Sekta ya madini ikipaa uharibifu wa mazingira, migogoro inatia doa

Dar es Salaam. Sekta ya madini imeendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi huku ikichangia asilimia 10.1 ya Pato la Taifa mwaka 2024 kutoka asilimia 9.1 mwaka 2023.

Hilo linashuhudiwa kupitia mauzo ya madini nje ya nchi yaliyofikia Dola bilioni 4.1 za Marekani huku dhahabu pekee ikiliingizia Taifa zaidi ya Dola bilioni 3.4 za Marekani.

Mbali na mapato sekta hii pia imetoa ajira kwa zaidi ya watu 19,000, huku asilimia 97 wakiwa ni Watanzania jambo lililoenda sambamba na kuchochea uwekezaji katika miundombinu na maendeleo ya viwanda vya kuongeza thamani.

Hata hivyo, changamoto kama uharibifu wa mazingira, migogoro, usimamizi wa haki za binadamu na usawa wa mgawanyo wa rasilimali bado zinahitaji suluhisho la kudumu.

Hiyo ni kutokana na baadhi ya maeneo kuendelea kukabiliwa na migogoro kati ya wananchi na wawekezaji, katika sekta ya madini hali ambayo wakati mwingine imekuwa ikikwamisha jitihada za uendelezaji wa sekta hiyo kwa kiasi kikubwa.

Mwenyekiti wa Chemba ya Wachimbaji madini Tanzania, Mhandisi Filbert Rweyemamu amesema mara zote shughuli za uchimbaji hazifanyiki bila kufuata sheria, hivyo malalamiko yanayotokea mara nyingi ni matokeo ya watu kukosa uelewa au kutoridhishwa na kile kilichokubaliwa kabla ya shughuli za uchimbaji kuanza.

Rweyemamu ambaye anazungumzia upande wa wawekezaji amesema shughuli za uchimbaji madini zimeidhinishwa katika katiba ya nchi kupitia sheria nne na hakuna uchimbaji unaofanyika bila sheria hizo kufuatwa.

Alizitaja sheria hizo kuwa ni ile ya Uhifadhi ya Mazingira ya mwaka 2004 na Sheria ya Madini 2010 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2017, Serikali za Mitaa ya 1982 ambayo inahusu ushirikishwaji wa jamii na Sheria ya Ardhi ya mwaka 1995 na Sheria ya ardhi ya vijiji mwaka 1999 ambayo inalinda haki za wananchi katika kuchukua ardhi.

“Shughuli zote za madini kuanzia utafiti ni lazima ziwe zimepita kwenye hatua hizo ikihusisha upatikanaji wa vibali ambavyo huwa havipatikani bila kuhusisha wananchi, na mamlaka zinazowalinda wananchi kwenye eneo husika.

“Hakuna uchimbaji utakaotokea bila kupitia ngazi zote. Malalamiko yapo ila cha msingi ni kwamba sheria za ardhi zinalinda haki ya jamii, hakuna namna utakiuka. Watu wanajadiliwa, wanahusishwa na kuna namna ya watu kuwasilisha malalamiko yao.

Anasema Sheria ya Hifadhi ya Mazingira inamlazimisha mwekezaji kupitia Serikali kujua vipaumbele vya wananchi ili kuhakikisha madhara yanayoweza kuletwa kutokana na uchimbaji yanazuiwa.

“Kampuni zinatakiwa kuwajibika yanapotokea malalamiko. Ila inawezekana malalamiko yanatokea kwa sababu hawana uelewa wa kutosha au waliyokubaliana hayakutimizwa”.

ili kuondoa hali hiyo anasema kwa mujibu wa taratibu kila mgodi una wajibu wa kuhakikisha wanatengeneza mfumo wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi katika eneo husika.

Anasema baada ya kupokea malalamiko hayo hufanyiwa utafiti na kutafutia suluhu kisha kurudisha majibu kwa wananchi.

Amesisitiza wahusika kuhakikisha wanaitumia mifumo hiyo kikamilifu kusikiliza na kutatua malalamiko ya wananchi.

