Mwajuma Mirambo: Mwanamichezo, mama lishe anayesaka funguo za Ikulu

Upo wakati inabidi kutuliza kichwa na kutafakari uzuri wa kile ulichonacho, kisha unamshukuru Mungu, halafu ndio unaomba kingine na kingine. Kanuni ni ile ile, anayepewa shukurani hutenda zaidi. Mungu huwajalia na kuwaruzuku zaidi wale wanaoshukuru kuliko wanavyoomba.

Mtanzania wa hali yoyote anaweza kuota ndoto ya kuwa kiongozi, huo ni uzuri wa Tanzania. Maskini au tajiri, inawezekana. Mzee au kijana, wana fursa sawa. Wanawake au wanaume, hakuna anayekatazwa kwa sababu za kijinsia. Ni matokeo ya nguvu ya demokrasia ya Tanzania. Ni umaridhawa wa utamaduni unaoongoza Jamhuri ya Muungano.

Mwajuma Noty Mirambo anaota ndoto ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni matokeo ya kutambua kuwa Tanzania yote yanawezekana. Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD) kimempa tiketi.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imemthibitisha. Sasa, Mwajuma yupo kwenye mapambano ya kuwashawishi Watanzania wampe funguo za kuingilia Ikulu baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.

Hadithi ya binadamu ni simulizi yenye mafumbo mengi katikati. Unaiona leo lakini huijui kesho. Jua linazama, giza linatanda, pakikucha ni siku nyingine unashangaa umekuwa toleo la tofauti. Ndivyo ilivyo kwa Mwajuma. Hakuwaza wala kutamani kuwa mwanasiasa hadi alipofikisha umri wa miaka 43.

Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, Mwajuma alichagua kuwa mfuatiliaji na shabiki. Alipenda harakati za vyama vya upinzani hasa Civic United Front (CUF). Alijiweka kwenye kundi la ufuasi, damu yake ni michezo. Ndilo eneo analolitumikia hadi sasa.

Waliotambua uwezo wake walimshawishi ajiunge kwenye siasa, ushawishi juu ya ushawishi. Leo hii Mwajuma anawania urais.

Mwajuma ni mwanamichezo. Amecheza mpira wa pete tangu akiwa shule ya msingi. Mchezo wa netball umempa hadi ajira ya kwanza. Ni zile nyakati ambazo vipaji vilithaminiwa na michezo ilikuwa nyenzo inayounganisha taasisi za Serikali, mashirika ya umma, vilevile nchi kupitia mashindano ya wilaya, mikoa na taifa. Mwajuma amepitia kote huko. Safari hiyo ndiyo imeunda wasifu alionao.

Julai 7, 1967, alizaliwa mtoto wa kike kwenye Hospitali ya Ocean Road, Magogoni, Dar es Salaam. Wazazi wake, Noty Sella Mirambo na Mwangaza Minshehe Kibinda, walimpa jina “Mwajuma.”

Akawa mtoto wa tatu miongoni mwa watatu wa familia ya Noty Sella Mirambo wa Mzimuni, Magomeni, Dar es Salaam.

Mwaka 1974, Mwajuma alianza darasa la kwanza Shule ya Msingi Mzimuni, Magomeni, na alihitimu elimu ya msingi mwaka 1980. Kuanzia 1981 mpaka 1984, alisoma kidato cha kwanza mpaka cha nne Shule ya Sekondari Kaole, Bagamoyo.

Baada ya kuhitimu elimu ya sekondari, alisoma kozi fupi za Ukatibu Muhtasi Chuo cha Baptist, Magomeni Kota, Dar es Salaam, kisha alijiunga na Chuo cha Msimbazi Centre, Dar es Salaam, kusoma utunzaji mizigo (storekeeping) mwaka 1984.

