Mwabukusi analipia gharama ya mguu alioingilia TLS

Stadi ya sayansi ya siasa, inathibitisha kuwa vyama vya upinzani hunufaika kupitia migogoro na serikali, kuliko maelewano. Tutapitia kazi ya mwanazuoni Elias Koch, kutoka Shule ya Hertie, iliyopo Berlin, Ujerumani.

Shule ya Hertie ni taasisi inayoshughulika na utafiti, midahalo ya utawala bora na masuala ya umma, Ujerumani na Ulaya. Kazi ya Koch ilichapwa Agosti Mosi, 2025, ikiwa na jina: “Opposition parties seek more conflict with the government when losing electoral support.”

Tafsiri, “Vyama vya upinzani hutafuta migogoro na serikali vinapokosa uungwaji mkono kwenye uchaguzi.”

Hii ni stadi ya Ujerumani na Ulaya Magharibi. Ipo stadi nyingine iliyofanywa na Profesa Rudy Andeweg, ambaye ni mbobevu wa saikolojia ya siasa.

Kitabu cha ‘Party Governance and Party Democracy’ (Uongozi wa Chama na Demokrasia ya Chama) kilichotoka mwaka 2013, kimeandikwa na waandishi 14. Hapa nitajielekeza kwenye kurasa 16 (99 – 114), zilizoandikwa na Profesa Andeweg.

Kurasa hizo zinaunda sura yenye kichwa kisemacho, “Parties in Parliament: The Blurring Opposition.” Ikimaanisha Vyama Bungeni: Kufifisha Upinzani.

Katika sura hiyo, Profesa Andeweg anaeleza kuwa wapinzani wanapokuwa na ushirikiano au wanapotoa sauti inayofanana na Serikali, upinzani huota ukungu na kufifia.

Zipo stadi nyingi. Profesa Andeweg anayo nyingine isemayo, “Parliamentary Opposition in Post-Consociational Democracy.” Ninachotaka ni kufikisha ujumbe kutoka kwa Koch hadi Profesa Andeweg kuwa upinzani hubeba matokeo kwa umma kupitia misuguano na Serikali.

Chukua mifano ya karibu, jinsi marehemu Morgan Tsvangirai wa Zimbabwe alipoingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa na aliyekuwa Rais, Robert Mugabe mwaka 2008. Ilikuwa mwanzo wa kufifia kwake kisiasa.

Sasa hivi huko Kenya, kiongozi wa upinzani, Raila Odinga na jinsi ambavyo amekuwa akiambatana na Rais wa nchi hiyo, William Ruto, vilevile kuruhusu wasaidizi wake kuteuliwa kwenye Baraza la Mawaziri, ndivyo na nguvu yake ya ushawishi inavyofifia.

Inawezekana nimeanzia mbali kidogo, lakini lengo ni kujenga hoja yenye kueleweka sawia, kumzunguka Rais wa Jumuiya ya Sheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi. Nimeona sehemu ya mahojiano yake kipindi cha 360, cha Clouds TV, Jumatatu (Septemba 15), bila shaka, yapo mambo yanamkwaza.

Katika mahojiano hayo, Mwabukusi anaonekana kuchukizwa na mashambulizi dhidi yake. Hivi karibuni, Mwabukusi alikutana na Rais Samia Suluhu Hassan. Mkutano huo umekuwa ukikosolewa na watu wengi ambao kwa muda mrefu wamekuwa na mtazamo unaofanana na Mwabukusi.

Kwa kukutana na Rais Samia, Mwabukusi anashambuliwa kuwa tayari amesaliti mapambano.

Wengine wanasema kafika bei.

Kupitia mahojiano yake Clouds TV, Mwabukusi amejibu kwa hisia hadi kufoka. Hakuna anayependa kuonekana amenunuliwa.

Binafsi namwelewa Mwabukusi. Hata hivyo, yanayomfika ni matunda ya aina ya demokrasia ambayo Watanzania wameichagua.

Jumlisha asili ya demokrasia duniani kote. Rejea maandiko ya Profesa Andeweg na Koch, halafu mifano ya Tsvangirai na Raila.

