Kinapigwa leo Dabi ya Wanajeshi Lgi Kuu Bara

LIGI Kuu Bara inaendelea leo kwa michezo mitatu kupigwa, huku mechi ya mapema ikiwa ni saa 8:00 mchana kati ya Fountain Gate itakayoikaribisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, lakini pia kuna Dabi ya Wanajeshi, Mashujaa dhidi ya JKT Tanzania.

Fountain Gate inaingia katika mchezo huo ikiwa ni timu ambayo imetoka kucheza playoffs na kunusurika kushuka daraja msimu uliopita, inakutana na timu ambayo imerudi Ligi Kuu baada ya kushuka daraja na kukosekana misimu miwili nyuma.

Mchezo mwingine utapigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma ukiikutanisha Mashujaa na JKT Tanzania saa 10:15 jioni. Kisha saa 1:00 usiku ni Namungo ikiikaribisha Pamba Jiji kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.

Akizungumzia maandalizi yao, kocha mkuu wa Mashujaa, Salum Mayanga alisema hautokuwa mchezo mwepesi kwao ingawa malengo ni kupata pointi tatu huku akiainisha wachezaji wote wako kwenye morali kubwa ya kupata ushindi.

“Tunahitaji kuendeleza rekodi nzuri kwenye uwanja wetu na hili tutalifanikisha kwa kuzingatia nidhamu ya kiuchezaji kuanzia uzuiaji na utumiaji wa nafasi vizuri kwa maana ya ushambuliaji, pointi tatu ndio malengo yetu makubwa mchezo wetu wa kwanza tukiwa na faida ya kucheza nyumbani,” alisema.

Kocha wa JKT Tanzania, Ahmed Ally, alisema hawana rekodi nzuri kwenye uwanja huo lakini wamejiandaa ili kuanza vizuri na kujiweka kwenye mazingira mazuri mzunguko huu wa kwanza.

“Mara ya mwisho tulitoka suluhu, tunakutana na timu nzuri na ngumu, malengo ni kuweka rekodi nzuri kwenye mechi ya kwanza msimu huu,” alisema.

Kocha wa Mbeya City, Malale Hamsini alisema wamejiandaa vizuri kuwakabili wapinzani wao Fountain Gate wakiwa na malengo ya kuanza kwa ushindi licha ya kwamba watakuwa ugenini wataingia kwa kumuheshimu mpinzani wao.

“Tumetoka Championship, tunacheza mchezo wa kwanza wa ligi ugenini, haitakuwa rahisi lakini tumejiandaa kuhakikisha tunapata matokeo mazuri ili kujiweka kwenye nafasi nzuri, wachezaji wangu wapo tayari.”