Hongera JKT Queens, Kenya wakubali tu

KIJIWE kinawapongeza Maafande wetu wa kike JKT Queens kwa kuibuka mabingwa wa mashindano ya kuwania kufuzu Klabu Bingwa Afrika 2025 yaliyofikia tamati Jumanne wiki hii huko Kenya.

Kwa kutwaa huko ubingwa, JKT Queens imejihakikishia tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake, shindano ambalo wiki kama mbili au tatu zijazo litafanyika Algeria likishirikisha klabu nane kutoka nchi na kanda tofauti za soka Afrika.

Kuna sababu mbili za msingi ambazo hapa kijiweni zinatulazimisha kupiga shangwe nyingi kwa JKT Queens kutokana na kile ambacho imekifanya kwa kwenda ugenini na kurudi ikiwa na taji na tiketi ya kufuzu ikiwa mkononi.

Sababu ya kwanza ni heshima ya Tanzania, inazidi kuboresha rekodi yake ya kuwa nchi ambayo klabu zake zimefuzu mara nyingi zaidi michuano ya Afrika kwa Wanawake kwa Kanda ya Afrika Mashariki na Kati na sasa ni mara ya tatu ikifuatiwa na Kenya na Ethiopia ambazo timu zao zimefuzu mara moja moja.

Ukiondoa hiyo, sababu nyingine ambayo imekifurahisha kijiwe ni JKT Queens imetwaa ubingwa huo katika ardhi ya Kenya tena kwa kuifunga timu mwenyeji katika hatua ya nusu fainali.

Ni kuwadhihirishia tu Kenya, bado soka lao linapaswa kufanya kazi ya ziada ili liweze kufikia ubora na thamani ya soka la Tanzania ambalo limepiga hatua kubwa ingawa majirani zetu hawataki kukubaliana na hilo.

Ushindi wa JKT Queens umekuja siku chache baada ya timu za Kenya kuonewa vilivyo na klabu za Tanzania katika mechi mbalimbali ambazo timu hizo zimekutana kwa kufungwa na ndani na nje ya ardhi ya Tanzania maana ndio imezika kabisa dhana ya kubahatisha.

Fikiria Pamba Jiji ilienda Kenya kwenye mashindano iliyoalikwa na timu ya Shabana kwa kuwafunga wenyeji, kisha Simba ikaifunga Gor Mahia na baadaye Yanga ikaichapa Bandari FC na pasipo kusahau Singida Black Stars iliifunga Police ya Kenya kwenye Kombe la Kagame.

Majirani wakubali tu tumewazidi kete kwenye boli. Timu zao tano tofauti kufungwa na zetu ni ishara ya sisi kuwa juu yao.