Mlinzi auwawa, mmoja ashikiliwa kwa mahojiano Shinyanga

Shinyanga. Mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Juma Mpuya (45) mkazi wa Ngokolo aliyekuwa akifanya kazi ya ulinzi katika Kampuni ya Shilo amekutwa ameuwawa usiku wa kuamkia leo Septemba 17, 2025 na watu wanaosadikiwa kuwa ni wezi kwa kupigwa na kitu kizito usoni.

Akizungumza na Mwananchi leo Septemba 17, 2025 Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo kata ya Ngokolo, Philemon Chikala amesema kuwa matukio kama hilo yamekuwa yakitokea  mara kwa mara katika mtaa huo na kuwataka wananchi kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenziye.

Mtendaji wa kata hiyo, Levania Josephat amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kufika kwa wakati katika eneo la tukio na kueleza kuwa wahalifu watakamatwa kwani Serikali ina mkono mrefu.

“Tumepata taarifa asubuhi tukafika eneo la tukio na kuwataarifu Polisi ambao walifika eneo la tukio na kufanya uchunguzi wao kisha wakachukua mwili wa marehemu na kuondoka nao kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” amesema Levina.

Aidha, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Amesema jeshi hilo mpaka sasa linamshikilia mtu mmoja kwa ajili ya mahojiano.

“Taarifa hizo tunazo mezani ambapo kwa uchunguzi wa awali tumegundua usiku wa kuamkia leo Septemba 17, 2025 mtu mmoja anayetambulika kwa jina la Juma Mpuya (45) ambaye alikuwa mlizi wa Kampuni ya Shilo amekutwa ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito usoni upande wa kulia,” amesema Magomi.

Amesema kuwa, “Kampuni za ulinzi zinatusaidia sana tunaposhirikiana kufanya ulinzi, lakini sasa dosari ni kuweka mlinzi mmoja kwa maduka saba kama ambavyo marehemu alikuwa akilinda na kutumia silaha aina ya rungu,” amesema Magomi.