TASAC YATOA MAFUNZO KWA WAMILIKI WA VYOMBO VYA USAFIRI MAJINI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) jana tarehe 16 Septemba, 2025 lilifanya mafunzo ya usalama na utunzaji wa mazingira majini kwa wadau wa usafiri majini  katika Mwalo wa Matema wilayani Kyela mkoani Mbeya. 

Elimu hiyo ililenga kuimarisha usalama wa usafiri majini katika Ziwa Nyasa ili kupunguza ajali na kulinda maisha ya wananchi wanaotegemea usafiri huo kwa biashara na shughuli zao za kila siku.

Akizungumza katika kikao cha uhamasishaji kilichofanyika ufukweni mwa Ziwa hilo, Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Mbeya, Naho. David Chiragi aliwataka wamiliki wa vyombo vidogo vya usafiri majini kuhakikisha wanazingatia kanuni na taratibu za uendeshaji wa vyombo hivyo kwa mujibu wa leseni zao.

“Tuzingatie matakwa ya leseni zetu ikiwemo kutofanya safari za usiku, safari zianze saa 12 asubuhi na kumalizika jioni ili kuepusha ajali zinazoweza kutokea gizani,” alisema Naho. Chiragi. 

Aliongeza kuwa abiria wanatakiwa kuvaa jaketi okozi muda wote wa safari, na kusisitiza kuwa katika usafiri majini hakuna ajali za bahati mbaya, bali ni uzembe na kutozingatia kanuni.

Kwa upande wake, Mkuu wa Bandari ya Matema, Bw. Beat Haule, aliwataka waendeshaji na wamiliki wa maboti kuhakikisha wanatimiza masharti yote yaliyowekwa na TASAC ili kufanya kazi kwa usalama na ufanisi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Maboti, Wilaya ya Kyela, Bw. Macarus Gowele, aliiomba Serikali kuwajengea miundombinu ya huduma katika maeneo yao ikiwemo vyoo na sehemu za kulala endapo wakikwama njiani hasa wakati wa mvua .

Wananchi na wamiliki wa vyombo vya usafiri majini walioshiriki kikao hicho waliipongeza TASAC kwa kutoa elimu hiyo, wakisema itasaidia kuimarisha usalama wa abiria na mizigo, kukuza biashara na kuendeleza shughuli za utalii katika eneo la fukwe ya Matema.