NIKAUFUNGA ule mlango wa stoo. Tukaenda kukaa sebuleni.
“Sasa nataka nikwambie kitu cha mwisho,” baba akaniambia, na kuongeza: “Hatujui nini kitatokea, lakini endapo utakamatwa, usikubali kuwa marehemu alikuja kwako kabla ya kuuawa. Hilo jambo likatae kabisa. Na hata kama namba za gari lako zitatajwa, pia usikubali wewe ndiye uliyekwenda kuitupa maiti yake. Sema namba za gari lako zimehusishwa kwa makosa. Umenielewa?”
“Nimekuelewa, baba.”
“Kwa vile hakutakuwa na ushahidi mwingine, polisi wanaweza kukuachia.”
“Sawa.”
“Hii habari iwe siri yako; usimueleze mtu yeyote. Sasa kama ni mumeo aliyehusika au mke wa marehemu au mtu mwingine yeyote, shauri yake!”
Maelezo ya baba kidogo yalinipa matumaini. Uso wangu ukawa na tabasamu.
Baada ya hapo wazazi wangu wakaniaga na kwenda zao.
Ilipofika saa nane Raisa akaja nyumbani. Nikamkaribisha sebuleni.
“Ndiyo unatoka huko msibani?” nikamuuliza.
“Ndiyo narudi hivi. Wamepanga maziko yatafanyika kesho. Si tutakwenda kuzika?”
“Kama nitajisikia vizuri tutakwenda sote.”
“Kwani umeanza lini kuumwa? Naona umekonda sana, shoga yangu!”
“Karibu wiki sasa sijisikii vizuri, nilikuwa natembea tu. Sasa hivi ndiyo vimezidi.”
“Sasa umekwenda hospitali?”
“Nimekwenda. Wameniambia nina malaria.”
“Umepata matibabu?”
“Nimepata. Najisikia vizuri kidogo.”
“Basi mimi nakuacha, narudi nyumbani.”
“Wanasemaje huko msibani?”
“Huko kuna mengi yanayozungumzwa. Inasemekana polisi wamelipata gari la Shefa. Lilikuwa limeegeshwa katika nyumba moja sijui wapi. Sasa polisi wanashuku Shefa aliuawa katika mtaa huo, kwani alipoliacha gari hilo hakurudi tena kulichukua.”
Moyo ukanipasuka — paah!
“Lakini bado si rahisi kwa polisi kugundua marehemu aliingia nyumba gani,” nikamwambia Raisa.
“Wanaweza kugundua. Wanachofanya ni kutafuta iwapo Shefa alikuwa anakwenda katika mtaa huo mara kwa mara au ilikuwa ni mara ile aliyouawa. Kama watagundua alikuwa anakwenda mara kwa mara, watatafuta kama katika mtaa huo kuna rafiki yake, ndugu yake au jamaa yake yoyote. Wakimgundua, watajua kuwa Shefa aliuawa nyumbani kwa mtu huyo kisha mwili wake ukaenda kutupwa makaburini.”
Nikashusha pumzi ndefu za kukata tamaa.
Kumbe polisi hawatapata shida kwani kila mtu katika mtaa huo alikuwa anajua kuwa Shefa alikuwa akija nyumbani kwetu. Hata mlinzi wa ile nyumba lilipokutwa gari lake alimuona akiingia humu ndani.
Na hata kama Raisa atagundua kuwa gari lilionekana mtaa ule tunaoishi, atajua tu kuwa Shefa alikuja kwangu, kwa vile siku ile tulikuwa na ahadi. Na yeye Raisa ndiye aliyekuwa kuwadi!
Raisa atajua ni mimi niliyemuua Shefa, hasa akizingatia alivyoliona gari langu kule makaburini.
Kama polisi watampata mlinzi huyo na kumhoji, atawaeleza kila kitu. Siku hiyo mume wangu alikuwa hayupo, na niliyekuwepo nilikuwa mimi. Hivyo itafahamika mimi ndiye niliyemuua Shefa.
Nguvu ziliniishia mwilini mwangu. Nikajiambia kimoyomoyo:
“Sasa nimekwisha!”
Niliona sikuwa na ujanja tena, si wa kuepuka kukamatwa tu, bali wa kuepuka hatia ya kumuua Shefa. Mazingira yalionyesha kuwa ni lazima nitakamatwa, na ushahidi ulionyesha kuwa ni lazima ningepatikana na hatia.
