Ligi Kuu Bara: Hawa mbona kazi wanayo!

MSIMU mpya wa Ligi Kuu Bara wa 2025-2026 unaanza leo ukiwa ni wa 62 tangu ilipoanza 1965.

Kila timu kati ya 16 zinazoshiriki zinaanza hesabu mpya kuwania pointi 90 kupitia mechi 30 kila moja, kukiunda na jumla ya mechi 240 kwa msimu mzima.

Klabu zinazoshiriki ni watetezi Yanga, Simba, Azam, Singida Black Stars, Tabora United, JKT Tanzania, Mashujaa, Tanzania Prisons, Namungo, Pamba Jiji, KMC, Dodoma Jiji, Coastal Union, Fountain Gate na zilizorejea ni Mtibwa Sugar na Mbeya City.

Kitu usichojua ni kwamba ni timu tano pekee ambazo zitakuwa na makocha walewale ziliokuwa nao msimu uliopita akiwamo Fadlu Davids wa Simba, Ahmad Ally (JKT Tanzania), Juma Mgunda (Namungo), Salum Manyanga (Mashujaa) na Simonda Kaunda (Tabora United).

Lakini, kuna timu 11 zinaanza vita ya Ligi Kuu na makocha wapya ambao watakuwa na kazi ya kufanya mbele ya wenzao waliopata uzoefu msimu uliopita, japo baadhi ya makocha wapya wamewahi kufundisha timu tofauti misimu ya nyuma.

WANAY 05
WANAY 05

Ni kocha mpya na kabla katika Ligi Kuu Bara akiinoa Yanga aliwahi kufanya kazi Mamelodi Sundowns, Amazulu FC, Ashant Gold, Bwechem United na Pyramids akiwa sasa na kibarua cha kuendelea kuwapa burudani mashabiki wa Jangwani ambao kwa misimu minne wamekuwa ‘wakinenepa’ kwa furaha.

Akiwa ameanza na kikosi tangu maandalizi ya msimu baada ya kumpokea Miloud Hamdi, Folz atakuwa na kazi ya kuingoza Yanga kutetea taji na kuendeleza ubabe uliofanywa na makocha waliomtangulia Yanga katika mechi kubwa.

Vincent Mashami  (Dodoma Jiji)

Ni mpya kabisa akitokea Rwanda ambapo ametua Dodoma Jiji kuchukua mikoba ya Mecky Maxime aliyeiongoza kwa misimu miwili ikimaliza uliopita ikiwa nafasi ya 12.

Dodoma Jiji ni moja ya timu zilizofanya usajili mzuri msimu huu, hivyo kumrahisishia kazi kocha huyo aliyewahi kuinoa timu ya taifa ya Rwanda na Polisi ya huko. Kwa namna yoyote akishindwa kuifikisha Dodoma Jiji katika nchi ya ahadi, huenda akawa na wakati mgumu kutokana na rekodi zilizopo timu hiyo kubadilisha makocha kila inapoyumba.

WANAY 06
WANAY 06

Marcio Maximo amerejea nchini kwa mara ya tatu kwani awali alikuja kama kocha mkuu wa Taifa Stars 2006-2010 kisha akaondoka kabla ya kurejea 2025 kuinoa Yanga, lakini aliondoshwa kipindi kifupi na sasa ametua KMC.

Hakuna asiyejua wasifu wa Maximo katika ufundishaji soka na hasa kutumia zaidi vijana, ambao wapo KMC iliyofika nusu fainali ya Kombe la Kagame na kumaliza ya nne.

Maximo ana kazi ya kuirejeshea makali KMC iliyowahi kumaliza ya nne na kukata tiketi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, vinginevyo anaweza kuwa na kipindi kifupi kama ilivyokuwa alipokuwa Yanga.

Ali Mohammed Ameir (Coastal Union)

Ni kocha kutoka Zanzibar, lakini anafundisha timu ya Ligi Kuu kwa mara ya kwanza akiwa na Coastal Union ambayo msimu uliopita ilifundishwa na makocha zaidi ya wawili akiwamo David Ouma, Juma Mwambusi na kumaliza na Joseph Lazaro.

Kocha huyo mzoefu wa kufundisha timu mbalimbali Zanzibar ikiwa ni pamoja na KVZ, timu ya taifa ya Zanzibar Heroes na ile ya vijana ya visiwani humo, hivi sasa ana kazi ya kurejesha makali ya Wagosi wanaousaka ubingwa kwa mara nyingine baada ya kutwaa 1988. Msimu uliopita Coastal ilimaliza nafasi ya nane ikiwa ni nafasi nne nyuma na ule wa 2023-2024 ilipokuwa ya nne na kukata tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika chini ya Ouma aliyefurushwa mwanzo wa msimu uliopita.

WANAY 02

Miguel Gamondi (Singida BS)

Mabingwa wa Kombe la Kagame 2025 wamemrejesha nchini kocha huyo wa zamani wa Yanga na kabeba taji la Kagame akiifunga Al Hilal ya Sudan kwa mabao 2-1.

Gamondi aliyeiongoza Yanga misimu miwili iliyopita na kuweka rekodi mbalimbali katika Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwamo kucheza makundi misimu miwili mfululizo baada ya miaka 25 tangu ilipocheza 1998, ana kazi ya kuibeba Singida msimu huu.

