona mashabiki wanakushangilia baada ya ushindi. Ndio maana nimekuja Simba, nataka kushinda vikombe na kuandika historia yangu hapa.”
Mashabiki wa Simba wamekuwa na matarajio makubwa juu ya nyota hao wapya, wakiamini kuwa ujio wao unaweza kuleta upepo mpya na kuibua matumaini ya kurejesha taji la ligi lililopotea mikononi mwa Yanga kwa muda mrefu.
Mara ya mwisho kwa Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ilikuwa 2020/21 ikijikusanyia pointi 83 kwa kushinda mechi 26, sare tano na ikipoteza mechi tatu, Yanga ilimaliza ya pili na pointi 74.