Masista, dereva waliofariki ajalini waagwa Mwanza, viongozi watoa neno

Mwanza. Miili ya masista watatu na dereva wa Shirika la Masista Wakarmeli wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu Duniani imeagwa leo jijini Mwanza.

Miili hiyo imeagwa na mamia ya waamini wa Kanisa Katoliki, watawa, maaskofu, mapadre, wananchi na viongozi wa Serikali katika ibada maalumu iliyofanyika katika Kanisa la Epifania Bugando Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza.

Miili hiyo iliwasili kanisani hapo saa 1:20 asubuhi na kusomewa sala kabla ya kuingizwa kanisani kwa ibada ambayo ilikamilika saa 10:04 asubuhi, sala ya buriani kwa marehemu hao imetolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Renatus Nkwande.

Walioagwa ni Sista Lilian Kapongo aliyekuwa Mkuu wa Shirika hilo, Damaris Mbinya aliyekuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Bukumbi, sista Stellamaris Muthini na dereva, Boniphace Msonola.

Baadhi ya viongozi walioshiriki ibada hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Anna Makilagi, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Johari Samizi na  wawakilishi wa Jeshi la Polisi.

Baada ya ibada miili ya masista watatu imesafirishwa kwenda uwanja wa ndege Mwanza kwa ajili ya safari ya kwenda jijini Dar es Salaam ambako watapumzishwa kwenye nyumba zao za milele.

Ratiba iliyotolewa jana Septemba 17, 2025 na Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza inaonyesha misa ya mazishi ya wapendwa hao itafanyika Septemba 19, 2025 kuanzia saa 4:00 asubuhi katika Parokia ya Mwenyeheri Isidori Bakanja, Boko, Dar es Salaam, ikifuatiwa na ibada ya mazishi katika Kituo cha Kiroho cha Mtakatifu Teresa wa Avila Boko.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema Serikali ilitimiza wajibu wake katika kushughulikia tukio hilo hadi miili hiyo kuagwa kanisani hapo.

Akitoa salamu za pole kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan,  katika ibada ya kuaga miili hiyo, Mtanda amesema baada ya kupata taarifa za tukio hilo aliwaagiza Mkuu wa Wilaya ya Misungwi na Jeshi la Polisi kufika eneo la tukio haraka na kutoa msaada.

Mtanda amesema Serikali imesikitishwa na tukio hilo na inatoa pole kwa Kanisa Katoliki, Shirika la Masista walioondokewa na rafiki, ndugu na viongozi wao na kwa waumini wote wa Katoliki katika Jimbo Kuu la Mwanza.

“Tumesikitishwa sana na ajali hii, na  ilipotokea nilimwagiza Mkuu wa Wilaya alifika eneo la tukio mapema kabisa na Jeshi la Polisi na tulitimiza wajibu wetu, kwa hiyo tunatoa pole nyingi sana kwa  kanisa na kwa waumini wote poleni sana,” amesema Mtanda.

Naye, Mhashamu Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Renatus Kwande ameishukuru Serikali na watu wote waliofika wa kwanza eneo la ajali kutoa msaada wa haraka akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Misungwi na vyombo vya usalama.
‎”Tuzidi kuwaombea masista wetu Mwenyezi Mungu awapokea mbinguni.

Tumuombee dereva wetu alikuwa dereva mzuri, basi siku yakitokea ya kutokea kunaweza kuwa na maneno mengi laini yote hayo ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu,” amesema Baba Askofu Nkwande.

Nilikula na kukumbatiana nao

Akisimulia tukio la mwisho kukutana na marehemu hao, Askofu wa Jimbo Kuu la Musoma, Michael Msonganzila amesema mara ya mwisho alikutana na masista hao wote wanne Septemba 8,2025 katika eneo la St. Dominic jijini Mwanza na kula nao chakula, kukumbatiana na kubusiana.
‎Askofu Msonganzila ambaye pia ameongoza misa ya kuaga miili ya masista hao na dereva, amesema taarifa za kifo chao zimemkuta akiwa kwenye matibabu Mwanza.

“Binafsi nimeguswa sana na msiba huu, kwa kweli nimekutana na hawa wanne tarehe 8 hapo St. Dominic tukala chakula pamoja na uongo mbaya tukabusiana nao wote, sikujua kama ni chakula cha mwisho kati yao na mimi na hadi mabusu ya mwisho,” amesema Askofu Msonganzila.

Ameongeza kuwa; “Habari hii ya kufariki kwao imenikuta mimi niko hapa kwenye matibabu lakini basi ninaahidi kwamba ninaporudi Musoma baada ya Septemba 26, 2025 nafanya mpango tutaenda kusali misa ya pamoja hapo Butiama ambapo nyumba yao ipo. Mwenyezi Mungu awabariki sana awape nguvu za kustahimili tukio hili kwa moyo wa imani na matumaini.” 

Awali akitoa mahubiri, Askofu Msonganzila amesema: “Tusiishie tu kusikitika tuchukue hatua wasafiri na vyombo vya moto lakini pia Serikali ichukue hatua kwa kuboresha miundombinu ili matukio haya yasijirudie,” amesema Askofu Msonganzila 

Ameongeza kuwa; “Tunapoomboleza tunafundishwa katika historia yetu kwamba waliopatwa na magumu, na sisi tunapokuwa kwenye majonzi tutumainie kwamba mtetezi wetu Yu Mungu pekee.”

Askofu Msonganzila ametoa wito kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bukumbi kuendelea kujifunza utulivu na kumuomba Mungu awajalie kuyapokea magumu na kuishi kwa upendo bila matukio hayo kuwagawa.

“Ni kweli lilikuwa tukio baya la kushtukiza tunashukuru wana nzengo wa kijiji kile walitoa ushirikiano, nasi tukumbuke kufarijiana na kutiana moyo ili maisha yaendelee,” amesema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Bukumbi, Donald Magesa amesema; “Tumeshtushwa na kifo hiki na kwa kuwa tulikuwa karibu tulishiriki mambo mengi. Bodi inatoa pole kwa kanisa na jumuiya yote ya Bukumbi, kwa sababu mkuu wa shule aliyefariki alikuwa Katibu wa bodi.”

Akizungumza kwa niaba ya familia ya Boniphace Msonola, Veronica Haule (shemeji wa marehemu), amesema ndugu yao atazikwa kesho Ijumaa saa 8 mchana katika makaburi ya Sweya, Nyegezi jijini Mwanza.

“Kwa niaba ya familia ya Boniphace tunawashukuru watawa, waumini wote na baba Askofu tunapenda kuwakaribisha nyumbani kwake saa 8 mchana kule Sweya Nyegezi, Karibuni sana,” amesema Veronica.