NITAWATUMIKIA WANA SIMANJIRO BILA UBAGUZI – OLE MILLYA

Na Mwandishi wetu, Simanjiro

MGOMBEA ubunge wa Simanjiro mkoani Manyara, kupitia CCM wakili msomi, James Ole Millya amesema endapo atapewa nafasi hiyo atawatumikia wakazi wa eneo hilo bila ubaguzi wowote.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya CCM uliofanyika mji mdogo wa Orkesumet, Ole Millya ameomba achaguliwe kwani yeye ni mtumishi wao.

Amesema hivi sasa yeye ni mbunge wa jumuiya ya Afrika mashariki inayowakilisha nchi nane, amepewa dhamana hiyo hivyo hana wasiwasi wakuitumikia Simanjiro katika nafasi ya ubunge.

“Nitaitumikia Simanjiro kwa umoja na amani na mtu anayetaka kutuvuruga sitakuwa nyuma yake kwani wote nitawatumikia bila ubaguzi wowote bila kujali mfugaji, mkulima, mvuvi wala mchimbaji,” amesema Ole Millya.

Amesema mwaka 2015 alichaguliwa kuwa mbunge wa Simanjiro na alijitoa kwa niaba ya watu wa eneo hilo bila kuwabagua na kuwaleta pamoja na ataendelea na moyo huo huo.

“Kura ni imani kama mnataka tuwatumikie kwa moyo mmoja kura za urais, ubunge na madiwani wa kata zote 18 tutiki kwa wingi kwenye CCM,” amesema Ole Millya.

Amesema ilani ya uchaguzi wa CCM imeahidi kila kitongoji kupata umeme hivyo atasimamia hilo na ataendeleza miradi ya maendeleo iliyoanzishwa Simanjiro.

Amesema atasimamia na kukomesha uuzaji ardhi holela kwenye vijiji na atasimamia hilo kwa maslahi mapana ya wana Simanjiro.

Mgeni rasmi wa uzinduzi huo, Janes Darabe ambaye ni mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi mkoa wa Manyara, amewaomba wakazi wa eneo hilo kutoa kura kwa CCM Octoba 29 mwaka 2025.

Darabe amewaomba wana Simanjiro kutoa kura kwa mgombea urais wa CCM Samia Suluhu Hassan, mgombea ubunge James Ole Millya na madiwani wa CCM.

Aliyekuwa mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema anaunga mkono maamuzi ya kamati kuu ya CCM kuondoa jina lake kugombea ubunge.

Ole Sendeka amesema hajanuna hata jina lake lake lilipoachwa na kutoletwa kwa wajumbe ili agombee nafasi ya ubunge Simanjiro.

“Chama changu kina katiba, kanuni na taratibu hivyo kocha aliyekuwa anapanga timu akaniambia wee baba kaa pembeni waachie nafasi vijana nikatii,” amesema Ole Sendeka.

Amesema yeye atakuwa meneja kampeni wa Ole Millya katika uchaguzi huo kwani hana mashaka kwa mgombea huyo katika kuitumikia nafasi hiyo.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Simanjiro, Kiria Ormemei Laizer amesema mgombea ubunge wa Simanjiro Ole Millya ni kiongozi mzoefu wa nafasi hiyo.

“Kura zote za urais, ubunge na madiwani 18 wa kata zote tunauhakika zitakwenda CCM bila wasiwasi wowote,” amesema Laizer.

Kwenye jimbo la Simanjiro kuna wagombea wanne wa ubunge wa vyama vya CCM, ACT Wazalendo, NRA na Chama Makini.