Unguja. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan kesho atafanya mkutano wa kwanza wa kampeni kisiwani Unguja, Zanzibar.
Samia ambaye ameteuliwa kupeperusha bendera ya CCM kwenye nafasi hiyo akiwa mwanamke wa kwanza, ataomba kura kwenye ardhi ya Zanzibar ambako ndipo lilipo chimbuko lake.
Taarifa ya Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM (Itikadi na Uenezi) Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis aliyoitoa leo Jumanne Septemba 16, 2025 inaeleza kuwa, Samia atahutubia mkutano huo kwenye Uwanja wa Mwehe, Makunduchi, Unguja.
Mbeto amesema maandalizi kwa ajili ya tukio hilo yamekamilika na wananchi wakiwamo wanachama na wafuasi wa CCM wanasubiri. “Hamasa zaidi inachagizwa na kuwa mkutano huo utafanyika Makunduchi ambako ndio Samia amezaliwa.
“Hili ni tukio kubwa na kihistoria kwa Watanzania wote wa bara na visiwani, mgombea wetu anarudi nyumbani kuzungumza na wapigakura wetu. Heshima ya CCM na Samia inakwenda kuufanya mkutano huu kuwa wa aina yake. Makunduchi inamsubiri Samia kwa hamu kubwa,” amesema Mbeto.
Kwa nyakati tofauti, wananchi wameelezea kuhusu ujio wa Samia kwenye mkutano huo, wamesema tukio linalokwenda kufanyika ni la kihistoria na kila Mtanzania anasubiri kushuhudia.
“Hili ni tukio kubwa kwangu, nasubiri kumuona Samia akisimama kwenye ardhi ya Makunduchi sio kuja nyumbani kupumzika, bali kuwaomba wananchi ridhaa ya kuitumikia Tanzania.
“Ni tukio ambalo halikutarajiwa kama linaweza kutokea miaka kadhaa iliyopita, ila Samia anakwenda kuandika historia kwa Tanzania kuwa na Rais anayetokea hapa nyumbani,” amesema Mustafa Ame.
Samia anakwenda kuomba kura Makunduchi, Zanzibar baada ya kuzunguka mikoa takribani 10 ya Tanzania Bara kunadi sera za CCM na kuomba kura kwa wananchi.
Tayari amefanya mikutano mbalimbali kwenye mikoa ya Dar es Salaam ambako kampeni rasmi za CCM zilizinduliwa, Morogoro, Dodoma, Singida, Katavi, Mbeya, Rukwa, Kigoma, Iringa na Njombe.
Samia atamaliza mikutano yake ya kusaka kura visiwani Zanzibar kwa kufanya mkutano mkubwa Pemba kisha atakwenda mkoani Ruvuma kuendelea na mikutano ya kunadi sera zake.