Dar es Salaam. Mabadiliko ya ratiba za wagombea yanayojitokeza mara kwa mara, ikiwemo kampeni za ghafla zinazofanyika nyumba kwa nyumba, yameelezwa kuwa changamoto kwa Jeshi la Polisi katika kutekeleza jukumu la kutoa ulinzi wa karibu kwa wagombea na wananchi.
Kauli ya Polisi imekuja wakati ambapo baadhi ya wagombea wanafanya kampeni za nyumba kwa nyumba za kusaka kura kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi limeelezwa namna ya kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu na sheria mbalimbali za nchi katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Akizungumza leo Septemba 18, 2025 Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Patience Ntwina amesema changamoto hiyo imebainika wakati wa kikao cha tathmini na mafunzo maalumu kwa wadau wa uchaguzi.
“Tumegundua kuwa mabadiliko ya ratiba yamekuwa yakileta ugumu kwa Jeshi la Polisi kutoa ulinzi kwa wakati. Hata hivyo, tunaona changamoto hizi ni ndogo na zinazoweza kudhibitiwa,” amesema Ntwina.
Amesema Tume imeanza mchakato wa kuwakumbusha wadau muhimu, ikiwemo Jeshi la Polisi na wanahabari, juu ya wajibu wao katika kusimamia haki za binadamu wakati wa uchaguzi.
Ntwina amesema Jeshi la Polisi lina jukumu kubwa la kuhakikisha wananchi na wagombea wanalindwa, huku wanahabari wakipewa jukumu la kutumia kalamu na vipaza sauti vyao kwa uadilifu katika kuelimisha umma bila kuchochea uvunjifu wa amani.
Kwa mujibu wake, mapokezi ya mafunzo kwa jeshi hilo yamekuwa mazuri, na matarajio ni kwamba tathmini hiyo itasaidia kuweka sawa masuala ya usimamizi wa uchaguzi, kudumisha amani na kuimarisha utulivu wa Taifa.
Aidha, amesema wiki ijayo Tume itakutana na wanahabari kwa lengo la kujadili nafasi yao katika mchakato wa uchaguzi, hasa namna ya kuhakikisha taarifa zinazotolewa zinabaki zikiwa na misingi ya haki za binadamu na utawala bora.
Kwa upande wake, Kamanda wa Kanda Maalum Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema mafunzo yaliyotolewa na THBUB yamelenga kuwakumbusha askari wajibu wao wa kisheria ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira ya amani na utulivu.
“Tume ya Haki za Binadamu imetukumbusha haki za wananchi kuchagua viongozi wanaowataka, haki ya kuchaguliwa, pamoja na wajibu wa kuhakikisha hakuna vitisho katika mchakato wa uchaguzi,”amesema Kamanda Muliro.
Pia amesema wamekumbushwa matumizi ya sheria, kuanzia zile za kimataifa ambazo Tanzania imeridhia, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya Vyama vya Siasa, Sheria za Uchaguzi na Sheria ya Jeshi la Polisi.
Muliro amesema katika mafunzo hayo askari wamekumbushwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, huku wakihakikisha usalama unaimarika kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
“Askari wetu wako vizuri na tumeendelea kusisitiza misingi ya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria. Maandalizi ya kiusalama ni ya hali ya juu na wananchi watekeleze majukumu yao ya kisiasa, kijamii na kiuchumi bila woga,” ameongeza.
Mbali na hayo, Muliro amesema madai ya uvunjifu wa amani ni propaganda za kisiasa na kusisitiza kuwa hali ya usalama katika Jiji la Dar es Salaam ni shwari.