WAUAJI wa Kusini, Namungo walikuwa na kambi ya wiki mbili jijini Dodoma kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu, ambapo Mwanaspoti lilitinga kujionea namna nyota wa kikosi hicho wanavyojifua.
Lakini, unaambiwa kazi haikuishia mazoezini tu, bali kuna mipango na mikakati mizito inasukwa kwa ajili ya kujenga upya ubora katika kupambania nembo ya klabu hiyo yenye maskani yake wilayani Ruangwa mkoani Lindi.
Kumbuka kwamba, baada ya kambi fupi ya Dodomba timu hiyo ilisafiri hadi Babati, Manyara ilikoshiriki mashindano ya Tanzanite Pre Season International ambayo yalishirikisha timu 10, ambapo wauaji wa Kusini waliukosa ubingwa katika fainali ukienda kwa City FC Abuja ya Nigeria.
Mwanaspoti limepiga stori na uongozi pamoja na nahodha waliozungumzia mikakati na mipango, wakidai kwamba msimu huu mambo yatakuwa tofauti na ule uliopita.
Nahodha wa Namungo, Jacob Massawe anasema kama mambo yatakuwa ilivyokuwa wakati wa maandalizi ya msimu, basi mashabiki wao watarajie ushindani mkubwa kikosini na wategemee makubwa, na hasa kutokana na usajili mpya.
“Wachezaji wapya wanajiona kama wapo muda mrefu hapa kutokana na mapokezi waliyopata na mimi kama kiongozi wao nimekuwa nikiwaunganisha wote ili tujione wa wamoja,” anasema.
“Ushi-ndani umeonekana kwenye wiki hizi mbili, kila mchezaji anapambana kuonyesha anaweza ili aweze kupata nafasi ya kucheza kwa hiyo kina Machupa, Makambo wameongeza kitu kambini.”
“Tunaamini tulichokifanyia kazi mazoezini kitaenda kuonekana na kila mchezaji anatamani hasa wale wageni wapate nafasi ili waonyeshe uwezo kwa kocha.”
Nyota mpya kikosini, Heritier Makambo anasema hawezi kuifananisha Namungo na timu alizotoka, lakini anafurahia maisha ya kiuchezaji kikosini hapo.
“Kwa kweli kambi iko vizuri na nimefurahia kikubwa zaidi ni namna viongozi wanavyoelewana, wapo karibu na timu na kuhakikisha kila mmoja anakuwa na furaha,” anasema Makambo.

Akizungumzia mipango ya msimu mpya, Katibu wa timu hiyo, Ally Suleiman anasema msimu huu hawataki kupitia presha ya msimu uliopita ambao timu sita ikiwamo Namungo zilijikuta kwenye vita ya kuepuka kushuka huku hatma yao ikiwa ngumu.
Anasema mipango ni kubaki Ligi Kuu na ikitokea wakamaliza ndani ya nafasi tano za juu itakuwa vizuri zaidi kwao.
“Hatuwezi kusema kwamba tunautaka ubingwa lakini ikitokea sawa, malengo makuu msimu huu ni kuibakisha salama timu bila ya presha yoyote na tunatamani duru la kwanza tufanye vizuri,” anasema Suleiman
Katibu huyo anaongeza kuwa kwa kuhakikisha wanafanya vizuri msimu huu wameongeza wachezaji na kumbakiza kocha Juma Mgunda aliyeinusuru timu msimu uliopita.
“Tuliacha wachezaji 14 msimu uliopita ambao tuliamini hatutaweza kuendelea nao. Baada ya hapo tulipewa ripoti ya kocha kuongezewa wachezaji ambao tumefanya hivyo umeona kuna kina Heritier Makambo, Hussein Kazi wana uzoefu mkubwa na tunaamini wataongeza kitu.”
Ili ifanye vizuri wameandaa bajeti ya maana wakijiwekea kiasi cha Sh1 bilioni ili kuhakikisha timu inafanya vizuri na kutimiza malengo.
“Hiyo inajumuisha vitu vyote kwa maana ya kuwalipa mishahara wachezaji, makocha benchi la ufundi, usajili wa wachezaji, bonasi na usafiri wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine.”
Kocha mkuu wa Namungo, Juma Mgunda anasema walikuwa na maandalizi ya msimu mazuri wakipata mechi za kirafiki ambazo zilisaidia kuona sehemu ipi ina upungufu, lakini bado wanahitaji muda ili wachezaji wazoeane.

“Labda hadi tupate muunganiko kwa wachezaji wapya ambao walikotoka waungane waendane na falsafa na Namungo, mpira ni hatua na tunaamini tutafika, tunahitaji muda na baada ya muda mchache tutapata kile tulichokitarajia.
“Mashindano yalitusaidia sehemu iliyopungua, usajili mpya na wachezaji wapya wengi wametoka kwenye mifumo tofauti, malengo msimu huu ni kufanya vizuri na tunaamini tutafanya hilo.”
Miongoni mwa wachezaji wapya wa Namungo waliosajiliwa kuelekea msimu wa 2025-26 ni Seleman Said Abraham, Mussa Malika Mussa, Cyprian Kipenye, Andrew Chamungu, Ally Saleh Machupa, Rashida Mchelenga, Shafih Maulid, Abdulaziz Shahame, Lucas Kikoti, Herbet Lukindo, Abdallah Denis, Abdallah Mfuko na Hussein Kazi.
Kocha wa makipa wa kikosi hicho, Peter Manyika alisema msimu huu ataingia na mpango kazi maalum kuhakikisha lango la timu hiyo linakuwa salama zaidi, anapambana kuwaandaa vijana wake kuwa katika kiwango sawa chenye ubora.
“Bado tunawaandaa vijana na hata pre-season ilikuwa ya muda mchache ambayo hatukuwa na muda mrefu zaidi, wakati tunawaandaa makipa tuwe katika hali gani, unawaona kuna kitu, kazi yetu ni kurekebisha tu, tunaangalia msimu huu wataruhusu mabao mangapi.”
Kocha huyo ametua Namungo hivi karibuni baada ya msimu uliopita kuwa kwenye benchi la ufundi la Dodoma Jiji, timu iliyoruhusu mabao 49 katika mechi 30 za Ligi Kuu Bara.
Takwimu zinaonyesha kuwa, Namungo ambayo tayari imeshiriki misimu sita ndani ya Ligi Kuu Bara, imekuwa na wastani wa kuruhusu mabao 30+ kila msimu jambo ambalo ni hatari kwa timu yenye malengo makubwa.