Irene Mosha kutoka Taasisi ya Haki Rasilimali amesema ili sekta ya madini iendelee kukua huku haki za binadamu zikiendelea kulindwa kunahitaji ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, azaki pamoja na wadau wengine wa maendeleo.

Pia jamii kuhakikisha wanafuata na kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa katika shughuli za uchimbaji wa madini.

“Serikali ina wajibu wa kusimamia sheria na wachimbaji pamoja na jamii inayowazunguka wana wajibu wa kuhakikisha wanafuata sheria,” amesema.

Ameshauri mamlaka husika kuendelea kutoa elimu ya sheria kwa lugha rahisi kwa wachimbaji wadogo ili waweze kuzizingatia na kuzifuata.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Tanzania (Tawoma), Salma Ernest ameshauri wadau wa masuala ya madini na mazingira kushirikiana na serikali kuhakikisha wanatatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo.

Pia ameziomba taasisi za kifedha kuendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo ili waweze kuboresha shughuli zao.

Licha ya kuwa uchimbaji wa madini ni miongoni mwa shughuli zinazokimbiliwa na wengi hasa wachimbaji wadogo kundi hilo bado linakabiliwa na changamoto zinazoweka hatarini maisha yao.

Mojawapo ya changamoto hizo ni matumizi ya zebaki ambapo takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 71 ya uchimbaji unaofanyika nchini unahusisha matumizi ya zebaki.

Irene anasema kati ya migodi 237 iliyopo nchini matumizi ya zebaki yamebainika katika migodi 197.

“Asilimia 71 ya uchimbaji unaotumia zebaki uko karibu na makazi ya watu unaweza kupata picha ni madhara kiasi gani. Hii inatuambia kwamba bado kuna matumizi makubwa ya zebaki na athari zake ni kubwa. Ule mvuke unaharibu mapafu, ini, figo.”

Irene amesema wachimbaji wadogo wanawake ni waathirika wakubwa katika hilo ambapo takwimu zinaonesha wapo asilimia 40.

Anasema changamoto nyingine inayolikabili kundi hilo ni urasimu wa kupata vibali na leseni za uchimbaji hali inayosababisha wengi wao kufanya shughuli za uchimbaji bila kufuata taratibu.

Kukabiliana na hilo Irene amesema HakiRasilimali kwa kushirikiana na ubalozi wa Canada inatekeleza mradi unaowafundisha wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao kwa kuzingatia vigezo vya kimataifa.

“Huwa tunawapa elimu ni jinsi gani wanaweza kufuata viwango vya kimataifa, wakajipima. Ni muhimu kwao wajue ni kitu gani wanapaswa kufanya na wajumuishe katika sera na sheria.

“Mabadiliko mengi ya sheria yanatokana na wachimbaji wadogo hawana uelewa wa hayo yanayofanyika.”

Katika kushughulikia mambo mbalimbali ikiwamo migogoro kati ya wachimbaji na wananchi, Kaimu Kamishna wa Madini kutoka Wizara ya Madini, Terence Ngole anasema Serikali imekuwa ikihakikisha uchimbaji wa madini unafuata sheria zinazoongoza ufanyaji wa shughuli hizo.

Anasema lengo ni kuhakikisha masuala ya mazingira, jamii na usimamizi wa shughuli za uchimbaji wa madini zinafanyika katika utaratibu, kufanya hivyo itasaidia mazingira yanayofanyika shughuli hizo kubaki salama na wananchi wanaozunguka maeneo hayo kunufaika.

Ametolea mfano kabla ya mgodi kuanza kuchimba wahusika huwasilisha mpango wa uchimbaji ili kuhakikisha kama unakidhi viwango vya kimazingira na kiusalama.

“Kuna sheria inayosimamia wachimbaji wadogo ambayo inakataza kuajiri mtu mwenye chini ya miaka 18, lengo ni kuhakikisha haki za binadamu zinazingatiwa,” anasema.