WAKATI wadau na mashabiki wa soka nchini wakisubiri kwa hamu kuanza kwa msimu wa Ligi Kuu 2025/26, Tanzania Prisons imesema inakuja tofauti kupambania nafasi Top 4, huku ikiahidi ‘kibunda’ kwa mastaa wake.
Ligi Kuu Bara imeanza jana Septemba 17, ambapo Wajelajela hao watashuka uwanjani siku hiyo wakianzia ugenini dhidi ya Coastal Union, mchezo ukipigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Prisons yenye historia kubwa nchini kwa ukongwe na ubingwa wa mara moja wa Kombe la Muungano mwaka 1999, kwa misimu tofouti imekuwa na matokeo yasiyoeleweka sana.
Hata hivyo katika kusuka kikosi kipya kwa msimu ujao, vigogo wa timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Magereza nchini, waliamua kufanya mabadiliko kwa kuwahamisha watendaji.
Mabadiliko hayo yaligusa upande wa katibu mkuu, akihamishwa John Matei na nafasi yake kuchukuliwa na Godfrey Madegwa huku sehemu ya meneja, akiondoka Raulian Mpalile na kuingia Oraph Mwamlima.
Pia mabadiliko hayo yaligusa sehemu ya benchi la ufundi, wakiachana na aliyekuwa kocha mkuu, Aman Josiah na kumpa kazi Zedekiah Otieno raia wa Kenya, akiwa ndio mara ya kwanza kufanya kazi nchini.
Katika msimu uliopita, Maafande hao walikuwa na wakati mgumu katika kuepuka kushuka daraja, ambapo walisubiri hadi mechi za mchujo ‘(playoffs)’ dhidi ya Fountain na kubaki salama.
Katibu mtendaji wa timu hiyo, Madegwa anasema katika kuondokana na presha za matokeo ya mwisho, uongozi umefanya mikakati ya kutoa bonasi ili kuongeza ari, nguvu na motisha kwa wachezaji.
Bila kutaja kiwango, Madegwa anabainisha kuwa katika posho hizo nje ya mshahara, wachezaji watakuwa wakikunja dau tofauti kwa matokeo ya sare na ushindi.
“Hilo liko wazi, posho na bonasi ni sehemu ya utaratibu wetu, lakini kwa namna tulivyopania msimu ujao, lazima dau litaongezeka kwa ajili ya vijana kuongeza morali.
“Matokeo ya sare yatakuwa na kiwango chake, vivyo hivyo upande wa ushindi, hili ni katika kuondoa pia presha ya kusubiri matokeo ya mwisho kwenye ligi na kuweka presha ndani na nje ya uwanja.”
Staa wa timu hiyo, Lambart Sabiyanka amesema maandalizi waliyonayo na mabadiliko kikosini kwa sura mpya ni dalili njema kwao kufanya makubwa msimu ujao.
Anasema presha iliyojitokeza msimu uliopita hawatarajii yajirudie badala yake wanajipa mechi 10 za mwanzo kuvuna pointi 30 ili kuleta nguvu kikosini.
“Hatutahitaji kusubiri mechi za mwisho ndio tupate matokeo, tutaanza mechi 10 zile za mwanzo kukusanya pointi ili huko mbele tuondoe presha.”
Straika, Tariq Simba amesema mazoezi yanayoendelea yanatoa taswira, huku akieleza kuwa timu zilizokwenda kambini nje ya nchi haziwapi homa.
“Hatuwezi kuwabeza walioweka kambi nje ya nchi, kila mmoja anayetafuta mafanikio anahitaji utulivu, sisi hapa Kiwira pamekuwa bora kiusalama na mazoezi tunayazingatia sana,” anasema Simba.
Beki wa timu hiyo, Wema Sadock anasema wanahitaji kupambania jezi ya ‘Wajelajela’, akieleza kuwa watacheza ligi kwa kujitoa.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Otieono amesema baada ya kutua nchini katika kikosi hicho, ameona ubora wa wachezaji kwakuwa amehusika kusajili na kupendekeza, akitoa shukrani kwa uongozi kwa ushirikiano.
Amesema kambi ya Kiwira imetumika kuwaangalia ubora nyota wake na kutengeneza muunganiko.
“Kwa sasa tunaelekea block ya tatu ambayo inaonyesha ubora wa mchezaji kuseti mipango ya kiufundi, nashukuru kumekuwa na muunganiko wa vijana na sasa tunasubiri ligi,” anasema.
Otieno anasema licha ya kuwa ni mara yake ya kwanza kufanya kazi nchini, uwezo na uzoefu alionao utaamua hatma ya Prisons, huku akibainisha kuwa ni muumini ya ushindi.
Anasema anazifahamu timu kubwa nchini ikiwamo ni Yanga, Simba na Azam akifafanuwa kuwa hakuna ushindi wa pointi sita au moja, hivyo mkakati wake kila mechi ni ushindi.
“Kila timu ina uwezo wake, lakini ushindi wowote ni pointi tatu, kwa maana hiyo sitaangalia Simba, Yanga wala Azam badala yake yeyote tunayekutana naye tunahitaji ushindi, binafsi naamini kushinda kwa mabao” anasema kocha huyo.
Wachezaji watakaoichezea Prisons msimu huu ni Mussa Mbisa, Edward Mwakyusa, Marco Mhilu, Dotto Shaban, Wema Sadock, Lambart Sabiyanka, Haroun Chanongo, Aboubakari Segeja, Ismail Mtambo, Kelvin Sengati na Jeremiah Juma.
Wamo pia Oscar Mwajanga, Harriet Lulihoshi, Masoud Cabaye, Lucas Sendama, Never Kaboma, Omary Mbuji, Emanuel Mtumbuka, Isaya Kassanga na Michael Mutinda.