Unguja. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuzilinda tunu za Muungano, amani na utulivu wa Taifa kama walivyoziacha waasisi, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume, kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Pia, ameahidi kujenga kituo cha kumbukumbu na nyaraka za Muungano ili wageni wanaoitembelea Tanzania wajifunze kwa kusoma nyaraka mbalimbali zinazohusu Muungano huo kati ya Tanganyika na Zanzibar.
Samia ametoa ahadi hizo leo, Septemba 17, 2025, katika mkutano wa kampeni zake za uchaguzi uliofanyika Jimbo la Makunduchi, Kusini Unguja, sehemu ambayo ni nyumbani kwao.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo mgombea urais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro, pamoja na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zuberi Ali Maulid.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Samia amesema moja ya mafanikio yaliyopatikana katika miaka mitano iliyopita ni kuuenzi Muungano na kulinda amani na mshikamano wa Watanzania katika pande zote za Muungano.
Amesema mafungamano ya wananchi wa pande zote mbili yameendelea kukua kijamii, kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa, jambo ambalo limeimarisha Muungano huo na kujenga umoja wa Watanzania. Pia, amesema wamefanikiwa kulinda uhuru na Mapinduzi ya Matukufu ya Zanzibar.
“Naweza kusema sasa umekuwa Muungano wa undugu wa damu zaidi kuliko vigezo vingine vyote. Pamoja na Muungano wetu, tumeweza kulinda uhuru na Mapinduzi matukufu ya Zanzibar na kudumisha umoja, amani na utulivu nchini.
“Hizi ndizo tunu kuu na za msingi kwa maendeleo ya taifa letu na hizi niwaambie, tutazilinda kwa bidii zetu zote, tunakwenda kulinda tunu ya Muungano, amani na utulivu ndani ya nchi yetu,” amesema Samia.
Ameongeza kuwa sifa hizo ndizo zimejenga taifa la Tanzania, zimekuza uhusiano wa kidiplomasia na kufanya Tanzania kuwa mbia muhimu na wa kutegemewa duniani kote. Amesisitiza kwamba hiyo imefungua milango ya ushirikiano na fursa zaidi kwa ustawi wa Tanzania.
“Katika jitihada za kujenga uelewa wa Muungano, mkitupa ridhaa, tunakwenda kujenga kituo cha kumbukumbu na nyaraka za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ili kiwe kituo ambacho vijana wetu na wageni wote wanaokuja, waingie, wasome, wajue Muungano wetu ukoje, una maana gani, ulianzaje na tunauendesha vipi,” amesema mgombea huyo wa urais.
Samia ameowaomba Watanzania kudumisha amani na utulivu hasa wakati huu wa uchaguzi, akiwataka kupiga kura wakatulie nyumbani na wasikubali kurubuniwa na watu wanaotaka kuona amani inatoweka katika Taifa hili.
“Tunakwenda kwenye uchaguzi mkuu wa nchi yetu, ninawaomba sana, twende tudumishe amani na utulivu. Uchaguzi ni tendo la demokrasia. Si muda wote kushika silaha kunaleta suluhisho, niwaombe sana ndugu zangu, amani na utulivu wa nchi yetu ni jambo la muhimu kuliko vitu vyote hasa wakati huu wa uchaguzi.
“Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimejipanga vema kuilinda nchi yetu, kwa hiyo tukapige kura, tutulie nyumbani,” amesisitiza Samia.
Katika hatua nyingine, Samia amempongeza Dk Mwinyi kwa kazi kubwa aliyoifanya Zanzibar kwenye kila sekta, jambo lililomfanya aitwe ‘Mzee wa mabati’ kwa sababu kila sehemu ilikuwa ni ujenzi.
“Sasa tumeona mabati yameondokewa na kilichofanyika mmekiona… baada ya mabati, mkasi unaongea na mimi mwenyewe nilikuja kuzindua ile hoteli kubwa,” amesema.
Amewataka wagombea wengine kwenda kufanya kazi itakayotoa matokeo na kwamba wakati huu wa kampeni, wanapokwenda kuomba kura, waende kueleza yaliyofanyika na kueleza watakayofanya.
“Maendeleo ni hatua, tunaanza tulipoishia, tunaendelea mbele. Hakuna awamu iliyomaliza changamoto zote, hakuna. Kwa hiyo tutafanya sehemu yetu, watakaokuja wengine wataendeleza tulipoishia. Kwa kuwa watu wanazaliwa kila siku, changamoto mpya nazo zinajitokeza, kwa hiyo niwahakikishie tutafanya yale tuliyowaahidi,” amesema mgombea huyo.
Mgombea urais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, amehimiza amani, umoja na mshikamano katika nchi kwani bila hivyo, mengine yote hayatawezekana. Amewataka wananchi kuendelea kukiunga mkono CCM kwani ndicho kinahubiri amani.
