Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ameiomba Mahakama iwaamuru mawakili wa Jamhuri kumtambulisha yeye kama mshitakiwa na sio mwezao.
Amesema kuwa yeye ni mshitakiwa wa makosa ya uhaini hivyo, anapaswa kuitwa hivyo na sio mawakili hao kumuita mwenzao.
Lissu anakabiliwa na shitaka moja la uhaini katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, ametoa malalamiko hayo leo Alhamisi Septemba 18, 2025, muda mfupi kabla ya upande wa mashtaka kuanza kujibu hoja za pingamizi zilizowasilishwa na mshtakiwa huyo.
Amefikia hatua hiyo, baada ya kudai kuwa amekuwa akiitwa jina hilo mara kwa mara na mawakili wa Jamhuri, tangu kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani hapo.
Kabla ya kuanza usikilizwaji wa kesi hiyo, Lissu aliieleza mahakama hiyo mbele ya jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru (kiongozi wa jopo) James Karayemaha na Ferdnand Kihwonde, kuwa ana hoja mbili hivyo anaomba kuieleza mahakama hiyo.
“Jambo la kwanza ambalo huenda linaonekana dogo kwa wengine, lakini kwangu si jambo dogo, ni pale Wakili wa Serikali anaposema ‘mwenzetu, mwenzetu’. Mimi si mwenzao…mimi ni mshtakiwa wa uhaini, ningependa aniite mshtakiwa na sio mwezetu” alidai Lissu na kuongeza:
“Mawakili wa upande wa mashtaka nimeona tangu kesi ihamishiwe hapa Mahakama Kuu mara kwa mara, wamekuwa wakiniita jina hilo, hivyo mimi nataka niitwe mtuhumiwa.”
Hoja ya pili, Lissu amedai ni kuhusiana na kuhusiana na ombi la Septemba 4, 2025 alilolitoa mahakamami hapo la kuwezesha kesi hiyo itatangazwe mubashara kwa umma.
“Waheshimiwa majaji, tangu niwasilishe ombi langu kwenu hadi leo ni wiki ya pili sasa halijajibiwa. Hilo ni ombi langu kubwa, watu wanapigwa hapo nje wanaopokuja kusikiliza hii kesi ya uhaini, namna ya kuhakikisha adhaa hii ya kupigwa ni kutangaza kesi hii mubashara ili watu waweze kufuatilia wakiwa huko majumbani badala ya kuja hapa mahakamani na kupigwa,” alidai Lissu na kiomba majaji aliangalie hilo.
Baada ya kutoa malalamiko hayo, Jaji Ndunguru alielekeza upande wa mashtaka wamuite kama alivyoomba.
Akijibu malalamiko ya Lissu Wakili Mkuu wa Serikali Nassoro Katuga, alidai kuwa wamekuwa wakimuita kwa jina la mwenzao kwa kuwa ni wakili mwenzao.
“Tulikuwa tunamuita mwenzetu kuwa ni wakili mwenzetu na amekuwa wakili kwa miaka zaidi ya 25. Na ni mwenzetu kwa sababu ni parties katika kesi, bila yeye sisi hatupo, ila tutasikiliza maelezo ya mahakama itakavyotuelekeza,” alida Katuga.
Baada ha kusikiliza hoja za pande mbili, Jaji Nduguru alielekeza upande wa mashtaka watumie neno mshtakiwa badala la ‘mwenzetu’.
Kuhusu ombi la kesi hiyo kurushwa mubashara, Jaji Ndunguru alisema lipo ndani ya mamlaka ya Mahakama hivyo litaotolewa uamuzi,
Baada ya kutoa uamuzi huo, Jaji Nduguru aliruhusu upande wa Jamhuri kuanza kujibu hoja na pingamizi lililowasilishwa na mshtakiwa huyo Septemba 16, 2025.
Endelea kifuatilia mitandao ya kijamii ya Mwananchi