KONGOLE TAKUKURU KUIKUMBUSHA JAMII KUKATAA RUSHWA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025

…………………

Na: Dkt. Reubeni Lumbagala, Tanga

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Oktoba 29, 2025 ni siku ambayo Taifa letu litafanya Uchaguzi Mkuu ili kuchagua viongozi katika nafasi za urais, ubunge na udiwani.

Agosti 28, 2025, kampeni zilizinduliwa rasmi ambapo wagombea walianza kunadi Ilani za vyama vyao na sera zao kwa ujumla katika kipindi cha miaka mitano ijayo 2025-2030 ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.

Rushwa ni moja ya tatizo kubwa hasa kipindi hiki cha uchaguzi kwani baadhi ya wagombea wasio na maadili hutoa rushwa ili kushawishi wapigakura wawapigie kura kuwachagua katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) haijalala, ipo macho kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa kutumia njia mbalimbali za utoaji elimu ili kuhakikisha nchi yetu inapata viongozi bora wasiotokana na rushwa. Sanjari na hilo, Takukuru imedhamiria kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika na kuthibitika kutoa au kupokea rushwa kwani ni kinyume na sheria za nchi yetu nzuri ya Tanzania.

Pamoja na uwepo wa njia kadhaa za utoaji elimu kwa Umma, Takukuru pia inatumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kama vile simu za mikononi ili kuwafikia wananchi wengi zaidi ikizingatiwa kuwa wananchi wengi wanatumia simu.

Sambamba na hilo, Takukuru imewaasa wananchi kutoa taarifa kuhusiana na vitendo vya rushwa kwa kupiga simu namba 113, bure bila malipo, ili kutoa taarifa za rushwa hatimaye wahusika waweze kuchukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria za nchi.

Moja ya ujumbe unaotumwa na Takukuru kwa wananchi kupitia simu za mikononi unasema “Usipokee rushwa ili kijitoa katika uchaguzi”. Huu ni ujumbe mahsusi kwa wagombea. Takukuru inawaasa wagombea kutokujitoa badala yake washiriki kikamilifu katika uchaguzi ili kuwapa fursa wananchi kuchagua viongozi bora kupitia mchuano wa wagombea.

Ujumbe mwingine wa Takukuru unasema “Ewe mwananchi, epuka vitendo vya rushwa katika uchaguzi, usitoe wala kupokea rushwa”.  Huu ni mwendelezo wa elimu kwa Umma juu ya umuhimu wa kujiepusha na vitendo vya utoaji na upokeaji wa rushwa. Wagombea, wapambe wao na wananchi kwa ujumla wanaaswa kujiepusha kabisa na vitendo vya rushwa, badala yake wajenge hoja zitakazowashawishi wananchi kuwachagua.

Vilevile, Takukuru imeendelea kuwaasa wananchi ambao ni wapigakura kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa kutuma ujumbe usemao “Kura si bidhaa, usikubali inunuliwe”. Kura moja ya mwananchi imebeba hatma kubwa ya maendeleo katika Kata, Jimbo na Taifa pia, hivyo  ni vyema wananchi wakazingatia kuwa kura zao zina thamani kubwa katika kupata viongozi bora ambao ni chachu ya maendeleo.

Takukuru inatoa rai kwa wananchi kuthamini kura na kamwe wasiithaminishe kura yao na thamani ya fedha kwa kuzingatia kuwa kura si bidhaa ya kununuliwa bali kura ni nyenzo ya kupata viongozi bora na kwa maendeleo na ustawi wao.

Ujumbe mwingine wa Takukuru unasema “Rushwa ni adui wa maendeleo; Chagua mgombea asiyetoa rushwa”. Mgombea anayetoa rushwa hatakuwa na deni la kuwatumikia wananchi wake badala yake ataweka mazingira ya kurejesha mali zake alizozitumia kupata uongozi. Ni vyema wananchi wakaelewa kuwa kwa kukubali kwao kupokea rushwa wanajicheleweshea maendeleo wao wenyewe kwani watashindwa kumuwajibisha kiongozi wao kwani wao watakuwa sehemu ya mkwamo wa maendeleo kwa kukubali kununulika pale walipochagua kupokea rushwa badala ya kuzingatia sera zenye mashiko.

Ninapohitimisha makala hii, niendelee kuwashauri wananchi wenzangu kuchagua wagombea wasiotoa rushwa ili wawe na deni la kututumikia na kutatua kero zetu. Takukuru imetimiza wajibu wake wa msingi kwa kutuelimisha kupitia jumbe mbalimbali katika simu zetu za mikononi. Tusipuuze jumbe hizo, kwani zimebeba hatma kubwa ya maendeleo ya nchi yetu. Tafakari, chukua hatua stahiki.

Dkt. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga.

Maoni: 0620 800462.