Amesema chama hicho kimefanya kazi kubwa katika kutekeleza ilani ya uchaguzi ya 2020 na kwamba wataendelea kufanya makubwa katika miaka mitano ijayo.
“Wananchi mmekuwa mkifurika kwenye mikutano yetu, lakini hilo ni jambo moja. Nikuombeni, ikifika Oktoba 29, 2025, tujitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura ili kukipatia ushindi chama chetu. Siku hiyo ikifika, tutoke kwa wingi kupiga kura ili tushike dola,” amesema Dk Mwinyi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro, amesema ndani ya familia ndiko kunafanyika maridhiano ya msingi, na kwa Taifa, umekuja maridhiano katika 4R ulizozianzisha Samia, jitihada zake za kuleta maridhiano.
“Taifa limebadilika kulingana na mazingira, hivyo kwenye 4R zako umekuja na mageuzi katika kuboresha sheria na mifumo mingine ili kuweka mazingira katika hali bora zaidi.
“4R ni falsafa yako, 4R ni dira, na kuelekea kwenye Dira ya Taifa ya 2050, 4R zako ni njia nzuri ya kutufikisha huko,” amesema Dk Migiro wakati akichambua 4R za Samia katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Wagombea ubunge watia neno
Mgombea ubunge wa Makunduchi, Wanu Hafidh Ameir, amemkaribisha Samia nyumbani na kusema wananchi wa Makunduchi wamempokea kwa pongezi kwani “paka wa nyumbani hafukuzwi.”
Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, wanajivunia umoja na mshikamano uliopo nchini, kutokana na uongozi makini wa Samia na Dk Mwinyi.
“Mmefanya makubwa katika sekta ya uchumi, hasa hapa Zanzibar. Dk Mwinyi amefanya kazi kubwa, tunatarajia ataendelea kufanya makubwa katika miaka mitano,” amesema Wanu, ambaye pia ni mtoto wa Samia.
Kuhusu ajira, amesema vijana wengi wamepata ajira katika miradi mbalimbali na kwenye sekta za elimu na afya. Amesema wanatarajia makubwa zaidi kutoka kwa viongozi hao katika miaka mitano ijayo.
Ameongeza kuwa kwenye sekta ya afya, fedha za Uviko-19 zilizotolewa na Samia zimeleta mapinduzi makubwa katika ujenzi wa shule mpya, na Dk Mwinyi alisimamia kikamilifu, na sasa wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri.
“Kwa haya yote mliyotufanyia, tunakwenda kuwalipa kwa kuwapigia kura nyingi za kishindo ili muendeleze kazi kubwa mliyoianza. Niwahakikishie kwamba wananchi hawa watawapigia kura nyingi za kishindo,” amesema.
Mgombea ubunge wa Paje, Sanya Amir Sanya, amewataka Watanzania wote kumpigia kura Samia na Dk Mwinyi ifikapo Oktoba 29, ili waendelee kuwaletea maendeleo wananchi.
“Hapa Wilaya ya Kusini hatuna tatizo, unatudai na siku ya uchaguzi tunakwenda kukulipa kwa kura nyingi ili uendelee kutuongoza,” amesema mgombea huyo.
Mgombea ubunge wa Chwaka, Ramadan Maulid Ramadhan, amesema wameshuhudia kazi kubwa iliyofanywa na wagombea urais wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na wananchi wameona katika maeneo yao.
“Kazi kubwa mliyofanya inajieleza yenyewe, hatuna mashaka kwamba wananchi watakwenda kuwapigia kura kwenye uchaguzi ujao, bila kutusahau sisi wabunge na madiwani. Ushindi ni kwa Chama cha Mapinduzi,” amesema.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mohamed Ali Kawaida, amesema Zanzibar ilipokea Sh240 bilioni kutoka kwenye fedha za Uviko-19, Dk Mwinyi alizitumia vizuri katika ujenzi wa miundombinu ya elimu na afya.
“Wahenga wanasema ‘mcheza kwao hutunzwa’. Kwa kazi kubwa mliyofanya, Oktoba 29, 2025, tunakwenda kuwatunza kwenye sanduku la kura. Vijana hawa wameridhika na kazi mnayofanya, mnastahili kutunzwa,” amesema Kawaida.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Mohamed Dimwa, amesema wagombea wa urais wameboresha miundombinu kama barabara, jambo linalochochea ajira kwa vijana.
Amesema amani na utulivu ndiyo tunu ya Taifa, hivyo amemtaka kila mmoja ahakikishe amani inatawala kwani mambo mengine yote ya maendeleo yanafanyika pale ambapo kuna amani na utulivu.
“Ukikichagua CCM, umechagua maendeleo… wanasema sumu haionjwi, nenda ukaonje vitu vingine. Haikisheni mnajitomeza kwenda kupiga kura ili chama chetu kishinde kwa kishindo,” amesema Dimwa.