Kwa aina ya wachezaji na uwezo wa kiuchumi ni wazi Gamondi ana kibarua cha kuhakikisha kuwa Singida iliyomaliza nafasi ya nne msimu uliopita na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) ikipoteza kwa mabao 2-0 mbele ya watetezi Yanga, inafanya vizuri. Huyu ni kocha mzoefu wa Ligi Kuu kwani hadi alipotimuliwa na Yanga msimu uliopita aliiongoza katika mechi 10, akishinda nane mfululizo bila kuruhusu bao kabla ya kutibuliwa na Azam iliyowafunga 1-0 kisha Tabora United iliyomfumua 3-1 na kuwa sababu ya kupewa tiketi ya kuondoka Jangwani.

Florent Ibenge  (Azam FC)

Bonge la kocha mwenye wasifu mkubwa kwa soka la Afrika hususani anga za kimataifa akitokea Al Hilal ya Sudan na anafundisha kwa mara ya kwanza timu ya Ligi Kuu Bara, akiwa na Azam FC.

Ibenge aliyewahi kutwaa ubingwa wa CHAN 2016 akiwa DR Congo ana rekodi ya kuzinoa timu kubwa akizipa ubingwa ikiwamo AS Vita ya kwao DR Congo, RS Berkane ya Morocco na Al Hilal ya Sudan na sasa ana kibarua cha kuiwezesha Azam kutwaa tena ubingwa wa Ligi baada ya kuopita miaka karibu 15 tangu ilipotwaa 2013-2014, mbali na kuipaisha katika michuano ya CAF.

Kwa aina ya kikosi alichosajili mwenyewe na kuanza maandalizi ya msimu ni wazi Ibenge hatakuwa na kisingizio kama atachemsha na akae akijua akizingua anaweza kuonyeshwa mlango wa kutokea kama ilivyowahi kutokea kwa makocha wa awali wa timu hiyo.

WANAY 03

Dennis Kitambi (Fountain Gate)

Siyo kocha mgeni wa Ligi Kuu kwani ameshazinoa Simba, Namungo na nyingine misimu kadhaa ya nyuma na sasa ana kibarua cha kuipaisha Fountain Gate iliyonusurika kushuka daraja msimu uliopita kwa kujiokoa kupitia mechi za mchujo mbele ya Mbeya City. Kitambi ni mmoja wa makocha wazawa wenye uwezo mkubwa akiwahi kufundisha soka Kenya, hivi sasa ana kibarua cha kuipaisha Fountain Gate ambayo msimu uliopita ilimaliza ya 14 na kuingia katika mchujo sambamba na Tanzania Prisons.

Yusuf Chipo (Mtibwa Sugar)

Ni kocha Mkenya na si mgeni Tanzania kwani mara kadhaa amefundisha timu za Ligi Kuu ikiwamo Coastal Union na safari hii anatajwa kuwa na kibarua cha kuirejeshea makali Mtibwa Sugar iliyorejea katika ligi hiyo ikitokea Championship.

Chipo aliyekuwa akiinoa Murang’a Seal ana kazi ya kuibeba Mtibwa ili kurejea mafanikio ya kubeba ubingwa wa ligi baada ya kufanya hivyo 1999 na 2000.

Kocha huyo atasaidiana na Awadh Salum ‘Maniche’ aliyeshuka na timu hiyo na kuipandisha daraja kwa kubeba ubingwa wa Ligi y Championship msimu uliopita.

WANAY 01

Francis Baraza  (Pamba Jiji)

Kocha huyo Mkenya amerejea nchini baada ya awali kupita timu kadhaa ikiwamo Dodoma Jiji, Biashara United na Kagera Sugar, lakini safari hii ameachiwa msala na Pamba Jiji ambayo inacheza Ligi Kuu kwa msimu wa pili baada ya kupanda uliopita ikiwa na KenGold.

Huyu ni kocha mzoefu aliyeanza na mguu mzuri kwa kuiwezesha timu hiyo kutwaa taji la kwanza ikiwa Kenya chini ya uenyeji wa Shabana FC na sasa atakuwa na kazi ya kuwapaisha wababe hao wa Mwanza ambao msimu uliopita Pamba walipita mikononi mwa Goran Kopunovic na kumalizia na Fred Felix ‘Minziro’ aliyewaokoa wasishuke daraja kama KenGold na Kagera Sugar.

WANAY 04

Malale Hamsini (Mbeya City)

Ndiye kocha aliyeipandisha daraja Mbeya City iliyoshuka misimu mitatu iliyopita na kila shabiki wa timu hiyo anataka kuona inatoboaje msimu huu kwa kurejea ilichofanya ilipopanda daraja mara ya kwanza msimu wa 2013-2014 na kushuka 2022-2023.

Katika msimu wa kwanza Mbeya City chini ya Kocha Juma Mwambusi ilizitetemesha Simba na Yanga na kumaliza nafasi ya tatu, huku mabingwa wakiwa ni Azam. Hivyo Malale atakuwa na kazi kubwa akiwa na kikosi hicho maarufu kama Wanakomakumwanya.

Zedekiah Otieno  (Tanzania Prisons)

Zedekiah Otieno ni kocha mwingine mpya kabisa katika Ligi Kuu Bara msimu huu akiwa na Tanzania Prisons iliyokuwa na msimu mbaya katika michuano hiyo msomi uliopita kabla ya kuchomoka kupitia mechi za mchujo (play-off) ili kuepuka kushuka daraja.

Otieno maarufu kama Zico enzi akiupiga kama mchezaji kabla ya kugeukia ukocha akizinoa KCB, Gor Mahia na Harambee Stars kwa sasa ana kazi kubwa ya kurejesha makali ya wababe hao wa zamani wa Ligi Kuu ya Muungano. Yote katika yote mashabiki watarajie utamu katika ligi.