SINGIDA Black Stars ilianza kwa kusuasua sana mashindano ya Kombe la Kagame yaliyomalizika Jumatatu wiki hii kwa fainali baina yao na Al Hilal ya Sudan.
Na sio kama ilikuwa inacheza vibaya bali pale mbele haikuwa na mtu wa kulainisha. Pupa zilikuwa nyingi sana ilipokuwa inashambulia.
Ilionekana wazi Mwamba wa Lusaka ambaye alisajiliwa lakini akachelewa kujiunga na timu angekuwa suluhisho na hata Kocha Miguel Gamondi alikiri baada ya mchezo dhidi ya Ethiopian Coffee.
Ndicho kilichotokea katika mechi zilizofuata ambazo Chama alianza kucheza na timu ilionekana kuwa na floo nzuri pindi ilipokuwa inakaribia eneo la timu pinzani.
Chama hakuishia kulainisha timu pekee bali pia akafunga mabao matatu muhimu ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangia timu yake kutwaa ubingwa ww mashindano hayo jambo ambalo inalifanya kwa mara ya kwanza.
Alifunga moja katika mechi ya nusu fainali dhidi ya KMC ambayo walishinda kwa mabao 2-0 na katika mechi ya fainali akafunga mabao yote mawili yaliyoifanya timu yake ishinde kwa ma mabao 2-1 na mwisho ndiyo akawa Mfungaji Bora wa mashindano hayo.
Kijiwe kinaamini usajili wa Clatous Chama Mwamba wa Lusaka ni jambo zuri mno ambalo Singida Black Stars imelifanya kwani imemnasa mchezaji mzuri ambaye ataongeza kitu kikubwa katika kikosi chao kama watamtumia vizuri.
Uwezekano wa Chama kufanya vizuri akiwa na Singida Black Stars ni mkubwa kwa sababu hana presha kubwa kama ambayo alikuwa anakutana nayo alipokuwa Simba na baadaye alipojiunga na Yanga.
Katika soka mchezaji anapokuwa hana presha kubwa anakuwa na nafasi nzuri ya kucheza kwa kiwango bora kinyume na anapokuwa na presha kwani anakosa utulivu ambao unamsaidia kufanya uamuzi sahihi uwanjani.