Nyota Twiga Stars apata dili Uturuki

MCHEZAJI wa timu ya taifa ya Wanawake ya Tanzania, Twiga Stars, Noela Luhala amejiunga naAntalyaSpor 1207 inayoshiriki Ligi Kuu ya Uturuki.

Noela ambaye msimu uliopita alikuwa akicheza Asa Tel Aviv ya Israel, alisafiri kwenda Uturuki jana tayari kuanza kuitumikia timu hiyo aliyosaini nayo mkataba wa mwaka mmoja ambao una kipengele cha kumruhusu kuondoka ifikapo Januari mwakani.

Staa huyu ambaye anaweza kucheza beki wa kati na kulia, anakuwa Mtanzania wa tatu kujiunga na timu inayoshiriki Ligi Kuu Uturuki baada ya Opah Clement na Diana Msewa.

Antalya ni miongoni mwa timu kongwe za ligi ya Wanawake na baada ya kushuka daraja msimu wa 2023/24, msimu uliopita ilichukua ubingwa wa Ligi Daraja la kwanza na kupanda daraja.

Noela ni miongoni mwa wachezaji walioiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la Dunia kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17, yaliyofanyika India mwaka 2022 na Tanzania ilitinga robo fainali.

Kabla ya kujiunga na timu hii, Noela alikuwa na ofa kadhaa ikiwemo ya Uzbekhstan, Israel na Mexico lakini badala yake aliamua kutimkia Uturuki.

Akizungumza na Mwanaspoti muda mchache kabla ya kusafiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalim Nyerere, Noela alisema nafasi hiyo kwake ni kubwa na atajitahidi kuhakikisha anaonyesha kiwango bora ili milango iendelee kufunguka.

“Hii nafasi ni nzuri sana kwangu kwenda kuonyesha, namshukuru sana Mungu kwa sababu bila ya yeye sidhani kama ningekuwa hapa leo.”

Staa huyu aliondoka Tanzania saa 10 Alfajiri ya Jumanne na kuwasili Istanbul Uturuki saa 6:00 mchana na aliunganisha ndege nyingine kwenda jijini Antalya ambako ndio makao makuu ya timu yake.

Ligi Kuu ya Wanawake Uturuki inatarajiwa kuanza Septemba 21, na Antalyaspor itakuwa na kibarua cha mechi ya kwanza dhidi ya Galatasaray itakayoanza saa 9:00 alasiri.