Waamua kuondokana na adha ya  kutembea kilomita 15 kufuata huduma za afya, Serikali yawaunga mkono

Tabora. Wananchi wa vijiji vitatu vilivyopo katika Kata ya Ugalla tarafa ya Ussoke Wilaya ya Urambo Mkoa wa Tabora, wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 15 kufuata huduma za afya ambapo ni zaidi ya miaka 20 wanaishi katika adha hiyo.

Wamebainisha adha hiyo leo Septemba 17, 2025 ambapo wameanzisha ujenzi wa kituo cha afya kwa nguvu zao ili kuitatua changamoto hiyo.

Ricado Daudi mkazi wa kata hiyo, ameiomba Serikali kuhakikisha inaunga mkono wananchi hao ili kituo hicho kiweze kukamilika kwa haraka, kwani uhitaji ni mkubwa.

“Sisi tunateseka sana kwa kweli na ni muda mrefu, yaani tuseme tu kuwa tunalazimika kupoteza muda mwingi hata kuwasindikiza wake zetu endapo huduma yake itashindikana kwa kiwango cha zahanati iliyopo, hivyo kulazimika kumpeleka kituo cha afya Ussoke,” amesema.

Esami Kegembe mkazi wa kata ya Ugalla amesema ikifika wakati wa mvua changamoto huzidi kuwa kubwa na hasa ikiwa kuna mama anayehitaji kupata huduma ya kujifungua kwa ngazi hiyo ya kituo cha afya.

“Yaani mke wako akiwa mjamzito mpaka unachanganyikiwa, maana unawaza ikitokea uchungu unauma itakuwaje mpaka tufikie huduma ya afya ya uhakika,” amesema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Mkoa wa Tabora, Grace Quintine amewapongeza wananchi kwa jitihada zao, akieleza kuwa Serikali imewaletea Sh250 milioni za awali kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho huku akiweka wazi kuwa itaendelea kuunga mkono juhudi hizo.

“Hii ni hatua kubwa mmefikia kikubwa tu ni kuendelea kuonyesha juhudi na uaminifu mkubwa na Serikali itawashika mkono, tunawaleteeni vifaa hapa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki, hivyo mvitunze na kuvilinda. Kituo hiki kinapaswa kukamilika kabla ya Novemba mwaka huu,” amesema Mkurugenzi huyo.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Nelson Majura amekiri wananchi wa eneo hilo kupitia changamoto hiyo na   Serikali tayari imeshaweka fedha kwa ajili ya kuunga mkono nguvu za wananchi.

“Tumeona juhudi zao na ni wazi kuwa wana kiu ya kupata kituo cha afya ili kupunguza adha wanayopata,” amesema.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Urambo, David Manyama amesema endapo kituo hicho kitakamilika kitakua cha tano kujengwa katika wilaya hiyo.

Amesema kitaanza kujengwa kwanza jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na vyoo vya kisasa ili wananchi waanze kupata huduma.