“SIMBA msimu uliopita tulitengeneza msingi lakini msimu huu ni wa kushinda makombe, dirisha la usajili limeshafungwa, nawaamini sana wachezaji wangu wote na nimefurahishwa na kikosi changu. Kama kocha nitapambana na kikosi hiki kutengeneza timu yenye ushindani msimu huu.”
Hayo ni maneno ya Kocha Mkuu wa Simba, Fadluraghman “Fadlu” Davids aliyoyasema mbele ya waandishi wa habari, Septemba 9, 2025 ikiwa ni siku moja kabla ya kufanyika kwa Tamasha la Simba Day. Kauli hiyo pia aliirudia wakati wa Simba Day, Simba ilipokuwa ikihitimisha tamasha hilo kwa kutambulisha kikosi cha msimu huu na kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Gor Mahia ya Kenya kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Huu ni msimu wa pili Fadlu anaiongoza Simba, baada ya ule wa kwanza kusema anajenga timu huku viongozi wakikubaliana naye. Katika kujenga timu, aliifikisha Simba fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, timu ikamaliza nafasi ya pili kwenye ligi nyuma ya Yanga, pia ikaishia nusu fainali ya Kombe la FA ikiondoshwa na Singida Black Stars.
Baada ya msimu wa kujenga timu huku Simba ikimaliza bila ya kombe lolote, sasa ni wakati wa kocha huyo na benchi zima la ufundi kutoa mbinu bora zitakazoifanya timu hiyo kubeba makombe.
Kumbuka Simba haijabeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo, ikiiacha Yanga ikitawala. Mara ya mwisho, Simba ilitwaa ubingwa wa ligi msimu wa 2020-2021 ambapo ilitawala misimu minne mfululizo kabla ya watani wao wa jadi kupindua meza.
Katika kuijenga Simba imara ambayo Fadlu anaamini itamfikisha kwenye kilele cha mafanikio, kuna wachezaji wapya wamesajili wakati wa dirisha kubwa lililofungwa Septemba 7, mwaka huu.
Wachezaji hao ni Yakoub Suleiman (kipa), Naby Camara (anacheza kiungo na beki), Vedastus Masinde (beki wa kati), Wilson Nangu (beki wa kati), Anthony Mligo (beki wa kushoto), Rushine De Reuck (beki wa kati), Alassane Kanté (kiungo wa kati), Morice Abraham (kiungo wa kati), Mohammed Bajaber (kiungo mshambuliaji), Hussein Semfuko (kiungo wa kati), Jonathan Sowah (mshambuliaji), Seleman Mwalimu (mshambuliaji) na Neo Maema (kiungo mshambuliaji). Pia kuna wachezaji watatu wamepandishwa timu ya wakubwa kutoka Simba U20 ambao ni Alexander Erasto, Ally Mbegu na Bashir Salum.
Kuingia kwa wachezaji hao, kulitoa nafasi kwa wengine kuondoka ambao ni Aishi Manula, Mohamed Hussein, Fabrice Ngoma, Valentine Nouma, Hussein Kazi, Augustine Okejepha, Kelvin Kijili, Debora Mavambo, Che Fondoh Malone, Edwin Balua, Ally Salim na Leonel Ateba. Pia Saleh Karabaka na Valentino Mashaka wametolewa kwa mkopo kwenda JKT Tanzania kama ilivyo kwa Omary Omary aliyepelekwa Mashujaa.
Ukiachana na wale vijana watatu waliopandishwa timu ya wakubwa ambao wataendelea kuingia ndani ya timu taratibu kwa kupata uzoefu, kuna majembe 28 ya kazi yaliyobeba dhamana ya kuipa mafanikio Simba.
Katika majembe hayo, kuna makipa watatu ambao ni Moussa Camara aliyemaliza msimu uliopita akiwa kinara wa clean sheet katika Ligi Kuu Bara akizikusanya 19. Wengine ni Husein Abel na Yakoub Suleiman ambaye ni ingizo jipya.
Kwa upande wa mabeki ni David Kameta, Anthony Mligo, Naby Camara, Abdulrazack Hamza, Rushine De Reuck, Chamou Karaboue, Vedastus Masinde, Wilson Nangu na Shomari Kapombe.
Viungo ni Yusuph Kagoma, Alassane Kante, Awesu Awesu, Morice Abraham, Kibu Denis, Hussein Daud Semfuko, Joshua Mutale, Mzamiru Yassin, Mohamed Bajaber, Ladack Chasambi, Neo Maema, Jean Charles Ahoua na Elie Mpanzu.
Safu ya ushambuliaji kuna Steven Mukwala, Seleman Mwalimu na Jonathan Sowah.
Fadlu Davids analiongoza benchi hilo la ufundi akiwa kocha mkuu huku wasaidizi wake ni Darian Wilken na Seleman Matola. Wayne Sandilands (Kocha wa Makipa), Riedoh Berdien (Kocha wa Viungo), Mueez Kajee (Mtathmini Mchezo), Patrick Rweyemamu (Meneja wa Timu), Hamis Mtambo (Mtunza Vifaa).