DKT.SAMIA AHUTUBIA MAELFU WANANCHI ZANZIBAR,AAHIDI KITUO CHA KUMBUKUMBU NA NYARAKA ZA MUUNGANO

Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Unguja

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa sasa umeimarika na umekuwa wa udugu wa damu  huku akiahidi Serikali kwenda kuanzisha kituo cha kumbukumbu na nyaraka za muungano.

Akihutubia maelfu ya wananchi wa Kusini Unguja leo Septemba 17,2025 pamoja na mambo mengine Dk.Samia ameeleza kuhusu kuimarika kwa muungano Tanganyika na Zanzibar.

Amesisitiza kwamba  kwa sasa muungano umeimarika na kuwa muungano wa undugu zaidi sambamba na kulinda uhuru na mapinduzi matukufu ya Zanzibar.

“Tumedumisha umoja, amani na utulivu nchini.Hizi ndizo tunu za msingi katika maendeleo ya Taifa letu.Kwa bidii zetu kubwa ni wahakikishie tunaendelea kulinda tunu za muungano, umoja, utulivu na amani ya nchi yetu,” alisisitiza.

Ameongeza tunu hizo ndizo zimejenga Taifa na utambulisho wa kipekee kimataifa kwani Tanzania imekuza uhusiano kidiplomasia, hivyo kuwa mbia muhimu mwenye kutegemewa duniani.

Mgombea huyo wa Urais alieleza kuwa hatua hiyo imefungua milango ya ushirikiano na fursa zaidi kwa Watanzania.

“Watanzania wapo huko duniani wakitembea kifua mbele na ikitajwa Tanzania wanakuuliza Mama Samia, hivyo nasi katika kijitahada za kuhifadhi urithi na kujenga uelewa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

“Tunakoendelea mbele tunakwenda kuanzisha kituo cha kumbukumbu na nyaraka za muungano wa Tanganyika na Zanzibar ili kiwe kituo ambacho vijana wetu na watu wanaotoka nje waingie, wasome na wajue kwamba muungano wetu una maana gani, ulianzaje na tunauendelezaje,” alisisitiza.

Kuhusu maendeleo amesema wote ambao wamezungumza katika mkutano huo wa kampeni amesema :”Kwa bahati nzuri neno kubwa walilolitumia ni hatuna deni na hawatudai. 

“Hawanidai mimi na hawamdai Rais Dk.Hussein Mwinyi. Na wapo tayari kutupa nafasi nyingine ili twende mbele tuwafanyie mazuri zaidi kwa hiyo hilinawashukuru sana.

“Maendeleo ndugu zangu ni hatua, tunaanza na hatua ya kwanza tunatekeleza tunapofikia na kila hatua zitakuwa zinakwenda.Hakuna awamu ambayo inamaliza maendeleo tukasema hapa tumefikia mwisho hatuhutaji kuendelea tena.

“Tutafanya kile tutakachojaaliwa na Mungu na wengine watakuja kuendeleza pale ambapo tutakuwa tumeishia.Kwa kuwa Watanzania tunazaana na tunakuwa, mahitaji wakati yote yapo na kila awamu ni wajibu kushughulikia.

“Tunawashukuru sana kwa ushirikiano mkubwa mliotupa Watanzania wote miaka mitano iliyopita na ukatuwezesha kufanya mazuri na makubwa tuliyoyafanya.Ushirikiano huohuo tunauomba huko tunakokwenda ili mazuri zaidi yapatikane.”