Mbeya. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amesema hakuna mgombea aliyepita bila kupingwa, na amewataka wagombea wa chama hicho kuendelea kusaka kura kwa wananchi nyumba kwa nyumba.
Amesema lengo la kusaka kura ni kuhakikisha ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 unapatikana.
Wasira ametoa kauli hiyo leo, Jumatano, Septemba 17, 2025, baada ya kuwasili katika Ofisi za CCM Mkoa wa Mbeya, ambapo amepokewa na viongozi mbalimbali akiwamo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutoka Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela, na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa.
Akizungumza na wanahabari nje ya ofisi za CCM kabla ya kuingia kwenye kikao cha ndani, Wasira amesema ziara yake mkoani Mbeya inalenga kufahamu hali ya kisiasa na maandalizi ya uchaguzi, kwa kuwa huu ni mwaka muhimu kwa chama na Taifa kwa ujumla.
“Nimefika kukutana na kamati ya siasa mkoa hakuna kupoa wala kulala, kwani baadhi ya majimbo tunakutana na viongozi wote wa matawi na kata ili tupeane majukumu namna ya kushinda sio kushindwa,” amesema.

Makamu Mwenyekiti CCM Bara, Stephen Wassira akisalimiana na mgombea mteule viti maalum Mkoa wa Mbeya Maryprisca Mahundi mara baada ya kuwasilisha katika Ofisi za Chama. Picha na Hawa Mathias
Amesema huu ni mwaka wa uchaguzi wagombea ubunge, udiwani waende wakasake kura kwa wananchi kwani hakuna mgombea aliyepita bila kupigwa.
Wasira, amewahimiza wanawake ndani ya CCM kuendelea na kampeni za nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anashinda kwa kishindo.
Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Nsalaga (Uyole), Clement Mwandemba, amesema wamepokea kwa mikono miwili maelekezo yaliyotolewa na Wasira na wapo tayari kutekeleza wajibu wao kwa bidii.
“Tumepokea maelekezo tumetakiwa kwenda kusaka kura usiku na mchana nyumba kwa nyumba, lakini pia tumeambiwa wazi hakuna mgombea aliyepita bila kupingwa,” amesema.
Amesema hatua hiyo inawapa hamasa ya kuongeza kasi ya kuhamasisha wananchi kupigia kura CCM na kushiriki katika uchaguzi Oktoba 29,2025 .