Subira Mgalu Aahidi Kuboresha Afya, Maji na Barabara Bagamoyo

Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bagamoyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Subira Mgalu, ameahidi kuboresha huduma za afya, maji na miundombinu ya barabara endapo atapewa ridhaa ya kuwaongoza wananchi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni uliofanyika jimboni humo, Mgalu alisema ataweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha barabara zote katika kata 11 za jimbo hilo zinaboreshwa kwa kiwango cha lami.

Aidha, aliahidi kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo katika sekta za afya, elimu, maji, pamoja na kuboresha mifereji ya kisasa na huduma za kijamii.

“Tutahakikisha mradi mkubwa wa ujenzi wa bandari unatekelezwa kwa ufanisi ili kutoa fursa za ajira kwa wananchi wa Bagamoyo na kuchochea maendeleo ya kiuchumi,” alisema Mgalu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Martha Mlata, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, aliwataka wanachama na wananchi wa Bagamoyo kumpa Subira kura za kishindo kwa lengo la kuwaletea maendeleo.

“Wanabagomoyo mmepata mgombea mwenye uwezo mkubwa na ninamtambua kwa muda mrefu. Nina imani atatatua changamoto zenu na kuwaletea mabadiliko makubwa ya kimaendeleo,” alisema Mlata.

Naye Mgombea Ubunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani kupitia Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Hawa Mchafu, aliwataka wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kumpa kura nyingi Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Subira Mgalu na wagombea wa udiwani.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Aboubakar Mlawa, alisema chama hicho kimejiandaa kikamilifu kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao, huku akisisitiza mshikamano wa wanachama kuhakikisha ushindi huo unapatikana.

Uzinduzi huo uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama ulienda sambamba na kuwanadi wagombea wa nafasi ya urais, ubunge na udiwani.