Taji la Kagame lampa mzuka Gamondi

KOCHA Mkuu wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi amesema taji la Kagame walilolitwaa litakuwa chachu ya kuiweka timu kwenye morali nzuri kuikabili Rayon Sports Jumamosi, Septemba 12, mwaka huu.

Gamondi alifunguka hayo saa chache baada ya timu yake ikiwa na nyota 26 kuanza safari ya kwenda Rwanda kuwafuata wapinzani wao kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, mchezo wa hatua ya kwanza.

Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi alisema timu yake ipo tayari na ina morali ya kuonyesha ushindani baada ya kutoka kutwaa taji kwenye mashindano ambayo ameyataja yameisaidia timu kutengeneza muunganiko, pia kuwaweka kwenye utimamu mzuri.

“Hautakuwa mchezo rahisi, tunaenda kukutana na timu bora ambayo pia ina wachezaji wazuri, lakini nafurahi nina timu nzuri ya kuonyesha ushindani na iliyojaa nyota wengi wazoefu na wenye uchu wa mafanikio na wamenithibitishia hilo kwenye michuano iliyopita tukitwaa taji la kwanza.”

“Mikakati yetu ni kuanza vizuri ugenini na kuja kumaliza mchezo nyumbani ili tuweze kuvuka hatua inayofuata hatutarajii urahisi tunajua mchezo utakuwa mgumu na wa ushindani dakika 90 ndio zitaamua nani bora zaidi ya mwingine wachezaji wangu wanafahamu umuhimu wa huo mchezo na wapo tayari kuipambania nembo ya klabu.”

Gamondi alisema amewafuatilia wapinzani wake kwa kuangalia mechi zao, pia kuangalia video za michezo yao wakiwa pamoja na timu yake anatambua ubora na udhaifu wa wapinzani atautumia ili kuweza kuipa matokeo timu yake.

Kikosi cha Singida Black Stars kilichoifuata Rayon Sports ni Metacha Mnata, Hussein Masalanga, Amos Obasogie, Kennedy Juma, Anthony Trabi, Mukrim Issa, Ande Koffi, Kelvin Kijili, Nockson Kibabage, Gadiel Michael, Morice Chikwu, Mohamed Damaro, Khalid Habib, Aboubakar Muhajiri.

Wengine ni Khalid Aucho, Idriss Diomonde, Kwame Keyekeh, Marouf Tchakei, Clatous Chama, Deus Kaseke, Rashid Saidi, Lamin Jarjou, Andrew Phiri, Daud Mishimo, Elvis Rupia na Horson Muaku.