Sh120 milioni kupoza maumivu kuungua Soko la Mashine Tatu

Wafanyabiashara 40 wa Soko la Mashine Tatu katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, waliopoteza bidhaa na mali zao kutokana na ajali ya moto, wamekabidhiwa Sh120 milioni ili kuwasaidia kujipanga upya na kurejesha biashara zao.

Fedha hizo, zilizotolewa na kampuni ya bima ya Reliance kwa kushirikiana na Benki ya NMB, ni fidia inayolenga kuwasaidia kurejesha mitaji na kuendeleza biashara zao, huku wafanyabiashara wengine wakihimizwa kujiunga na bima ili kujikinga na majanga ya aina hiyo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi hundi hiyo leo Alhamisi, Septemba 18, 2025, katika Soko la Mlandege, Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira), Dk Baghayo Saqware, amesema tukio hilo ni mfano halisi wa faida za kuwa na bima katika biashara, huku akiwataka wafanyabiashara kuendelea kutambua wajibu wao wa kulinda mali zao.

Amesema elimu ya bima ni muhimu kwa kuwa mara nyingi wafanyabiashara hujikuta kwenye shughuli za kila siku bila kuzingatia namna ya kujikinga na majanga yasiyotabirika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Reliance Insurance, Ravi Shankar, akiwa eneo la soko la Mlandege akizungumza na Wafanyabiashara ambao ni wanufaika wa fidia ya Sh 120 milioni baada ya soko la Mashine Tatu kuteketea kwa moto.picha na Christina Thobias

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Reliance Insurance, Ravi Shankar, amewashukuru wafanyabiashara hao kwa kujitokeza katika tukio hilo kwa kuwa linajenga mshikamano.

Amesema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara, huku akiwataka wasikate tamaa bali waendelee kuamini huduma za bima kama nguzo ya kulinda biashara.

Kwa upande wake, Ofisa Biashara wa Mkoa wa Iringa, Asifiwe Mwakibete, ameipongeza NMB na Reliance Insurance kwa mshikamano wao, akisema tukio hilo limewafungua macho wafanyabiashara wengi kuhusu umuhimu wa bima.

Asifiwe ameeleza kuwa mara nyingi wafanyabiashara hutambua thamani ya bima pale majanga yanapowapata, lakini ni vyema kuwa tayari mapema ili kupunguza madhara.

“Nawaomba viongozi wa taasisi za kifedha na bima kuendelea kutoa elimu endelevu. Pia niwatake wafanyabiashara waliopokea fidia hii kuwa mabalozi wa kuhamasisha wengine kujiunga,” amesema Asifiwe.

Rafael Ngulo, Mwenyekiti wa Umoja wa Masoko wa Manispaa ya Iringa, amesema tukio hilo limewafariji wafanyabiashara waliopoteza mali, kwani wengi walikuwa kwenye hali ngumu baada ya kuunguliwa bidhaa na mitaji.

Katika hatua nyingine, Ngulo ameongeza kuwa mshikamano uliooneshwa na taasisi hizo ni jambo la kuigwa, na wafanyabiashara wataendelea kushirikiana na taasisi hizo.

‎Mkuu wa Idara ya Bima kutoka Benki ya NMB, Martin Masawe,akiwa eneo la soko la Mlandege akizungumza na Wafanyabiashara ambao ni wanufaika wa fidia ya Sh 120 milioni baada ya soko la Mashine Tatu kuteketea kwa moto.picha na Christina Thobias

Mkuu wa idara ya bima kutoka NMB, Martin Masawe, amesema utaratibu wa madai kwa wafanyabiashara wa Iringa ulikuwa mwepesi, jambo lililoleta imani kubwa kwa wateja.

“Niseme tu kwamba bima za biashara huanzia Sh10,000 pekee na zinaweza kulipwa fidia ya hadi Sh500,000, hivyo kuwa nafuu kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati,” amesema.

Katika kulisisitiza suala hilo, Masawe amekiri kuwa benki hiyo itaendelea kutoa elimu ya kifedha kwa wafanyabiashara, na pia kuhamasisha mikopo kwa ajili ya kuongeza mitaji na kukuza biashara zao.

Miongoni mwa wafanyabiashara waliopokea hundi wameeleza kuwa fidia hiyo imewatoa kwenye hali ya hofu, kwani mali zote ziliungua moto, na sasa wanaweza kuanza upya biashara kwa ujasiri.

“Sijui niseme nini, lakini msaada huu wa fidia umenipa nguvu ya kurudi sokoni. Niwaombe wafanyabiashara wenzangu wasikate tamaa bali waendelee kuamini huduma za bima,” amesema Maria Ngoda, mfanyabiashara wa mali mbichi Soko la Mlandege.‎‎