Mwajuma ni mwanamichezo kindakindaki. Tangu shule ya msingi na sekondari, alikuwa mchezaji mahiri wa netball. Mwishoni mwa masomo ya sekondari, Kiwanda cha Viatu Tanzania (Tanzania Shoes), kwa kuvutiwa na uwezo wake wa netball, kilimpa ajira kama karani wa Idara ya Ununuzi kuanzia Oktoba 1984 hadi 1987. Kipindi chote hicho, Mwajuma alikuwa mchezaji tegemeo wa timu ya kiwanda cha Tanzania Shoes.

Mwaka 1987, aliachana na ajira ya Tanzania Shoes na kuajiriwa na Kiwanda cha Nyuzi Ubungo, Dar es Salaam, alikitumikia hadi 1990, alipoamua kujiajiri. Mwaka huo huo, alifungua duka la nguo Mikumi, Lango la Jiji, Magomeni, Dar es Salaam, likiuza kanga, vitenge, na vipodozi. Duka hilo lilidumu hadi 2008, alipoamua kubadili biashara.

Hivi sasa, Mwajuma ni mama lishe, akifanya biashara ya chakula Tabata, Dar es Salaam, na vilevile ana duka la kuuza kanga na vitenge, soko la Karume, Ilala, Dar es Salaam. Hii ni kusherehesha kuwa tangu 1990 alipoacha ajira ya Kiwanda cha Nyuzi, hadi 2025, Mwajuma anatimiza miaka 35 ya ujasiriamali.

Maisha ya Mwajuma yamezungukwa zaidi na netball na soka la wanawake. Shule ya msingi, sekondari na timu za taasisi zilizomwajiri, Tanzania Shoes na Kiwanda cha Nyuzi, Mwajuma alicheza netball.

 Mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990, alipokea maombi mengi ya kuchezea timu mbalimbali, mialiko inayojulikana kama “ndondo.”

Mwajuma anamkumbuka Mwanaheri Ng’adu, aliyekuwa mfanyakazi wa Idara Kuu ya Watumishi wa Serikali, akisema alimwalika kwenda kucheza timu ya Idara Kuu ya Watumishi wa Serikali.

Walisafiri mikoa mbalimbali, na mkoani Tanga palibadilisha mtazamo wake. Mwanzoni mwa miaka ya 1990, timu za soka za Tanga, Coastal Union na African Sports, zilikuwa miongoni mwa chache Tanzania zilizo na soka la wanawake.

Mwajuma alipokuwa anakwenda Tanga kushiriki michezo, alivutiwa na soka la wanawake. Ni hapo ndipo alipoingia kama mchezaji. Bahati mbaya, ndoa ilikatisha ndoto yake ya kuendelea kuwa mcheza soka.

 Mwajuma anasema kuwa kwa mialiko ya “kupiga ndondo,” alishachezea timu ya netball ya Wizara ya Mambo ya Nje na Bohari Kuu ya Serikali. Mitaani kwao Magome, alicheza kwa nyakati tofauti timu za Tuwashukuru Wazazi, Young Sisters na Muungano.

Baada ya kujikita kwenye soka, Mwanaheri Ng’adu alianzisha timu ya soka la wanawake ya Sayari, makao makuu Magomeni Kota. Mwajuma alijiunga kama mchezaji, baadaye akachaguliwa kuwa meneja wa timu.

Mwaka 1994, Mwajuma alifunga ndoa. Mumewe alijua mwanamke anayetaka awe mkewe ni mchezaji wa soka, lakini baada ya ndoa, alimzuia kucheza mpira wa miguu.

Mumewe alimkatalia kucheza, lakini hakumzuia kuwa kiongozi wa timu ya soka. Mwajuma akawa meneja wa timu. Kisha, Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Manispaa ya Kinondoni (Kifa), Msafiri Mohammed, alimteua Mwajuma kuwa mjumbe wa Kifa.

Pamoja na hayo, Mwajuma ni mwelimishaji wa afya ya uzazi na Virusi vya Ukimwi (VVU). Alipewa mafunzo na taasisi ya Amref na kumjumisha katika mradi wa Zinduka kupitia soka, yaliyomwezesha kufundisha watoto wa kike kuhusu afya ya uzazi na VVU.

