Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mwanza, imeamuru kurudishwa kazini kwa aliyekuwa Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji, Dominic Adam, aliyefukuzwa kazi kutokana na mashtaka ya kinidhamu yaliyohusiana na kughushi vibali na stakabadhi.
Mahakama hiyo imeamuru arejeshwe kazini na kulipwa stahiki zake tangu alipofukuzwa kazi na iwapo ametimiza umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria alipwe stahiki zake kuanzia tarehe ya kufukuzwa kazi hadi tarehe ya kustaafu, pamoja na mafao yake kwa mujibu wa sheria.
Uamuzi huo umetolewa Septemba 17,2025 na Jaji Stanley Kamana, kufuatia maombi ya mapitio ya mahakama ya kupinga kufukuzwa kazi yaliyokuwa yamefunguliwa na Dominic na nakala ya uamuzi huo kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Maombi hayo ya madai yalifunguliwa dhidi wajibu maombi wanne ambao ni Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Dominic aliyekuwa katika Ofisi ya uhamiaji akiwa na cheo cha Mkaguzi Msaidizi, alifukuzwa kazi Aprili 14, 2020 baada ya kushtakiwa kwa tuhuma za kughushi vibali na stakabadhi.
Baada ya kufukuzwa kazi alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, kujibu mashtaka ya jinai yanayohusu makosa yaliyotajwa hapo juu, hata hivyo, mashtaka yalifutwa na upande wa Jamhuri, ambapo alijaribu kuomba kurejeshwa katika kazi yake ya awali hata hivyo jitihada zake ziligonga mwamba.
Jaji huyo amesema baada ya kupitia hoja za pande zote, amebaini mamlaka iliyomfukuza kazi haikuwa sahihi kisheria hivyo kubatilisha mwenendo na maamuzi ya kamati ya nidhamu yaliyotolewa dhidi ya mwombaji huyo, na kuamuru AG amrejeshe kazini bila kupoteza stahiki zake tangu alipoachishwa kazi.
Amesema iwapo Dominic amefika umri wa kustaafu anapaswa kulipwa stahiki zake kuanzia tarehe ya kufukuzwa kazi hadi tarehe ya kustaafu na mafao mengine kwa mujibu wa sheria.
Domonic aliiomba Mahakama kufanya uamuzi wa kesi zake za kinidhamu dhidi yake akiomba uamuzi wa mjibu maombi wa kwanza ambao ulimfukuza kazi, kumrejesha katika ajira yake kama Mkaguzi Msaidizi na kumlipa stahiki anazostahili za malipo, ambazo angepata tangu alipofukuzwa kazi.
Mwombaji huyo aliwakilishwa na Wakili Octavian Kamugisha ambaye alieleza kuwa mjibu maombi wa kwanza alikiuka masharti ya Kanuni ya 27(2) ya Tume hiyo.
Alieleza Mahakama kuwa mwombaji yuko chini ya mamlaka ya kinidhamu ya mjibu maombi wa tatu, ambaye ndiye awali alianzisha na kutoa uamuzi wa shauri la kinidhamu dhidi yake.
Wakili huyo alisema jukumu la mjibu maombi wa kwanza lilikuwa ni mamlaka ya rufaa na kuwa ilifanya kinyume na mamlaka yake ya kisheria kumfukuza mwombaji ilihali mjibu maombi wa pili ndiye mwenye mamlaka ya kumfukuza kazi.
Alihitimisha kuwa uamuzi wa kumfukuza mwombaji, kuwa haujatoka kwenye mamlaka inayostahili, ulifanywa bila mamlaka na haukubaliki kisheria.
Amefafanua kuwa baada ya kupitia mwenendo, mawasilisho ya hoja za pande zote mbili, masharti ya sheria na mamlaka zingine Jaji mahakama hiyo inajikuta ikiwa na wajibu wa kuamua masuala mawili, likiwamo kujiridhisha kama kufukuzwa kazi kwa mwombaji kulifanyika kwa mujibu wa sheria na wahusika wanastahili katika hali ya kesi hiyo.
Jaji Kamana amesema katika kushughulikia suala la kwanza ni vema akasisitiza kuwa masuala ya kinidhamu yanayowahusu maofisa wa uhamiaji yanasimamiwa na masharti ya Jeshi la Polisi, Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Sheria ya Tume ya Utumishi ya Uhamiaji.
Amesema kwa mujibu wa kifungu cha 7(3) cha Sheria tajwa, mamlaka ya nidhamu kwa maofisa wenye vyeo kuanzia Mkaguzi Msaidizi hadi Kamishna Msaidizi ni Inspekta Jenerali, ambapo mamlaka ya mwisho ya nidhamu ni ya mjibu maombi wa kwanza.
Jaji amesema tafsiri hiyo inaungwa mkono zaidi na Kanuni ya 27(2) ya Kanuni hizo, ambayo inatamka mjibu maombi wa kwanza anakuwa na mamlaka ya mwisho ya nidhamu na kuwa jukumu lake (mjibu maombi wa kwanza) ni la rufaa.
“Mjibu maombi wa kwanza alikosa mamlaka ya kisheria ya kumfukuza mwombaji, na kwa kufanya hivyo, alitenda makosa makubwa zaidi ya uwezo wake wa kisheria,”amesema Jaji.
Baada ya kupitia hoja za pande zote mbili kuhusu hoja hiyo, Jaji Kamana amesema Mahakama hiyo katika kutekeleza mamlaka yake ya usimamizi haijazuiliwa kutoa amri zinazofuata ikiwa ni pamoja na kurejeshwa kwa mwombaji kazini kwa nafasi aliyokuwa nayo kabla ya uamuzi unaopingwa.
Huku akinukuu mashauri mbalimbali yaliyowahi kutolewa na Mahakama ya Rufani, Jaji aliamuru mjibu maombi wa tatu (Kamishna Jenerali wa Uhamiaji) amrejeshe kazini Dominic bila kupoteza stahiki zake kuanzia tarehe aliyofukuzwa kazi.
Jaji amehitimisha kuwa iwapo mwombaji huyo ametimiza umri wa kustaafu, alipwe stahiki zake kuanzia tarehe ya kufukuzwa kazi hadi tarehe ya kustaafu na mafao yake ya kustaafu kwa mujibu wa sheria.