MSIMU uliopita ilibaki kidogo Fountain Gate ishuke daraja, lakini ikanusurika baada ya kuichapa Stand United katika mechi za mtoano.
Timu hiyo ilimaliza ligi katika nafasi ya 14, ikacheza mtoano wa kwanza dhidi ya Tanzania Prisons iliyomaliza ya 13, ikapoteza kwa jumla ya mabao 4-2 kwani nyumbani ilitoka 1-1, ugenini ikafungwa 3-1.
Ilipoenda kukabiliana na Stand United, Fountain Gate ikashinda kwa jumla ya mabao 5-1, kufuatia kushinda 3-1 ugenini na ushindi wa 2-0 nyumbani.
Wakati ikipambana isishuke, kuna maeneo matatu yalionekana kuiangusha Fountain Gate ambayo ni kufunga mabao, kujilinda na nidhamu ya wachezaji.
Katika mechi 30, Fountain Gate ilifunga mabao 32 na kuruhusu 58, ikiwa ndiyo timu ya pili kuruhusu mabao mengi zaidi ikitanguliwa na KenGold (62) iliyoshuka daraja.
Lakini pia timu hiyo ilikuwa na kadi nyekundu mbili walizoonyeshwa Abalkassim Suleiman na John Noble.
Kocha wa wakati huo, Robert Matano wakati msimu unaelekea ukingoni, alisema: “Timu yangu ina makosa mengi katika safu ya ulinzi, nina kazi kubwa kuhakikisha nayapunguza, bora timu isifunge lakini pia isiruhusu mabao.
“Kwa upande wetu tumekuwa tukifungwa zaidi ya kufunga, hili ni tatizo kubwa, bado tuna nafasi ya kufanya vizuri kwenye mechi zilizobaki ili kuinusuru timu.”
Hayo yamepita, sasa Fountain Gate inauanza ukurasa mpya ikiwa imekuja kivingine kwa kufanya maboresho kuanzia benchi la ufundi hadi wachezaji.

Kwa asilimia kubwa, kikosi cha Fountain Gate kina sura mpya nyingi akiwamo Obina Awara, Mussa Habeeb, Antony Nwadioha, Aziz Kada, Emmanuel Ihezuo, Chigozie Akabuike, Modou Camara, Falodun Onome, Joshua Ibrahim, Obasi McDonald na Jonathan Habakkuk.
Nyota walioondoka baadhi yao ni John Noble, Shafiq Batambuze, Laurian Makame, William Edgar, Salum Kihimbwa, Mtenje Albano na Said Mbatty.
Timu hiyo imefanikiwa kuwabakisha Jackson Shiga, Daniel Joram, Abdallah Kulandana, Anack Mtambi, Elie Mokono, Mudrick Shehe, Fadhil Kisunga na Ibrahim Parapanda.
Benchi la ufundi linaongozwa na kocha mkuu, Denis Kitambi, msaidizi wake ni Mohamed Ismail ‘Laizer’, huku Henry Joseph ni kocha wa viungo. Nahumu Muganda ni daktari na meneja wa timu yupo Zamkufo Elias ambaye msimu uliopita alikuwa mchezaji wa timu hiyo akicheza nafasi ya kiungo.
Akizungumza na Mwanaspoti kuhusu malengo na mikakati ya Fountain Gate, rais wa klabu hiyo, Japhet Makau anasema wakati wanamchukua Kitambi kuifundisha timu hiyo, walimpa masharti ya kuhakikisha timu inamaliza ndani ya nafasi sita za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara. “Tumetoka kwenye msimu ambao timu yetu haikufanya vizuri kabisa ambapo tumeponea kupitia mtoano, sio jambo ambalo tunalihitaji kabisa kama klabu.
“Mechi za mtoano zina changamoto nyingi na gharama kubwa, kwa hiyo jambo la kwanza tulilolifanya ni kuwa na timu bora itakayoleta ushindani msimu huu.
“Mwalimu tumempa changamoto ya kuhakikisha anamaliza ndani ya nafasi sita za juu kwenye ligi msimu huu,” anasema Makau.

Timu hiyo ambayo iemfanya usajili wa nyota wengi baada ya pia kuondoka wengi wakiwamo wale waliokuwa wakiunda kikosi cha kwanza, Makau anasema: “Kwanza sisi tunasajili kutokana na mapendekezo ya kocha, hatusajili kwa sababu kiongozi anamtaka mchezaji fulani kwenye timu, kocha anaangalia mahitaji, sokoni kuna watu gani na nani anaweza kutusaidia katika timu yetu. Mwalimu anapoona anamuhitaji mchezaji, anawasilisha kwa uongozi inafanyiwa kazi.
“Yote kwa yote, tumeongeza vijana katika timu yetu, tumeleta wachezaji wa kigeni ili kutoa changamoto na kufikia malengo, pia tuna wachezaji wazoefu wa ligi ya Tanzania, naamini mchanganyiko huu utatusaidia sana kuwa na timu bora sana katika msimu huu wa ligi.”
KAULI YA KOCHA DENIS KITAMBI
Jukumu alilopewa Denis Kitambi ndani ya kikosi cha Fountain Gate, kwake amelichukua kwa mikono miwili huku akisema ana kazi kubwa ya kufanya baada ya kufika na kugundua kikosi hicho kuna sehemu zina upungufu.
Kitambi ambaye ni kocha mzawa, ana uzoefu na Ligi Kuu Bara akifundisha timu kadhaa ikiwamo Simba, Namungo, Singida Black Stars na Geita Gold.
Akiwa na kibarua cha kuanza msimu nyumbani dhidi ya Mbeya City, Kitambi anasema: “Kila mchezo tunaouendea lengo ni kushinda, haijalishi uwe wa kwanza au wa 23, mpira wa miguu ni mchezo wa kushinda mechi, zile tano za kwanza tutajipanga vizuri ukizingatia tunaanzia nyumbani. “Kikubwa tusimdharau mpinzani wetu kwa kuwa amepanda daraja, cha msingi sisi wote tupo daraja moja. Cha kwanza ni kuhakikisha tunapata pointi tatu hapa nyumbani.”
“Tunawaahidi tutajituma sisi kama benchi la ufundi kuwaandaa vijana wetu ili waweze kupambana na changamoto za ligi, hicho ndicho ambacho ninaweza kusema, suala la kushinda ama kutoshinda linategemea na maandalizi. Kama unajiandaa vizuri una nafasi kubwa ya kushinda.
“Mimi sio mtabiri kwamba nitakwambia tutashinda, hapana, hakuna kocha ambaye ana uhakika wa ushindi ila ana imani kwamba nimeiandaa timu kwa ajili ya ushindi na hicho ndicho tunalenga kufanya.”