Taifa Stars yaanguka nafasi nne viwango FIFA

Dar es Salaam. Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeanguka kwa nafasi nne katika viwango vya ubora wa soka vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) vilivyotangazwa leo, Septemba 18, 2025.

Tanzania imedondoka kwa nafasi kutoka ya 103 ambayo ilikuwepo awali hadi nafasi ya 107 kwa viwango vilivyotolewa leo na FIFA.

Kufanya vibaya kwa Taifa Stars katika mechi mbili zilizopita za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026, kumeonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa kuiangusha katika viwango vipya vya ubora wa soka.

Katika mechi hizo, Taifa Stars ilitoka sare ya bao 1-1 na Congo ugenini kisha ikapoteza nyumbani kwa bao 1-0 mbele ya Niger.

Wakati Taifa Stars ikianguka, Uganda imezidi kupaa ambapo kwa mujibu wa chati ya sasa, ipo nafasi ya 82 kutoka ile ya 88 iliyokuwepo awali.

Kufanya vizuri katika mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Msumbiji na Somalia kumeonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa kuibeba Uganda ambayo imepanda kwa nafasi sita zaidi.

Kenya imeanguka kwa nafasi mbili kutoka ile ya 109 ambayo ilikuwepo katika chati ya mwezi Julai hadi katika nafasi ya 111 licha ya kupata ushindi mara moja na kupoteza moja katika mechi mbili za kuwania kufuzu Kombe la Dunia.

Morocco ndio timu bora kwa Afrika ikishika nafasi ya kwanza huku kidunia ikiwa katika nafasi ya 11 na kwa Afrika inayofuatia ni Senegal ambayo kidunia ni ya 18.

Kidunia kuna mabadiliko katika nafasi tatu za juu yanayozihusisha Argentina, Hispania na Ufaransa.

Hispania ambayo ilikuwa nafasi ya pili, imepanda hadi katika nafasi ya kwanza ikichukua nafasi ya Argentina ambayo imeshuka hadi nafasi ya tatu.

Ufaransa ilikuwa katika nafasi ya tatu, imesogea kwa nafasi moja hadi katika nafasi ya pili.