Dodoma. Watu tisa akiwamo dereva wa basi la abiria la Kampuni ya Abuu Trans, wamefariki dunia huku wengine 16 wakijeruhiwa baada ya basi linalofanya safari zake kati ya Dodoma na Kondoa, kupata ajali likitokea Kondoa kwenda Dodoma Mjini.
Chanzo cha ajali hiyo kinaelezwa ni dereva wa Fuso kutaka kulipita basi bila kuchukua tahadhari na kusababisha kugongana uso kwa uso katika eneo la Kambi ya Nyasa wilayani Chemba mkoani Dodoma, alfajiri ya kuamkia leo Alhamisi Septemba 18, 2025.
Katika ajali hiyo watu watano wamefariki dunia papo hapo na wengine wanne walifariki dunia wakati wanapelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kupatiwa matibabu.
Katika ajali hiyo, mtoto anayekadiriwa kuwa na umri chini ya mwaka mmoja amejeruhiwa, wazazi wake bado hawajatambuliwa.
Akizungumza leo na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Gallus Hyera amesema ajali hiyo ilitokea saa 12:40 na chanzo chake ni uzembe wa dereva wa lori, aliyepoteza mwelekeo na kuingia upande wa basi na kusababisha magari hayo kugongana uso kwa uso.
“Basi lilikuwa likitoka wilayani Kondoa kwenda Dodoma, huku lori likitokea Dodoma kwenda Kondoa. Dereva wa lori alihama upande wake wa kushoto na kuingia kulia, kisha magari hayo yakagongana uso kwa uso,” amesema Kamanda Hyera.
Amesema miongoni mwa waliopoteza maisha ni wanafunzi wanne aliowataja kuwa ni Carolyne Joachim (13), Rukia Ally (14), Bashir Hashim (13) na Nasra Mohamed (18).
Aidha, ametoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazotokana na uzembe.
Kamanda huyo amesema dereva wa lori ni miongoni mwa majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu na baada ya uchunguzi kukamilika, atafikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Ernest Ibenzi amesema walipokea taarifa za ajali saa nne asubuhi na wamepokea majeruhi tisa.
Dk Ibenzi amesema majeruhi hao wamepata majeraha mbalimbali mwilini ikiwemo mikononi, miguuni na kichwani, hata hivyo hali zao zinaendelea kuimarika baada ya kupatiwa matibabu ya awali.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ametoa wito kwa madereva kuhakikisha wanapumzika wanapohisi uchovu au usingizi ili kuepusha madhara.
Amesema ajali hiyo imetokea katika eneo lenye barabara nyoofu, jambo linaloashiria uzembe wa dereva.
Aidha, Senyamule amewashukuru wananchi waliotoa msaada wa haraka kwa majeruhi pamoja na watumishi wa afya waliowahudumia mapema na kuwasafirisha hadi hospitali ya mkoa.