Kaizer Chiefs, Nabi shughuli imeisha

Taarifa kutoka Afrika Kusini zinabainisha kuwa, Kaizer Chiefs imefikia makubaliano ya kusitisha mkataba na kocha wake, Nasreddine Nabi.

Ripoti mbalimbali zilizochapishwa na vyombo vya habari nchini humo zinabainisha sababu ya Kaizer Chiefs kufikia uamuzi huo ni baada ya kubainika Nabi leseni yake ya ukocha ya CAF imekwisha muda wa matumizi, hivyo kumfanya asikubalike kuongoza timu katika mashindano ya kimataifa.

Habari hizo zimekuja huku Amakhosi ikijiandaa kucheza hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Kabuscorp SC ya Angola, Jumamosi wiki hii mjini Luanda.

Taarifa kutoka Afrika Kusini zinaeleza kuwa, uamuzi huo umetokana na kanuni za mashindnao yaliyopo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kuwataka makocha wakuu na wasaidizi kuwa na angalau Leseni A ya CAF ya ukocha.

Ingawa Nabi anamiliki Leseni ya UEFA Pro, ambayo ni sifa ya juu zaidi, pia tayari amewahi kuiongoza Yanga kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2022-2023 akikaa benchi akiwa kocha mkuu.

Hali ilizidi kuwa mbaya zaidi baada ya Chiefs kupokea kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Sekhukhune United mbele ya mashabiki wao kwenye Uwanja wa FNB, kipigo kilichozua sintofahamu juu ya mustakabali wake.

Kocha huyo raia wa Tunisia, alijiunga na Amakhosi Julai 2024 akitokea FAR Rabat ya Morocco, baada ya kutamba akiwa na Yanga ya Tanzania.

Ingawa msimu wake wa kwanza ulikuwa na changamoto, Nabi aliwavutia mashabiki kwa kukata kiu ya zaidi ya miaka 10 ya kutoshinda kombe, kwa kutwaa Kombe la Nedbank akiwafunga Orlando Pirates 2-1 kwenye fainali.

Vyanzo vya karibu na klabu hiyo vinaeleza kuwa imani kati ya pande hizo mbili ilianza kuyumba tangu walipokosa kumaliza nafasi nne za juu kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini msimu uliopita na suala la leseni limekuwa doa la mwisho.

Hata hivyo, taarifa zinasema Nabi amewasilisha leseni yake inayomruhusu kukaa benchi katika mashindano ya kimataifa, lakini Kaizer haikuonyesha nia ya kutaka kuendelea naye.

Kaizer inatarajiwa kutoa tamko rasmi kuthibitisha kuvunja mkataba na Nabi ambaye alikuwa amebakisha mwaka mmoja kuendelea kusalia kikosini hapo.