Ahadi za wagombea zinatekelezeka? | Mwananchi

Dar es Salaam. Kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu, zimemaliza theluthi ya kwanza, majukwaa ya kisiasa yamegeuka uwanja wa matumaini, kila mgombea akiahidi mazuri kwa wananchi.

Ingawa ahadi hizo zinawapa matumaini wananchi kufikia matarajio na matamanio yao lakini kwa upande mwingine, zinaibua maswali nje ya majukwaa ya kisiasa, kwamba je, zinatekelezeka?

Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya siasa, inakuwa vigumu kupima utekelezwaji wa kinachoahidiwa, kwa kuwa hakuna nafasi ya wananchi kuhoji matokeo ya ahadi walizopewa wakati wa kampeni.

Wengine wamekwenda mbali zaidi na kueleza, hata ahadi zinazotolewa, baadhi hazina mazingira ya kupima utekelezwaji wake, ni maneno yasiyopimika iwapo yatatekelezwa au yataishia kwenye jukwaa la kampeni.

Kila msimu wa uchaguzi unapowadia, majukwaa ya siasa hubadilika kuwa viwanja vya matumaini. Wagombea wa urais hutumia nafasi hiyo kutoa ahadi zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja kuanzia elimu, afya wote, ajira na miundombinu.

Historia ya uchaguzi Tanzania inaonyesha mfano dhahiri wa ahadi ambazo hazijawahi kutekelezwa. Wakati fulani kumeshuhudia kauli mbiu za ‘maisha bora kwa kila Mtanzania.’

Hata hivyo, baada ya muda, changamoto za bajeti, ukosefu wa rasilimali na misukosuko ya kiuchumi duniani iliibua picha tofauti na matarajio ya wananchi.

Hili linaibua hoja ya msingi kwamba si kila ahadi ya kisiasa hujengwa juu ya misingi ya utafiti wa kiuchumi na mipango thabiti.

Mtaalamu wa uchumi, Profesa Benedict Mongula anasema ahadi yoyote ya kisiasa inayotolewa na mgombea wa urais hupaswa kulingana na uwezo wa bajeti ya nchi na vipaumbele vilivyoainishwa katika mipango ya kitaifa, kama Dira ya Maendeleo 2050 na Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano wa Maendeleo.

Anasema ikiwa ahadi zinapingana na takwimu za mapato ya ndani, deni la taifa, au uwezo wa kuvutia uwekezaji, utekelezaji wake huwa vigumu na mara nyingi hutengeneza hali ya wananchi kukata tamaa baada ya uchaguzi.

Anasisitiza ahadi zisizo na uchambuzi wa kifedha ni sawa na ndoto za mchana. Kwa mfano, kuahidi kuongeza mishahara ya watumishi wa umma kwa asilimia kubwa ndani ya kipindi kifupi bila kuonyesha chanzo cha mapato mapya ni kutengeneza pengo la bajeti.

“Ndiyo maana baadhi ya nchi jirani zimeshuhudia maandamano ya wananchi baada ya kugundua Serikali zao hazina uwezo wa kutimiza yale yaliyotamkwa kwa majukwaa ya kisiasa,” anaeleza Profesa Mongula.

Anasema ahadi zinazotekelezeka lazima ziwe na vigezo vitatu ambavyo ni mlinganyo wa ahadi na hali halisi ya uchumi, ziwe ndani ya uwezo wa kisera na kisheria na ziwe na muda wa utekelezaji unaoeleweka.

“Mwananchi anapopewa ahadi ya ajira milioni moja kwa mwaka, anapaswa kujiuliza je, sekta binafsi na umma zina miundombinu ya kuzalisha nafasi hizo kwa uhalisia? Bila majibu ya moja kwa moja, ahadi hizo zinabaki kama maneno ya kampeni badala ya dira ya maendeleo,” anaeleza.

Hata hivyo, anasema haimaanishi kuwa kila ahadi ni ndoto tupu, zipo zilizotekelezwa, hasa pale zinapojikita kwenye mpango mpana wa kitaifa na kupata uungwaji mkono wa kifedha na kisera.

“Ujenzi wa miundombinu mikubwa kama reli ya kisasa (SGR) na madaraja makubwa ni mifano inayoonyesha kuwa pale ambapo ahadi zinaambatana na vyanzo vya mapato na uongozi thabiti, ndoto za wananchi hubadilika kuwa uhalisia,” anafafanua Profesa Mongula.

Akizungumzia hilo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda anasema ni wajibu wa chama kuandaa ilani ili wananchi wasikilize sera.

Kinachohubiriwa kwenye mikutano ya kampeni, anasema ni ilani za vyama vya siasa, ingawa kuna wakati wagombea wanazungumza mambo yao binafsi, nje ya kilichomo kwenye ilani.

Lakini, anasema ni vigumu kujua iwapo ahadi zinatekelezeka au laa, kutokana na mazingira ya siasa za Tanzania. Siasa za nchini hazitoi mwanya wa wananchi kuhoji.

“Ilani ya 2020/25 ya CCM ilikuwa inasema inajenga barabara za juu kama 10 hapa Dar es Salaam, lakini hakuna hata moja iliyojengwa katika kipindi hicho, ilitakiwa wananchi wahoji,” anasema.

Anaeleza tatizo inaonekana wananchi hawajui kama wanaposikiliza ilani wanaingia kwenye mkataba na wagombea, hivyo wana wajibu wa kuhoji.

“Inawezekana hawajui kwamba wanaingia kwenye mkataba wa kijamii na wana mamlaka ya kuhoji kuhusu utekelezaji husika. Katika mazingira haya, ni vigumu kuona ahadi zikitekelezeka,” anasema.