Mbali na ujumbe wa Kifa, ameshakuwa mjumbe wa Kamati wa Soka la Wanawake, Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), mjumbe wa Soka la Wanawake, Klabu ya Yanga, na mwaka 2019, aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Mshindo Msolla, alimteua Mwajuma kuwa Msimamizi wa timu ya Yanga Princess. Pia ameshakuwa kiongozi wa timu ya soka ya Mburahati Queens.

Kwa sasa, Mwajuma ni Katibu wa Umoja wa Wacheza Soka Wanawake Wastaafu. Kupitia uzoefu wake kama mchezaji na kiongozi, anatamba kwamba anaujua mwarobaini wa michezo Tanzani, hivyo akiwa Rais, taifa litapiga hatua za haraka kimichezo.

Mwaka 2010, alipokuwa Morogoro kwenye safari ya kimichezo, alipokea simu kutoka uongozi wa UMD. Uchaguzi Mkuu 2010 ulikuwa unapamba moto, UMD wakaona ilikuwa lazima Kata ya Mzimuni, Magomeni, wapate mgombea. Rafiki wa Mwajuma, Asma Hemed Mshamu, aliwaambia viongozi wa UMD: “Mtafuteni Mwajuma, yule siyo mwanasiasa, lakini anaweza kufanya siasa na kuwasaidia kushinda kata.”

Mwajuma aliporejea kutoka Morogoro, hakuwatafuta viongozi wa UMD. Asma aliwapa namba yake ya simu wampigie. Walizungumza, wakamshawishi, akashawishika. Akachukua kadi ya uanachama na akagombea udiwani Kata ya Mzimuni. Hakushinda, lakini kipaji cha siasa kilidhihirika.

Mwaka 2010, aliteuliwa kuwa Mratibu wa Wanawake UMD Mkoa wa Dar es Salaam. Mwaka 2011 hadi 2014, alikuwa Mratibu wa Wanawake UMD Tanzania Bara.

Mwaka 2015, aligombea na kushinda nafasi ya Uratibu wa Wanawake UMD Taifa, baada ya aliyekuwa Mratibu, Mary Osward Mpangala, kuomba kupumzika. Mwajuma anaendelea kutumikia nafasi ya Uratibu wa Wanawake Taifa kwa kipindi cha tatu.

Uchaguzi Mkuu 2025, UMD wameweka matumaini yao kwa Mwajuma, ambaye Uchaguzi Mkuu 2015, aligombea ubunge jimbo la Kinondoni. Uchaguzi mdogo wa ubunge Kinondoni uliofanyika Februari 17, 2028, Mwajuma aliwania. Mwaka 2020, aliwania ubunge jimbo la Ubungo. Majaribio yote aliyafanya kwa tiketi ya UMD, na hajawahi kuambulia chochote.

Shabaha ya kwanza ya Mwajuma ni kuhakikisha Watanzania wanajivunia kuzaliwa Tanzania, kwa kupata huduma bora za afya.

Mwajuma anasema, kwake, afya ni mtaji namba moja. Anataka aongoze nchi ili Serikali itoe elimu bora na siyo elimu duni. Anataka kilimo kiwe biashara na kiendeshwe kitaalamu. Ahadi yake ni kuhakikisha Serikali inatoa mazingira safi kwa kilimo.

Anasema, akiwa Rais wa Tanzania, kila mzawa atapata shughuli ya kufanya kwenye eneo lake, iwe kilimo, uchimbaji madini au biashara. Kauli mbiu yake kwenye ajira ni: “Mtanzania kwanza, mgeni baadaye.” Anasisitiza: “Nikiwa Rais, hakuna Mtanzania atajuta kuzaliwa Tanzania. UMD tutajenga taifa lenye faraja na furaha.”

Mwajuma ni mama wa familia. Mume wake anaitwa Omar Farijala Hemed. Kutoka tumboni mwake, Mwajuma amefanikiwa kupata mtoto mmoja, Hanifa Sembe Mohamed. Anaomba Watanzania wamuunge mkono, wasikilize sera na ahadi zake, na anaahidi utumishi uliotukuka kwa ajili ya Watanzania wote.