Tuanze kwa kuiweka hivi; kwanza Mwabukusi anabeba gharama ya namna alivyoingia TLS. Ni chama cha kitaaluma. Hata hivyo, uingiaji wake ofisini ulibeba sura ya kisiasa kwa asilimia 100. Uchaguzi wa TLS ulikuwa sawa na uchaguzi wa jimbo la uchaguzi. CCM dhidi ya Chadema. Au, CCM vs upinzani.

Uchaguzi wa TLS ulifanyika Agosti 2, 2024, kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC).

Mwabukusi akibeba sauti inayomuunga mkono Chadema, alimshinda Sweetbert Nkuba, ambaye ni kada wa CCM na ilionekana chama chake kilimpigania ashinde.

Wagombea wengine katika uchaguzi huo, Ibrahim Bendera, Paul Kaunda, Emmanuel Muga na Revocatus Kuuli, hawakuwa wakitajwa sana, ni kwa sababu siasa ziligawa mchuano kuwa pande mbili, CCM vs Chadema.

JKCC ni ukumbi wa CCM. Naikumbuka kauli ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, wakati huo akiwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tanzania Bara. Lissu alisema: “Tumewashinda kwenye ukumbi wao.”

Kwamba, Chadema kupitia kete ya Mwabukusi, waliishinda CCM, waliosimama na Nkuba. Je, ni yapi ya kufafanua zaidi kuthibitisha kwamba uchaguzi TLS uliomwingiza madarakani Mwabukusi uligubikwa na siasa?

Sasa, kanuni ya uchaguzi, wanaokuunga mkono, wanaokupigania ushinde na wanaofadhili ugombea wako, wanakuwa na masilahi juu yako. Tujiulize sasa, Chadema wakimuunga mkono na kumpigania mwanasheria awe Rais wa TLS, wanachohitaji ni nini?

Bila kuzunguka mbuyu, Chadema masilahi yao kwenye kiti cha Rais wa TLS, ni kuona taasisi hiyo inakwenda mkabala na Serikali. Tena, Chadema wangetamani kuona TLS inabeba agenda zao na kuzisimamia kwa uaminifu mkubwa dhidi ya Serikali.

Kitendo cha Mwabukusi kukutana na Rais Samia, Ikulu, Chamwino, Dodoma na kuonekana wanazungumza kwa maelewano, tena Rais huyo wa TLS, akiwa mwenye tabasamu, ilikuwa kero kwa waliompigania ashinde urais TLS.

Kipindi ambacho Chadema wanapambana kuhakikisha wanafanikisha agenda yao ya “No Reforms, No Election” halafu Mwenyekiti wao, Lissu, akiwa mahabusu akikabiliwa na kesi ya uhaini, wanamwona Mwabukusi akitabasamu na Rais Samia. Hapo ni lazima waone wamesalitiwa.

“Huwezi kumfokea Rais,” Mwabukusi anasema. Ni sahihi kabisa. Na utetezi wake kwamba anapaswa kuwasilisha hoja badala ya kukinukisha, huo ndiyo ukweli, na ndivyo Rais wa TLS anavyopaswa. Shida ni kuwa mtazamo wake unakinzana na waliomuunga mkono.

Mwabukusi anapaswa kutambua kuwa mguu uliompeleka TLS ni wa kisiasa, tena siasa za upinzani, ambazo mng’aro wake hutegemea misuguano na Serikali. Wapinzani wahafidhina huwa hawataki mazungumzo na Serikali. Chadema chini ya Lissu, ni wapinzani wa msimamo mkali.

Mwabukusi atambue kwamba hawezi kutaka majadiliano na dola, halafu akakubalika Chadema na wanaharakati wa msimamo mkali. Mwenyekiti mstaafu Chadema, Freeman Mbowe, alilipa gharama ya kupenda maridhiano, akaondolewa, itakuwa Mwabukusi aliyeungwa mkono kwa upepo tu?

Mwisho kabisa, aina ya demokrasia na mtazamo wa kundi linalobeba sauti ya upinzani Tanzania ni hatari. Ukiwa mwenye kuendeshwa na mantiki, halafu ukakubaliana na Serikali, pale unapoona ipo sahihi, hutahukumiwa kwa uhuru wako wa kufikiri, utaambiwa umehongwa. Umelamba asali.