Raisa aliniona nilivyokuwa nimegwaya, akaniuliza:
“Bado unajisikia kuumwa?”
“Bado naumwa. Hivi tunazungumza tu, lakini nahisi moyo wangu unakwenda mbio sana. Sijui ni presha?”
“Naona jasho pia linakutoka. Labda ni presha.”
Sikujua kama jasho lilikuwa limeanza kunitoka. Raisa aliponiambia hivyo ndipo nilipohisi kuwa uso wangu ulikuwa umejaa chembe za jasho.
“Basi nenda ukajipumzishe kitandani, acha niende zangu. Nitakupigia simu usiku kukujulia hali.”
“Sawa. Basi wewe nenda, acha nikalale kidogo.”
Raisa akaniaga na kuondoka.
Baada ya Raisa kuondoka, nikampigia simu baba na kumueleza alivyonieleza Raisa.
“Nilishakwambia, lolote linaweza kutokea. Kama utakamatwa, usikubali kuwa Shefa alifia nyumbani kwako na usikubali kwamba ulikwenda kuitupa maiti yake,” baba akaniambia kwa mkazo kwenye simu.
“Yule mlinzi wa nyumba ya jirani akiulizwa anaweza kusema alimuona akiingia nyumbani kwangu usiku wa siku ile aliyokuja kwangu.”
“Mlinzi alimuonaje wakati analinda kwenye nyumba nyingine?”
“Aliliacha gari kwake, na mimi niliwachungulia kupitia kwenye dirisha. Nikiona alikuwa anamuona wakati akiingia nyumbani kwangu. Atakapoulizwa, atasema aliingia nyumbani kwangu. Huo ni ushahidi ambao sitaweza kuukataa.”
“Mara ya kwanza uliniambia kuwa Shefa alikuja kwako ghafla na kubisha mlango usiku ukiwa umelala. Sasa hivi unaniambia ulimchungulia na ulimuona wakati alipokuwa anakuja, kama vile mlikuwa na makubaliano. Sasa tushike lipi?”
Nilikuwa nimesahau kwamba nilimwambia baba kuwa Shefa alikuja nyumbani kwangu na kugonga mlango, nikiwa nimelala.
Nikagwaya.
“Mwanangu, unatakiwa uwe na kauli moja. Unapokuwa na kauli zaidi ya moja katika jambo hilo hilo, ni sawa na kujipalia moto wewe mwenyewe. Hata wakili atashindwa kukutetea.”
“Basi nisamehe, baba. Nilighafilika kidogo,” ikabidi niombe msamaha.
“Sasa huyo Raisa si polisi wala si nani. Asikutie wasiwasi. Wewe kuwa kimya, uangalie kitakachotokea.”
“Sawa, baba.”
Nikakata simu. Nilikuwa nimefikiria nitoke niende saluni kwangu, mama akanipigia.
Nilipopokea simu yake akaniambia: “Huyo Raisa ni rafiki yako, kwanini hamui kitu kimoja?”
“Mama, sikiliza. Hili tukio linahusu mauaji. Mtu aliyeuawa pia yuko karibu sana na Raisa. Raisa nilishamficha tangu mwanzo. Nikianza sasa kumueleza ukweli hatanielewa,” nikamwambia mama.
“Maana yangu ni akijua kuwa ni wewe, hataendelea kufuatilia.”
“Acha tu, mama. Raisa siwezi kumueleza kitu. Kama alivyonieleza baba, nitakapokamatwa nikatae nilihusika.”
“Sawa. Nitajaribu kushauriana na baba yako, kama atakubali nije nilale na wewe huko.”
“Hapana. Mume wangu ameniambia atarudi leo. Nitakuwa naye.”
“Sasa kama ndiye mbaya wako kama alivyosema baba yako, itakuwaje?”
“Sidhani, lakini sijui. Moyo wa mtu ni msitu. Kilicho ndani huwezi kukijua. Lakini kama ndiye kweli, nitajua tu — tena nitajua leo. Ila ninachotaka kusema, namuamini sana mume wangu. Hawezi kufanya kitu kama hicho, tena Sufiani hana ujasiri kama huo.”
“Atakapokuja utamueleza kilichotokea?”
