Askofu Novatus Rugambwa afariki dunia Roma

Askofu Mkuu, Novatus Rugambwa, Mtanzania aliyewahi kuhudumu kama Balozi wa Baba Mtakatifu katika nchi mbalimbali duniani amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu huko Roma, Italia.

Askofu Mkuu Rugambwa amefariki dunia usiku wa Septemba 16, 2025 akiwa Roma,  alikokuwa akiishi baada ya kustaafu utumishi wake wa kidiplomasia.

Askofu huyo alizaliwa Oktoba 8, 1957 mkoani Kagera na kuwekwa wakfu katika daraja takatifu ya upadre Julai 6, 1986 na Askofu Nestorius Timanywa wa Jimbo Katoliki Bukoba (wakati huo).

Baada ya miaka kadhaa ya huduma, Machi 18, 2010 aliwekwa wakfu katika daraja takatifu ya Uaskofu na Kardinali Tarcisio Pietro Evasio Bertone, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Vatican.

Katika safari yake ya utumishi, Askofu Rugambwa aliwahi kuteuliwa Balozi wa Baba Mtakatifu katika nchi mbalimbali ikiwamo Angola, Honduras na visiwa vya Fiji, ambapo alitambulika kwa mchango wake katika kuimarisha uhusiano wa Vatican na mataifa hayo.

Endelea kufuatilia Mwananchi