BAO la Habib Kyombo dakika ya 56, limetosha kuipa Mbeya City ushindi wa 1-0 dhidi ya Fountain Gate katika mechi ya Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara.
Kyombo alifunga bao hilo kwa penalti baada ya Riphat Khamis kuchezewa faulo ndani ya eneo la hatari na Mudrick Abdi wa Fountain Gate katika harakati za kuokoa hatari.
Kabla ya kufunga bao hilo, Kyombo aliyewahi kuichezea Fountain Gate, Simba, Singida Black Stars na Pamba Jiji, alikuwa mchezaji hatari kwa wapinzani.
Kipindi cha kwanza ambacho kilimalizika kwa matokeo ya 0-0, Kyombo alikaribia kuiweka mbele Mbeya City, lakini shuti alilopiga liligonga nguzo na kurudi uwanjani.
Mbeya City ambayo imerejea Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kukosekana kwa misimu miwili mfululizo, imeanza vizuri mbio za kurudisha ubabe wake kama ilivyokuwa msimu wa kwanza 2013-2014 ilipomaliza nafasi ya tatu.
Kocha Malale Hamsini kwake huo ni mwanzo mzuri huku Denis Kitambi wa Fountain Gate akianza na mguu mbaya baada ya kukabidhiwa kikosi hicho.
Mchezo huo ni wa tatu tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara baada ya kushuhudiwa KMC ikiichapa Dodoma Jiji bao 1-0, kisha Coastal Union nayo kupata ushindi kama huo dhidi ya Tanzania Prisons.
Kikosi cha Fountain Gate kilianza hivi; Fadhil Kisuga, Shaaban Pandu, Daniel Joram, Elie Mokono, Abdallah Kulandana, Lamela Maneno, Sadick Ramadhan, Jackson Shiga, Mudrick Abdi, Shomari Mussa na Hassan Ally Mey.
Mbeya City walianza hivi; Beno Kakolanya, Ibrahim Ame, Yahaya Mbegu, Omary Chibada, Bakari Filemon, David Mwasa, Riphat Khamis, Mukrim Juma, Habib Kyombo, Eliud Ambokile na Vitalis Mayanga.