Othman aahidi kukipa kipaumbele kilimo cha karafuu

Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman ameahidi kulivalia njuga zao la karafuu ili liwanufaishe wakulima na kuiingiza kipato Zanzibar.

Othman ambaye ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, ameeleza hayo Alhamisi Septemba 18, 2025 katika mwendelezo wa kampeni zake Pemba ambapo alipata fursa ya kuzungumza na wanakijiji pamoja na wajasiriamali wa karafuu eneo la Chokochoko. 

“Ni wakati mwafaka kwa wananchi wa Pemba kuanza kunufaika na rasilimali zao hususan zao la Karafuu. Tutalipa kipaumbele zao karafuu kwa kuweka mifumo bora ya kilimo, maandalizi ya shamba yatakayofanyika kwa utaalamu wa kisasa.

“Tutahakikisha bei ya karafuu inalindwa na kumnufaisha mkulima wa Pemba na Unguja. Karafuu imekuwa na thamani kubwa duniani, lakini faida yake haijawahi kumnufaisha mkubwa, ACT Wazalendo, tumedhamiria kuliboresha zao hili,” amesema Othman.

Amewataka Wazanzibari kukichagua ACT Wazalendo, kitakachounda Serikali mpya yenye heshima, itakayosikiliza wananchi na kuwaletea maendeleo ya kweli. 
“Karafuu ni uchumi wetu, lazima uchumi huu urejee mikononi mwa wananchi,” amesema Othman.