Anasema mara nyingi uchaguzi wa Tanzania haujafikia viwango vya mkataba wa kijamii, kwa sababu wananchi hawana uwezo wa kuhoji na hawajui wahoji nini.

Dk Mbunda anasema kuna utafiti uliwahi kufanywa ukionyesha kuna idadi kubwa ya wafuasi kwenye chaguzi za Tanzania kuliko washiriki, hivyo wafuasi hawana uwezo wa kuhoji utekelezaji wa ilani.

Hata hivyo, anasema kuahidi ni jambo moja na utekelezaji ni jambo lingine, ilimradi ahadi zinatolewa zinapaswa kuaminiwa, isipokuwa kuwe na nafasi ya kumhoji yule atakayechaguliwa.

“Hiyo itafanya hata wakati mwingine mtu akitoa ahadi atajitathmini. Namna ya uwajibikaji huu ilipaswa kuongozwa na asasi za kiraia, lakini kwa namna zilivyo hapa nchini hakuna anayeweza kuhoji uwajibikaji,” anasema.

Anasema kwa hatua iliyofikiwa, kunatakiwa watu wapewe elimu kuhusu haki ya kuhoji utekelezwaji wa waliyoahidiwa wakati wa kampeni.

Dk Mbunda anasema ahadi yoyote ni sawa, isipokuwa muhimu ni kuwapo nafasi ya kuhojiwa iwapo atachaguliwa.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Kiama Mwaimu anasema ahadi nyingi zinazotolewa hazina mazingira ya kupimwa utekelezaji wake, isipokuwa wagombea wanaahidi kuwafurahisha wananchi.

“Suala lilikuwa kupatikana nafasi ya kuhoji mkakati wa utekelezaji wa kila kinachoahidiwa, wagombea wengi wangeshindwa, ambao wangemudu labda hawa waliokuwa kwa muda mrefu madarakani,” anasema.

Mwaimu anasema wagombea wengi wanazungumza ilimradi kuwafurahisha wasikilizaji.

“Bahati mbaya hatuna jukwaa la kuhoji utekelezaji wa ahadi, yanabaki kuwa maneno ya mdomoni, lakini kwenye utekelezaji patupu,” anasema.

Anasema labda ingesaidia iwapo kungekuwa na midahalo ya wagombea wa urais inayofanyika mbele ya umma, badala ya kuishia kusikilizwa na kusubiri matokeo.

Kampeni za urais nchini zimekuwa sehemu muhimu ya historia ya kisiasa tangu mwaka 1965, pale mfumo wa vyama vingi ulipofutwa na TANU kuibuka kama chama kimoja kilichokuwa na mamlaka ya kusimamisha wagombea.

Hata hivyo, uchaguzi wa mwaka 1995, baada ya kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, ndio uliweka msingi wa taswira ya kisasa ya kampeni za urais tunazoziona leo.

Katika uchaguzi wa pili wa vyama vingi, Benjamin Mkapa wa CCM aliibuka kidedea kwa kupata kura asilimia 61.8.

Katika kampeni zake, aliahidi mageuzi makubwa ya kiuchumi kupitia sera za ubinafsishaji na kuimarisha uchumi wa soko huria.

Ingawa baadhi ya mageuzi yalifanyika, kama kufunguliwa kwa milango ya uwekezaji na uliberali wa soko, wananchi wengi walibaki wakilalamikia ukosefu wa ajira, kufungwa kwa viwanda vya ndani na kushamiri kwa ukosefu wa usawa wa kipato.

Hapa ndipo taswira ya ahadi zisizotekelezeka ilipoanza kuonekana waziwazi.

Uchaguzi wa mwaka 2005 ulikuwa na mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete, ambaye alishinda kwa kishindo kwa kupata zaidi ya asilimia 80 ya kura.

Kampeni zake ziliibua hamasa kubwa, hasa kwa vijana, kutokana na ahadi za “maisha bora kwa kila Mtanzania.”

Aliahidi ajira milioni moja kwa vijana ndani ya miaka mitano, lakini takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu zilionyesha kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana kilibaki kuwa juu, kikipanda hadi asilimia 13 mwaka 2010.

Ingawa miradi ya miundombinu na huduma za kijamii iliongezeka, ajira zilizotokana na sekta hizo hazikuwiana na matarajio yaliyokuwapo kabla.

Mwaka 2015, John Magufuli aliingia ulingoni kwa kampeni zilizojaa kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu.” Aliahidi kuondoa ufisadi, kusimamia nidhamu ya kazi na kubana matumizi ya Serikali.

Kwa kiasi fulani, baadhi ya ahadi zake ziliwiana na vitendo, hasa katika kupambana na ufisadi na kuboresha nidhamu ya ukusanyaji mapato kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Hata hivyo, baadhi ya ahadi, kama ajira mpya kwa vijana na kuboresha hali ya maisha kwa kiwango kikubwa, hazikufikiwa.

Vilevile, ahadi za kisiasa za kuimarisha demokrasia zilishindwa, kwani kipindi chake kilishuhudia kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa kwa vyama vya upinzani.

Kwa jumla, historia ya kampeni za urais Tanzania inadhihirisha mzunguko wa matumaini na mashaka. Kila mgombea amekuwa akijenga hoja za kisiasa kwa msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, lakini mara nyingi utekelezaji umekwama kutokana na ukosefu wa rasilimali, mabadiliko ya kipaumbele, au mazingira mapya ya kisiasa na kiuchumi duniani.

Wapigakura wamebaki wakijifunza somo gumu kwamba si kila ahadi ya kisiasa huweza kutimia na kwamba kampeni mara nyingi huwa zaidi ni jukwaa la matumaini kuliko mkataba wa kisheria wa utekelezaji.