“Sitamueleza, kwa sababu nitazua maswali mengi. Nitamueleza tu kuwa rafiki yake amekutwa ameuawa.”
“Sasa sikiliza, lolote litakalotokea utatujulisha.”
“Sawa, mama.”
Nilipomaliza kuzungumza na mama, nilikwenda kuoga, nikavaa nguo nyingine kisha nikatoka kwenda saluni. Nilikuwa nataka kujichangamsha tu, kwani ninapokaa nyumbani peke yangu, mawazo hayaondoki kichwani mwangu.
Nilikwenda saluni kwa kutumia pikipiki ya bodaboda. Nilipofika, nikawasaidia wafanyakazi wangu kuhudumia wateja niliowakuta. Mpaka ilipofika saa kumi, Sufiani akanipigia simu.
“Nipo nyumbani,” akaniambia, na kuongeza: “Naona nyumba imefungwa, uko wapi?”
Nilishtuka kidogo kabla ya kumjibu.
“Niko saluni.”
“Una kazi nikufuate huko huko?”
“Nisubiri, ninakuja.”
Wakati huo nilikuwa nikipiga mahesabu na Suzana. Baada ya Suzana kunipa pesa za kazi walizofanya jana ambazo sikuwa nimezichukua, nikapanda bodaboda tena kurudi nyumbani.
Nilimkuta Sufiani amekaa barazani akiwa na begi lake.
“Habari ya safari?” nikamuuliza.
“Nzuri. Za hapa?”
“Za hapa ni nzuri. Ndiyo umeingia sasa hivi?”
“Niliingia muda kidogo, nilikuwa kwenye msiba.”
“Msiba wa nani?”
“Msiba wa Shefa.”
Nikashituka. Amejuaje kuwa Shefa amekufa wakati sikumwambia?
Nikafungua mlango tukaingia ndani.
“Mbona hapa dirishani pana tundu?” akaniuliza.
Lilikuwa ni lile tundu lililotobolewa na mtu aliyemuua Shefa.
Kwanza nikajiona nilikuwa mzembe kwa kughafilika kumuita fundi ili arekebishe mahali hapo tangu tundu hilo lilipotobolewa.
Nilifikiri kidogo na kugundua sikuwa mzembe kupaacha mahali hapo. Mbali ya kughafilika kutokana na mishemishe zilizonipata, pia nilitaka mahali hapo pabaki kama ushahidi endapo ningekamatwa.
Sufiani aliponiuliza swali hilo nilibabaika sana kumjibu. Sikujua ningemjibu nini.
“Hilo tundu lilitobolewa na wezi,” nikamwambia.
“Lilitobolewa na wezi? Hao wezi walikuja lini?”
“Juzi usiku. Walitoboa hapo halafu sijui walibadili mawazo wakaondoka.”
“Mmh! Siku hizi wezi wamechacha sana.”
“Yaani usalama umekuwa mdogo sana. Mtu ukilala una mawazo ya kuibiwa tu. Lakini nashukuru sikuibiwa kitu.”
“Sasa kwanini hujapatengeneza?”
“Ah! Ni mambo ya kusahau tu. Labda leo nitakwenda kumleta fundi apatengeze.”
Nililichukua lile begi la Sufiani nikaingia nalo chumbani. Mwenyewe akaketi sebuleni kwenye kochi. Nilitaka nilifungue begi hilo nilitazame ndani, lakini nikahisi kama vile mwenyewe anaweza kuingia. Nikaliacha na kutoka. Nikaenda kuketi naye.
“Unajisikiaje kuumwa?” nikamuuliza.
“Najisikia vizuri kidogo.”
“Ilikuwa ni malaria?”
“Nimeambiwa nina wadudu wanne.”
“Malaria nayo siku hizi, usiseme!”
“Ile sehemu niliyokuwa, ina mbu wengi sana. Si mimi peke yangu, watu wengi hupata malaria.”
“Enhee… aliyekwambia kuwa Shefa amekufa ni nani?”
“Kwani Shefa amekufa au ameuawa?” Sufiani akaniuliza.
“Nilivyosikia, ameuawa.”
“Aliyekwambia ni nani?”
“Habari zilitangazwa mpaka kwenye televisheni.”
Sufiani akanitazama vizuri usoni.
“Mbona hukuniambia kama rafiki yangu ameuawa?”
Bado Watatu – 31 | Mwanaspoti
